Breaking News

Your Ad Spot

Mar 31, 2011

BAADA YA KUZOA TIZO KIBAO TANZANIA KILI MUSIC AWARDS 20% ALONGA

*Asema hapendi sifa bila ushahidi
*Anajiita 20% kwa sababu ya akili na maisha anayoishi
 *Asema anaandika nyimbo zake katika fikra za Ki-hip hop



Abbas Hamisi  20% akipiga gita ndani ya
 studio ya Combinations Sound.
 MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya, Abbas Hamisi, maarufu kwa jina la 20%, mwishoni mwa wiki iliyopita aling’ara baada ya kushinda tuzo tano za muziki za Kilimanjaro katika sherehe zilizofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Abbas aliibuka mshindi katika tuzo ya msanii bora wa kiume, mwimbaji bora wa kiume, mwandishi bora wa nyimbo wa mwaka, wimbo bora wa mwaka na wimbo bora wa Afro-pop.

Hata hivyo, Abbas hakuwepo ukumbini kupokea tuzo zake. Zilipokelewa na mtayarishaji wake wa muziki, John Shariza ‘Man Water’ kutoka Kampuni ya Combination Sound.

Je, kwa nini Abbas hakuwepo kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee siku hiyo? Aliupokeaje ushindi huo? Ni kwa nini anajiita 20%? Nini kinafuata katika maisha yake na kazi zake? Makala hii ya ana kwa ana ya mtandao wa Bongo Celebrity inaelezea.

SWALI: Mambo vipi 20%?
JIBU: Ee bwana mimi Mungu ananisaidia, sijui wewe bradha.
SWALI: Yuko nasi pia. Kwanza hongera sana kwa ushindi wako wa mwishoni mwa wiki iliyopita. Tuzo tano kwa mkupuo sio mchezo. Hongera sana
JIBU: Ni kweli kabisa Bradha. Hata mimi namshukuru sana Mungu kwa kuniwezesha kuibuka mshindi namna ile.
SWALI: Labda swali la kwanza, ambalo watu wengi wangependa kujua ni ilikuwaje ukakosa kuhudhuria shughuli ya utoaji wa tuzo zile? Nini kilitokea?
JIBU: Kwa kweli hata mimi mwenyewe nilisikitika kutokuwepo pale. Ilitokea tu kwa bahati mbaya nilikuwa na onyesho lingine la kijamii mjini Tabora, ambalo nilishalitengea nafasi muda mrefu sana uliopita. Kwa hiyo ilinibidi kwenda kule kwa sababu kama unavyojua, katika onyesho huwezi kutuma mwakilishi kama ambavyo unaweza kufanya au nilivyofanya katika tuzo za Kili.
SWALI: Hilo linaeleweka na naamini mashabiki wako watakuelewa. Sasa zile taarifa kwamba umeshinda ulizipataje na ulizipokea namna gani?
JIBU: Taarifa za ushindi ule nilizipata kupitia luninga kwa sababu nilikuwa sehemu fulani nikifuatilia kila kitu kupitia ITV kabla ya kwenda kwenye onyesho letu. Pale nilipokuwa nilifuatilia mpaka niliposhinda tuzo ya nne ndio jamaa wakanifuata kwamba sasa twende kwenye onyesho. Taarifa za tuzo ya tano nilizipata nikiwa tayari nipo kwenye onyesho pale uwanjani Tabora. Kwa kweli nilifurahi sana kupata ushindi ule.
SWALI: Sasa kuna baadhi ya mashabiki wamekuwa wakijiuliza huyu 20% ni nani? Hawa ni wale, ambao walikuwa hawajawahi kufuatilia kwa karibu muziki wako au kazi zako za kiusanii. Labda kwa faida ya mashabiki hao, ambao hawakufahamu, wale ambao ndio ilikuwa mara ya kwanza kusikia jina lako, je jina lako kamili ni nani na kwa nini uliamua kujiita 20%?
JIBU: Jina langu kamili ni Abbas Hamis. Ni mzaliwa wa mkoa wa Pwani. Ni mtoto wa pili katika watoto wa kiume wa mzee wangu.
Hili jina la 20% nililipata kutokana tu na jinsi mimi mwenyewe nilivyokuwa najiona.Hata wewe mwenyewe kama utabahatika kusimama na mimi, utajua mimi kweli ni 20% kutokana na kimo na maumbile.
Halafu pili mimi najitambua kama 20% kimatendo kwa sababu tofauti na labda watu wengine mashuhuri au matajiri duniani, ambao wanaishi kwa kutegemea utajiri waliorithi au akili nyingi walizopewa na Mungu na mambo kama hayo, mimi natumia akili yangu ndogo kuishi na kufanya mambo yangu, kitu ambacho mimi nakiona ni 20%, yaani kulinganisha akili yangu na labda za wale manabii wa hapo zamani.
SWALI: Sasa nikisikiliza nyimbo zako tangu umeanza, nyimbo kama vile ‘Maisha ya Bongo’ ukielezea jinsi watu wanavyochomwa moto, vijana hawana mwelekeo; yaani suluba zinazowakuta vijana wa Uswazi, ulikuwa kwenye mahadhi ya hip hop zaidi kwa (mtazamo wangu). Ingawa bado unazungumzia mambo yale yale (heko kwa hilo), kwanini umebadilisha mtindo kidogo? Au ulikuwa unajitambulisha tu?
JIBU: Ni kweli kwamba kuna mabadiliko kidogo hususani katika midundo.Kwa jumla mimi natumia mitindo mbalimbali.Utaona kwa mfano wimbo kama ‘Maisha ya Bongo’ upo kwenye mtindo wa reggae zaidi wakati wimbo kama ‘Money Money’ upo katika mahadhi ya Pop zaidi.
Na mimi mwenyewe jambo moja, ambalo labda watu wengi hawajui ni kwamba, ni mtunzi mzuri wa nyimbo za mitindo tofauti tofauti kama vile reggae, hip hop, zouk nk.Kwa hiyo kinachotokea hivi sasa ni kwamba naziandika nyimbo zangu katika fikra za ki-hip hop na kisha kuziimba katika mahadhi tofauti tofauti.
SWALI: Hivi karibuni kumekuwa na hoja kwamba mwelekeo wa Bongo Fleva kwa ujumla umekuwa kama haueleweki. Lakini inaonekana wewe sasa hivi (hata kabla ya kuchukua tuzo) ndio ‘alama’ ya muziki wa Tanzania. Wengine wanaufananisha uwepo wako katika muziki wa kizazi kipya na kama vile alivyo Chameleon kule Uganda. Je, unachukuliaje maoni kama hayo? Je ni jukumu ambalo uko tayari kulibeba au inakuwaje?
JIBU: Nianze kwa kusema nashukuru kusikia sifa kama hizo kwa sababu najua Chameleon ni msanii anayeheshimika vyema kule kwao. Lakini kiukweli mimi katika maisha yangu nilivyo ni kwamba sipendi sifa ndogo na pia sipendi sifa bila ushahidi.Mimi ninachopenda kuona ni kwamba watu wote au wasanii wote waliopo katika hii tasnia ya Bongo Fleva wawe wanaumiza vichwa.
Binafsi nathamini sana suala la kuumiza kichwa katika tungo na kazi zangu. Kwa hiyo kama kuna, ambao wananiona mimi kama ‘mfano wao wa kuigwa’, basi la muhimu ni kufuata nyayo kwa kuumiza vichwa katika tungo zao na kazi zao kwa ujumla kabla hata hawajaingia studio. Binafsi namshukuru Mungu kwamba mpaka hivi sasa sijawahi kutengeneza wimbo ambao ukaishia studio tu.Namshukuru sana Mungu kwa hilo.
SWALI: Sasa hebu tuongelee kidogo kuhusu wimbo wako wa ‘Malumbano’, ambao ni miongoni mwa nyimbo zako zilizotokea kupendwa zaidi, ni wimbo wa mapenzi. Bahati mbaya au nzuri, Tanzania sasa hivi wasanii wengi wanapenda kuimba nyimbo za mapenzi. Unadhani ni kwa nini wimbo ule, ingawa uko katika maudhui, ambayo tunaweza kusema yameshazoeleka kupita kiasi, wenyewe umetokea kubamba zaidi?
JIBU: Kikubwa zaidi katika nyimbo ya ‘Malumbano’ ni kwamba nimeongelea mazingira ambayo tunaweza kuita ni mapenzi.Lakini ‘Ya nini malumbano’ ni neon, ambalo linajibeba lenyewe,halimaanishi mapenzi peke yake.
Maudhui ya wimbo huu yanaweza kutumika katika maeneo mengi, mfano hata barabarani, ukiwa barabarani na gari yako mbovu na ukaona inataka kuzimika, ni vyema ukaliweka pembeni.Kwa busara unalisogeza pembeni na kupisha wengine.Hakuna haja ya malumbano.
Mfano mwingine unaweza kuwa na taaluma yako nzuri, unaingia kazini na unakuta eneo limetawaliwa na chuki na maneno maneno. Katika mazingira kama hayo, mimi sioni kama kuna haja ya kuendelea kulumbana.Basi unaweza tu kujiweka pembeni kwani taaluma yako inabakia kichwani mwako.Mifano ipo mingi sana kuonyesha jinsi gani haina haja ya Malumbano ambayo ndio maudhui makubwa ya wimbo ule.
SWALI:Sasa hebu tuongelee kidogo masuala ya ubunifu kwamba unapokuwa studio yule mtayarishaji wako anakupa uhuru wa kufanya unachotaka au kuna mtu/watu wanaokupa muongozo zaidi. Unapoingia studio huwa inakuwaje?
JIBU: Mimi binafsi huwa napenda sana kufanya kazi na prodyuza, ambaye ananipa pia muda wa kuzungumza na kuchangia katika uboreshaji wa kazi nzima kwa sababu mimi ninapotunga wimbo huwa natunga pia kila kitu, mfano mapigo, kiitikio, mpangilio wa ala na viginevyo.
Kwa hiyo huwa napenda kupata prodyuza, ambaye pia ananisikiliza. Nashukuru Mungu kwamba watayarishaji wangu wa muziki ninaofanyanao kazi, tunashirikiana vizuri kabisa katika kuhakikisha kwamba kitu kinachotoka ni katika kiwango cha kueleweka na kukubalika.
SWALI:Taarifa nilizonazo zinasema kwamba watu waliposikia umeshinda tuzo kibao, kuna sehemu inasemekana watu walishangalia kama tunavyoshangilia mpira. Unajisikia vipi ukisikia vitu kama hivi?
JIBU: Kwa kweli inatia moyo na kuleta raha sana kuona jinsi gani watu wanakubali kazi zangu. Na nasikia kelele hizo hazikuwa pale ukumbini tu bali sehemu zingine nyingi nchini Tanzania.Hiyo ni kumaanisha kwamba watu wengi walipenda ushindi ule utokee na walijitolea na kujituma katika kunipigia kura. Haishangazi kuona kwamba jina langu lilipokuwa linatajwa tu katika kategori fulani fulani, tayari watu walikuwa wanalipuka kwa kushangilia.
Napenda kuwashukuru sana mashabiki wangu na watanzania wote kwa kuniwezesha kuibuka na ushindi huo.
SWALI: Sasa nini kinafuata baada ya hapa.Unaendelea na ziara zako,unajiandaa kufyatua albamu nyingine au mambo gani yanaendelea?
JIBU: Kusema kweli hapa nahitaji kuingia ofisini kumalizia filamu yangu moja ninayofanya na ndugu yangu Afande Sele. Inaitwa Haki Iko Wapi? Baada ya hapo nitaendelea na kazi zangu zingine na pengine kama kutakuwa na ‘Kili Music Awards Tour’-maana mpaka hivi sasa bado sijapokea au kusikia chochote kuhusiana na kitu kama hicho. Zaidi ni kuendelea na kazi tu kama kawaida.
SWALI: Labda kwa kumalizia tu,una ushauri gani kwa vijana wanamuziki wenzako au wengine wanaoota kufikia mafanikio kama haya yaliyojidhihirisha kupitia Tuzo za Muziki za Kili?
JIBU: Ninachopenda kuwaambia neno la kwanza ni waandike sana.Na neno la pili waandike sana na hata neno la tatu pia waandike sana.
SWALI: Asante sana kwa muda wako 20%. Kila la kheri katika kazi zako.
JIBU: Asante sana Bradha.

1 comment:

  1. Namkubali sana 20% kwani Kama alivyoelezea kwamba mashairi anatunga yy melody snatengeneza yaani am happy kwamba anajua anachofanya
    Tunzo zisimfanye amefika aendeleze Makali

    ReplyDelete

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages