Dk. Asha-Rose Migiro |
Na Mwandishi Maalm, New York
Maendeleo endelevu ya mamia ya mamilioni ya watu katika Asia, Amerika ya Kusini na Afrika, ambao wamejitahidi kujiondoa kutoka lindi la umaskini, hayawezi kuwa endelevu kama mazingira asilia ya Mama Dunia yataendelea kuharibiwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha-rose Migiro ameyasema hayo wakati Jumuia ya Kimataifa, ilipoadhimisha hapo siku ya jumatano, siku ya kimataifa ya Mama Dunia. Huku akisema kuwa dunia katika miongo miwili iliyopita imepitia mabadiliko makubwa yakiwamo ya kuinukia kiuchumi kwa baadhi ya mataifa.
“ Mamia ya mamilioni ya watu wetu katika Asia, Amerika ya kusini na hususani Afrika wamejitahidi kuondokana na umaskini.” Akabainisha Migiro na kuongeza “ tunahitaji kutawanya mafanikio hayo kwa mamia ya milioni zaidi ya watu kwa kuwapatia ajira zenye heshima, mazingira safi, nishati nafuu pamoja na faida zote za kijamii na kiuchumi zinazoweza kuharakisha maendeleo yao”.
Akasema wakati jumuia ya kimataifa ikiadhimisha siku hiyo ya Mama Dunia, kunahitajika kuwapo kwa mtizamo wa jumla wa suala zima la mazingira, kijamii na kiuchumi kwa sababu hayo ndiyo msingi mkuu katika kuleta maendeleo endelevu.
Hata hivyo anasema, amendeleo endelevu hayo hawezi kufikiwa bila kuheshimu makazi asili ya binadamu ambayo ni muhimu kwa mafanikio na ustawi wao.
Naibu Katibu Mkuu amewaeleza washiriki wa maadhimisho hayo ambayo yamefanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwamba, mwaka 2009 Baraza kuu la UM liliitangaza April 22 kuwa siku ya kimataifa ya Dunia Mama. Mkazo ukiwa katika kusisitiza uwiano kati ya mahitaji ya kiuchumi, ya kijamii na kimazingira kwa maslahi ya sasa na vizazi vijavyo, pamoja na kwa kukuza maelewano kati binadamu , mazingira ya asilia na ardhi.
Amesema kuwa athari za uharibifu wa mazingira asilia ya Mama dunia ziko wazi na zinatokana na matendo na kazi za mwanadamu mwenyewe.
Anazitaja athari hizo ambazo anasema zinaweza kabisa kubadilisha mwenendo wa dunia katika kuhimili maendeleo ya mwanadamu , kuwa ni pamoja na uchafuzi wa vyanzo vya mji,upotevu wa bioanuwai, ukataji wa misitu, uharibifu wa tabaka la Ozon na mabadiliko ya tabia nchi.
Migiro anasema ,nchi zinaweza kuharibu misitu yake, zinaweza kutokomeza samaki na viumbe hai wengine.Lakini katika kuangalia faida chanya ya pato lake la taifa hasara hiyo ya uharibifu wa mazingira na viumbe hai haiigizwi kwenye vitabu vya hesabu.
“ Tunajali zaidi faida itokanayo na mauzo ya silaha pamoja na kutumia mabilioni mengi ya dola kwa mwaka kwaajili ya kufidia makaa ya mawe, gesi na mafuta, huku mkazo mdogo ukielekezwa katika kuzikabiri athari wanazozipata watu maskini”. Anasema Naibu Katibu Mkuu
Na kuongeza. “Tunahitaji kurekebisha mahesabu yetu na kuongeza ufanisi katika matumizi ya raslimali pamoja na kuwa na mipango mizuri ya uchumi inayolenga na kuzingatia mahitaji ya watu maskini” anasisitiza Migiro.
Akahimiza na kuzitaka nchi kuzingatia matumizi ya nishati ambazo ninazalisha kiasi kidogo cha hewa ukaa, upatikanaji wa nishati nafuu ambayo zitahakikisha uwepo wa mahusiano mazuri na mazingira asilia.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269