Lionel Messi akishangilia |
LONDON, England
UBISHI wa nani zaidi umefikia tamati yake jana baada ya Barcelona kutwaa ubingwa wa ulaya kwa kuibugiza vibaya Manchester United mabao 3-1 katika pambano kali la fainali lililopigwa akwenye uwanja wa Wembley.
Matokeo hayo, yameendeleza ubabe wa Barca kwa Man United ambapo mwaka 2009, waliwafunga Mashetani Wekundu mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa, Rome nchini Italia.
Katika mchezo wa jana, Barcelona walianza kwa kasi huku wachezaji wake Lionel Messi, Javier Mascherano na David Villa wakifanya mashambulizi ya kushtukiza.
Dakika ya kumi, Villa nusura aipatie bao Barcelona, lakini shuti alilopiga liliokolewa na Rio Ferdinand kabla ya kutoka nje.
Nao Man United walijibu shambulizi kupitia kwa Javier Hernandez 'Chicharito', lakini shuti lake lilikuwa butu.
Pedro Rodriguez aliiandikia Barca bao la kuongoza dakika ya 27 baada ya kuwalamba Nemanja Vidic na Ferdinand na kisha kuachia mkwaju uliotinga kimiani.
Man walicharuka na kujipanga kutafuta bao la kusawazisha ambapo Wayne Rooney aliachia kombora kali lililojaa kimiani dakika ya 34 na kufanya hadi mapumziko kuwa nguvu sawa.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, lakini Barca ndio walionekana kutawala zaidi. Muda mwingi, walimiliki mpira asilimia 67 dhidi ya 33 za Man United.
Dakika ya 54, Messi anafanikiwa kufunga bao la pili kwa Barca akipiga shuti la mguu wa kushoto na kumuacha kipa wa Man United, Edwin van der Sar akiduwaa.
Licha ya Man U kuwaingiza Paul Scholes na Nani kuchukua nafasi za Fabio na Michael Carrick, bado walishindwa kuhimili mikikimikiki ya Barca.
Vijana wa Pep Guardiola walijihakikishia ubingwa wa ulaya dakika ya 70 baada ya David Villa kufunga bao la tatu.
Kuingia kwa bao hilo kulichanganya Man United ambao walianza kucheza rafu jambo lililomfanya mwamuzi Victor Kasai wa Hungary kuwaonyesha kadi za njano Antonio Valancia na Michael Carrick kwa mchezo mbaya.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269