NA MWANDISHI MAALUM
NEW YORK
Tanzania imechaguliwa kuwa kati ya nchi 41 zitakazounda Bodi ya kwanza ya Wakurugenzi watakaosimamia Chombo kipya cha Umoja wa Mataifa kijulikanacho kama UN WOMEN kitakachojihusisha na masuala yote yanayohusu maendeleo ya wanawake.
Uchaguzi wa kuzipata nchi hizo 41 , umefanywa na wajumbe wa Baraza la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Uchumi na Jamii (ECOSOC)katika kikao chake kilichofanyika mwishoni mwa wiki.
Ili kupata idadi hiyo ya nchi zitakazounda Bodi ya kwanza, ECOSOC iliweka utaratibu rasmi wa kugawa viti kwa kuzingatia makundi matano. Makundi hayo ni kundi la nchi za Afrika lililopewa viti 10, kundi la nchi za Asia lililopewa viti 10, kundi la Ulaya Mashariki lililopewa viti vinne na kundi la Amerika ya Latini na Visiwa vya Caribbean wao walipata viti sita.
Aidha Baraza hilo pia lilitenga viti vingine sita ambavyo vilitolewa kwa nchi ambazo zimejitokeza kuwa wachangiaji wakubwa wa chombo hicho.
Kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na ECOSOC,Wakurugenzi wa Bodi hiyo watadumu kwa vipindi vya miaka kati ya miwili na miaka mitatu. Na Tanzania itakuwa ndani ya Bodi hiyo kwa miaka miwili. Uamuzi wa nchi gani ikae ndani ya Bodi kwa miaka mitatu au miwili ulifanywa kwa njia ya kura ya siri.
Nchi nyingine zinazounda Bodi hiyo ni Angola, Argetina, Bangladesh, Brazil, Cape Verde, China, Kongo, Cote D’Ivore, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Denmark, Jamhuri ya Dominica, El Salvador, Ethiopia, Estonia, Ufaransa, Grenada, Hungary na India.
Nyingine ni Indonesia, Italia, Japan, Kazakhstan, Lesotho, Libya, Luxembourg, Malaysia, Mexico, Nigeria, Norway, Pakistan, Jamhuri ya Korea, Urusi, Saudi Arabia, Spain, Sweden, Timor-Leste, Ukraine, Uingereza na Marekani.
Katika kugawana viti hivyo kumi, kundi la Afrika lilivigawa tena viti hivyo kwa Kanda yaani kanda ya Afrika Mashariki, Kanda ya Afrika ya Kusini, Kanda ya Afrika ya Kati, Kanda ya Afrika Magharibi na Kanda ya kaskazini.
Kanda ya Afrika Mashariki ilipewa viti viwili na nchi zilizojitokeza kuomba nafasi hizo zilikuwa ni Tanzania, Kenya, Ethiopia, Mauritius na Djibout. Katika mzunguko wa kwanza Ethiopia ilipata nafasi ya kunyakua kiti kimoja kati ya viwili ili hali Mauritius na Djibout walijitoa
Mpambano wa kuwania kiti kilichobaki ulibaki kuwa kati ya Tanzania na Kenya ambapo Mabalozi wa nchi hizo, walipambana vikali kwa kujenga hoja zakutetea ni kwanini nchi yake ilistahili kupata kiti hicho.
Baada ya vuta nikuvute iliyodumu kwa saa tatu ndani ya kikao cha mabalozi wa kundi la Afrika ambao ndio waliokuwa wakipitisha waombaji kabla ya kuteuliwa na ECOSOC, hatimaye Tanzania iliibuka kidedea.
UN- Women ni chombo kilichoundwa kuchukua kazi na majukumu yote yahusuyo mausuala ya wanawake yaliyokuwa yakifanywa na taasisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa na kilipitishwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Julai mwaka huu , na kitanza rasmi kazi mwezi Januari mwakani.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269