Breaking News

Your Ad Spot

Jan 26, 2011

NGO ZINAZOJINUFAISHA KUPITIA MATATIZO YA WANAWAKE ZISIPEWE NAFASI-TANZANIA

Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue, akizungumza wakati wa mkutano wa kwanza wa Bodi ya Chombo kipya cha Umoja wa Matiafa kijulikanacho kama UN Women, chenye jukumu la kushughulikia matatizo ya wanawake katika nyanja mbalimbali zikiwemo za maendeleo, uwasa na jinsia, uwezeshwaji, Elimu, nafasi mbalimbali za uongozi, Ulinzi, Amani na Usalama na vitendo vya ukatili dhidi yao. Tanzania ni kati ya nchi kumi za Afrika ambazo ni wajumbe wa Bodi ya chombo hicho. Aliyekaa nyuma ya Balozi ni Meshacrk Ndaskoi, Mkurugenzi wa Idara ya Jinsia na Maendeleo katika Wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia na watoto.
====================================================================
HABARI KAMILI

Na Mwandishi Maalum, NEW YORK


Tanzania imeutaka Umoja wa Mataifa kutozikumbatia taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) zinazolenga kujinufaisha kupitia matatizo ya wanawake.


Tanzania imetoa wito huo kupitia Balozi wake katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Bodi ya Chombo kipya cha Umoja wa Mataifa, kinachoshughulikia masuala ya wanawake maarufu kama UN-WOMEN.


Akizungumza katika mkutano huo wa siku tatu, ambao Tanzania ni kati ya nchi za kwanza zinazounda Bodi ya UN-WOMEN. Balozi Sefue anasema wakati Tanzania ikiunga mkono na kukaribisha ushirikiano wa wadau mbalimbali zikiwamo NGOs katika kuchagiza maendeleo na haki za wanawake, tahadhari ichukuliwe dhidi ya wale wanaotaka kujinufisha kupitia matatizo ya wanawake.


“tunakaribisha wazo hili la kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwamo NGOs, na hasa wale ambao kweli wamedhamiria kuonyesha kwa vitendo nia hiyo na si wale wanaolenga kujinufaisha wao” akasisitiza Balozi.


Aidha Mwakilishi huyo wa Tanzania katika UN, amekitaka Chombo hicho kipya katika ujumla wake, kuhakikisha kinakidhi kiu na matarajio ya nchi wanachama na hasa wanawake.


Anaeleza kuwa ni vema watendaji wa Chombo hicho ambacho kimechukua majukumu ya taasisi nyingine nne za UN zilizokuwa zikihusika na masuala ya wanawake. Kwamba licha ya kuwa wabunifu na wanaojituma, lakini pia wanapashwa kuyatambua kwa kujielemisha mazingira watakayofanyia kazi.


Anafafanua kwa kusema. Kila nchi inachangamoto zake linapokuja suala la kushughulikia haki, usawa na maendeleo ya wanawake. Na kwamba kila nchi ina mila, desturi na tamaduni zake, hivyo ni vema watendaji wa Chombo hicho wakayajua na kuyazingatia hayo.


Balozi Sefue anaeleza kuwa ni vema pia Chombo hicho katika utekelezaji wa majukumu yake na hasa kwa kuzingatia kwamba kitalenga zaidi kufanya kazi ndani ya kila nchi husika, kwamba kikazingatia mipango mkakati ya kila nchi na vipaumbele ambavyo nchi hizo imevichagua.


“ Kila nchi inachangamoto zake, kila nchi ina mila na taratibu zake, na kila nchi imejipangia program zake na kuchagua vipaumbele vyake, kwa hiyo ni muhimu sana kwa Chombo hiki kufanya kazi kwa ukaribu sana na serikali husika ” akasisitiza Balozi.


Akatumia nafasi hiyo kuelezea hatua mbalimbali za kisera, kisheria na kimipango ambazo zimefanywa na serikali ya Tanzania katika kutatua kero za wanawake.


Akasema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameonyesha utashi mkubwa wa kisiasa katika kushughulika haki za wanawake na kwamba utashi huo hauishi kwa Rais tu bali hata kwa viongozi wengine wa Serikali.


Pamoja na mambo mengine akasema Tanzania imejitahidi sana kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za utoaji wa maamuzi.


Kwa mfano, akasema kupitia juhudi hizo za serikali, Tanzania hivi sasa Spika wake wa Bunge ni mwanamke, imeazisha Benki ya wanawake, pamoja na kutoa nafasi sawa za kielimu kwa watoto wa kike na wakiume.


Hata hivyo amesema pamoja na mafanikio hayo na mengine mengi Tanzania bado ina safari ndefu katika utekelezi wa mipango ya kuwasaidia wanawake.


Akasema ni matumaini ya Tanzania ya kufanya kazi kwa karibu na Chombo hicho katika kuongeza kasi ya kushughulikia matatizo ya wanawake katika Nyanja mbalimbali.


Awali Mkurugenzi Mtendaji wa UN-WOMEN Madam Michelle Bachelete ambaye aliwahi kuwa Rais wa Jamhuri ya Chile. Aliainisha mbele ya wajumbe wa Bodi vipaumbele vinavyotakiwa kutekelezwa katika siku mia moja pamoja na mipango kazi ya baadaye ya Chombo hicho.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages