Na Mwandishi Maalum
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim akizungumza wakati wa Mkutano huo. |
Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi zisizofungamana na upande wowote maarufu kama Non –Aligned Movement (NAM), wameitaka Israel kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa wa Kipalestina.
Mawaziri hao ambao walikutana kwa siku nne katika mkutano wao wa 16 uliofanyika Bali, nchini Indonesia, wamesisitiza katika tamko lao kwamba kitendo cha Israel kuwaachia wafungwa hao kitakuwa nikupiga hatua moja muhimu kuelekea mchakato wa amani ya kudumu.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Mahadhi Juma Maalim (MB). Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ombeni Sefue alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Tanzania katika mkutano huo.
Mawaziri hao katika tamko lao wameitaka Israeli kuachia huru idadi kubwa ya wafungwa wa kisiasa wa kipalestiana, kitendo ambacho kitatafisiriwa kama hatua sahihi inayolenga kujenga mazingira ya kuaminiana na kufungua milango ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili zinazohasimiana.
“Tunaitaka Israeli kuwaachia huru angalau wafungwa 300 ambao kati yao ni watoto walio chini ya miaka 18 wakiwamo pia wanawake. Tunasikitishwa sana na mwendelezo wa vitendo visivyo vya kibinadamu dhidi ya wapalestina” inasema sehemu ya tamko hiko.
Inakadiriwa kwamba kuna wafungwa wa kiasiasa wa Kipalestina wapatao 6,000 waliofungwa nchini Israel.
Kupitia tamko hilo, Mawaziri wa NAM wanasema licha ya kuitaka Israel kuwaachia huru wafungwa hao wa kisiasa, pia inaunga mkono uwepo wa mataifa mawili yanayoishi sambamba kwa kuzingatia mipaka ya mwaka 1967.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Naibu Waziri Mahadhi Juma Maalim, amesema, wakati Tanzania ikiridhishwa na kile ambacho NAM imefanikiwa kukitekeleza katika kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, lakini bado inasikitishwa sana na kutopatikana kwa ufumbuzi wa suala zima la matatizo ya Palestina.
“ Tatizo la Palestina limesuasua kwa muda murefu sana, na kusababisha madhara makubwa. Ujumbe wa Tanzania leo hii ni mfupi na ulio wazi, nao ni kwamba, madhara na maumivu wanayoyapata wananchi wa palestina ni lazima sasa yakomeshwe ” anasema Naibu Waziri
Na kuongeza. “ Maeneo yanayokaliwa kimabavu na waisraeli lazima yarudishwe kwa wananchi wa Palestina. Na ndoto iliyodumu kwa muda mrefu ya wananchi wa Palestina ya kuwa na taifa lao huru na mji mkuu wao ukiwa ni Mashariki ya Jerusalemu, wakiishi sambambana na kwa amani na usalama na taifa la Israeli ni lazima itimie sasa”.
Akabainisha kwamba, Jumuia ya Kimataifa inaowajibu wa kutowaangusha wananchi wa Palestina, halikadhalika NAM nayo haipashwi kuwaangusha raia wa Palestina.
Akizungumzia wajibu wa NAM na hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali, Naibu Waziri anasema wanachama wa NAM wanatakiwa kuwa kitu kimoja na kushikamana wakati huu kuliko wakati mwingine wowote.
Anasema Naibu Waziri , nchi wanachama wa NAM ambazo hivi sasa wamefikia 120 baada ya kujiunga kwa FIJI na AZEBAIJAN wanatakiwa kushikamana na kuwa kitu kimoja katika kuzikabili changamoto za sasa na zile mpya zitakazoimbuka.
“ Ni lazima na ni wajibu wetu kutumia nguvu na uwingi wetu, tupo wanachama 120 hivi sasa, idadi hii inatupa nguvu ya kusukuma mbele ajenda zinazolenga kuleta mabadiliko katika mfumo wa utendaji kazi wa Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa.” akasema
Na kuongeza kuwa idadi ya wanachama wa NAM inawawezesha kuitisha mabadiliko katika utekelezaji wa ahadi za mipango ya maendeleo, kusisitiza upokonyaji wa silaha, uwepo wa mifumo halali na sawa ya biashara na itakayojielekeza katika uainishaji wa matakwa sahihi ya nchi maskini zaidi duniani.
“haya ni mambo ambayo tunaweza kuyasimamia kama tukiamua.” Anasema Naibu Waziri.
Akimnukuu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuhusu nguvu na wajibu wa NAM katika masuala mbalimbali yakiwamo ya nguvu za kiuchumi.
Alisema hivi miaka ya 1970 na hapa ninamnukuu “ Tunaweza kusaidiana kuimarisha uhuru wetu na kukataa kutaliwa kiuchumi kwa kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana kwa faida yetu pamoja. Kwa sababu hatutaweza kamwe kuwa na uhuru wa kweli kama tu wadhaifu kiuchumi, huku matarajio yetu kiuchumi yakitulazimsiha kupiga makoti kama vile waokotezaji au ombaomba kutoka kwa mataifa makubwa”.
Mkutano huo wa 16 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa NAM licha ya kujadili suala la Palestina, pia walijadiliana kwa kina na kubadilishana mawazo kuhusu mwelekeo na mchango wa baadaye wa NAM katika kipindi cha miaka 50 ijayo na hasa kwa kuzingiatia mabadiliko makubwa na changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia hivi sasa.
NAM ambayo imetimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961 pamoja na kutoa mchango mkubwa sana katika kipindi cha uhai wake, yakiwamo mafanikio ya kumalizwa kwa ukoloni.
Lakini baada ya kumalizika kwa vita baridi ambayo hasa ndiyo iliyopeleka kuanzishwa kwa chombo hicho kisichofungamana na upande wowote. Sasa NAM inalazimika kujitazama upya na kutafakari nafasi yake, nguvu yake na ushawishi wake katika dunia inayobadilika kwa kasi huku ikikabiliwa na changamoto mbalimbali.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269