Breaking News

Your Ad Spot

Feb 13, 2011

TUWAPE MATUMAINI VIJANA KUEPUSHA VURUGU-TANZANIA

Na Mwadishi Maalum, New York
Tanzania imeshauri kwamba ili kuliepusha Bara la Afrika na Dunia kwa ujumla na vitendo vya uvunjifu wa amani, ni vema vijana wakapewa matumaini ya kuwa na maisha bora.


Hayo yamesemwa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue, wakati Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipokutana mwishoni mwa wiki, kujadili uhusiano uliopo kati ya usalama na maendeleo.


Katika hali ambayo wanadiplomasia waliiona si ya kawaida na kuibua hisia mbalimbali, Baraza hilo lilitenga siku nzima ya ijumaa kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu udhibiti wa amani na usalama. na uhusiano uliopo kati ya suala zima la usalama na maendeleo.


Mada hiyo ilipendekezwa na Brazil, nchi ambayo kwa mwezi huu wa February ndiyo Rais wa Baraza hilo.


Mwakilishi huyo wa Tanzania, amewaeleza washiriki wa mjadala huo uliofunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ukiwashirisha pia wawakilishi wa Bank ya Dunia, na baadhi ya mawaziri kwamba,


“ Ni jambo lililodhahiri kuwa kukata tamaa, kunyimwa fursa, na ufukara na hasa miongoni mwa vijana, ni chachu tosha ya tishio kwa amani na usalama katika nchi moja moja na dunia kwa ujumla”


Akasema vitendo vya uhalifu kama vile biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji wa binadamu , uharamia, ugadi na uhamiaji haramu ni matokeo ya umaskini.


Balozi Sefue amebainisha katika hoja yake kwamba, suala la usalama ni la msingi sana kwa maendeleo, na maendeleo kimsingi ni usalama na Baraza hilo haliwezi kulikwepa hilo.


Anasema “Kwa kuwapa matumaini vijana wa Afrika, matumaini ya kuwa na maisha bora huko mbeleni, kutasaidia sana kupunguza shinikizo la kuwapo kwa vitendo vinavyoweza kupelekea uvunjifu wa amani, uhalifu na migogoro”.


Akaongeza kuwa watu wanatakiwa kushirikishwa katika suala zima la usalama na maendeleo yao, katika njia sahihi na bora itakayoimarisha amani na kuibua mazingira sahihi ya utawala bora, na kuheshimu haki za binadamu.


Awali akifungua mjadala huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, hakusita kueleza bayana kwamba, matukio kadha ambayo yamekuwa yakiendelea katika baadhi ya nchi katika siku za hivi karibuni yalikuwa ujumbe mzito kuwa hali ya mambo si shwari.


Anasema Ban Ki Moon. “ Matukio ya hivi karibuni duniani, yanabeba ujumbe mzito kwamba, kunahitajio la kuwapo kwa utulivu wa kisasa unaojikita katika amani, fursa sawa, uhakika wa maisha bora na matakwa ya wale wanaotawaliwa”.


Akasema amani, usalama na maendeleo ni mambo yanayohusiana au kutegemeana. Na ushahidi unaonyesha wazi kuwa katika kipindi cha miaka 20, nchi nchi tisa kati ya kumi ambazo viwango vya maendeleo viko chini zimekubwa na migogoro.


Aidha akasema, nchi ambazo wananchi wake hawana fursa sawa, huku taasisi zake zikiwa dhaifu ziko katika hatari kubwa ya kutumbukia katika migogoro.


“ Mgawanyo usio sawa wa raslimali, ukosefu wa nafasi za ajira, fursa na uhuru na hasa kwa idadi kubwa ya vijana kunaweza kuwa chimbuko kubwa la uvinjifu wa amani” anasisitiza Ban Ki Moon.


Akawaeleza wajumbe wa mjadala huo kwamba, kama ukosefu wa maendeleo unaweza kuwasha moto wa machafuko, halikadharika kuwapo kwa uchumi imara na maendeleo ya kijamii, kunaweza kupunguza mlipuko wa mioto hiyo na hivyo kuwapo kwa hali ya amani.


Karibu wajumbe wote waliochangia mjadala huo, Tanzania ikiwamo, licha ya kukubaliana kwamba, usalama na maedeleo ni mambo yanayowiana, lakini walitahadharisha kwamba Baraza hilo halikuwa na dhamana ya kulijadili na lilikuwa linafanya kazi ya vyombo vingine vya Umoja wa Mataifa kama vile Baraza Kuu la Umoja huo.


Balozi wa Misri katika Umoja wa mataifa, yeye hakusita kabisa kuelezea hisia zake pale aliposema huenda mchakato wa mageuzi yaliyokuwa yakiendelea nchi mwake ndiyo yaliyopelekea kuwapo kwa mjadala huo.


Akasema kuwa ingawa anakubaliana na ajenda hiyo, lakini alikuwa anatoa tahadhari kuwa isingekuwa busara wala haki kuyahusisha mageuzi ya kisiasa nchi mwake na mjadala huo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages