Breaking News

Your Ad Spot

May 19, 2011

MAHAKAMA KUU YAITUPA KESI YA KUMVUA UBUNGE DK. LIMBU BAADA YA MLALAMIKAJI KUSHINDWA KULIPA SH. MILIONI TISA ZA DHAMANA YA KESI


Dk. Festus Limbu
 Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, imeitupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Magu mkoani Mwanza, Julius Lwinzi Ngongoseke (UDP), dhidi ya mbunge wa sasa wa jimbo hilo , Dk. Festus Limbu (CCM).
Baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana Ngongoseke alifungua kesi hiyo No. 71 ya mwaka 2010, Novemba 16, 2010, akimshitaki Dk. Limbu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuhusiana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, yaliyompa ushindi mbunge huyo wa Magu.

Kwa mujibu wa mahakama, mlalamikaji (Ngongoseke), alipaswa alipe sh. milioni tisa (9,000,000), kama dhamana ya kesi hiyo, ili iweze kuingizwa kwenye utaratibu wa mashitaka kwa mujibu wa sheria za nchi.

Wakili wa mbunge Limbu, Methaw Nkanda aliwaambia waandishi wa habari jijini Mwanza kwamba, kesi hiyo iliyokuwa chini ya Jaji Nyangalika wa Mahakama Kuu, ilitupiliwa mbali na mahakama hiyo baada ya mlalamikaji kushindwa kulipa fedha hizo kwa muda aliotakiwa na mahakama.

Wakili huyo alisema Mahakama imetupilia mbali kesi ya mteja wangu Dk. Limbu, baada ya mlalamikaji kushindwa kulipa sh. milioni tisa kama dhamana ya kesi na kwamba kesi hiyo haipo tena wala haiwezi kufunguliwa upya.

Alifafanua kuwa Mahakama ilimpa muda Ngongoseke wa kulipa fedha hizo, lakini kila unapofika muda husika anaiomba mahakama imuongezee muda mwingine.
 
‘Kwa maana hiyo faili la kesi hiyo limetupiliwa mbali na mahakama mbele ya mlalamikaji Mei 17 mwaka huu 2011, siku ambayo alipaswa alipe fedha hizo milioni tisa ila akashindwa kulipa", alisema Wakili huyo wa Dk. Limbu, huku akimtaka mlalamikaji (Ngongoseke), asiupotoshe umma.

Alisema, mahakama hiyo ilifikia maamuzi hayo baada ya kuona kuna ucheleweshwaji wa wananchi kupata mwakilishi wao waliyomchagua, hivyo kwa vile Mahakama hiyo Kuu Kanda ya Mwanza imetupilia mbali kesi hiyo, Dk. Limbu ni mbunge halali wa jimbo la Magu mkoani Mwanza, na anapaswa atimize wajibu wake kama mbunge aliyechaguliwa na wananchi wake na kushinda Uchaguzi Mkuu uliopita.

"Tafsiri ya kutupwa kwa kesi hii, maana yake ni kwamba Dk. Limbu sasa ni mbunge halali wa jimbo la Magu. Kilichopo mbele yake ni kutekeleza majukumu yake kwa wananchi waliomchagua", alifafanua Wakili Nkanda, na kuongeza.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages