Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, wiki iliyopita ilifanya ziara ya siku sita katika mkoa wa Singida kuanzia Mei 10 hadi Mei 15 mwaka huu. Ziara hiyo ilihusisha Naibu Katibu Mkuu wa CCM, John Chiligati, Katibu wa NEC, Itikati na Uenezi, Nape Nnauye, Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Mwigulu Nchemba na Katibu wa NEC, Oganaizesheni Asha Juma Abdallah.
Kufuatia ziara hiyo, Katibu wa NEC Itikati na Uenezi Nape Nnauye leo amezungumza na waandishi wa habari, katika ukubi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba mjini Dar es Salaam. Nkoromo Daily Blog imepata taarifa kamili na ndiyo hii ifuatayo:-
1. UTANGULIZI:
Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya CCM ya Taifa ilifanya ziara katika Mkoa wa Singida kuanzia tarehe 10/05/2011 hadi 15/05/2011. Katika ziara hiyo wilaya zote na baadhi ya kata na matawi ya Mkoa huo yalitembelewa. Aidha Sekretarieti ilitembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali yetu ya CCM na pia ilifanya vikao vya ndani.
Pia Wajumbe hao walifanya mikutano mikubwa ya hadhara na baadhi ya kata iliwalazimu kusimama na kusalimia kutokana na hamasa kubwa waliyokuwa nayo wana CCM hasa baada ya matumaini mapya yaliyoletwa na uamuzi wa CCM kujivua gamba.
Katika wilaya ya Singida vijijini maeneo yafuatayo yalitembelewa; Ikugi, Lighwa, Mapuma, Ngori, Ngamu na Masawia. Kwa Wilaya ya Iramba kata za Makunda na Nkinto zilitembelewa. Wilaya ya Manyoni kata za Itigi, Manyoni Mjini na Chikuyu zilitembelewa na Singida Mjini Kata ya Mjini ilitembelewa.
Madhumuni ya ziara hiyo ilikuwa ni kukutana na kuwaelezea wanachama na wananchi zana nzima ya Mageuzi makubwa ndani ya chama na tafsiri sahihi ya falsafa ya kujivua gamba na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
2. HALI YA KISIASA:
Sekretarieti kwa ujumla iliridhika na hali ya kisiasa Mkoani Singida na katika ziara hiyo wanachama 580 walihama kutoka CHADEMA kuja CCM na wanachama wapya 188 walijiunga na CCM.
Changamoto kubwa iliyojitokeza kisiasa ni hali ya Madiwani kutojuwa vizuri wajibu wao wa kusimamia rasilimali za umma zikiwemo pesa zinazopelekwa kwenye halmashauri na serikali katika kusaidia Maendeleo, hivyo Sekretarieti ya halmashauri kuu inatoa wito kwa madiwani wa CCM nchi nzima kuhakikisha wanasimamia vizuri halmashauri na hasa watendaji wa Halmashauri hizi ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi na matumizi ya rasilimali za umma yanatumika vizuri na kwa lengo lillilokusudiwa.
3. UJENZI WA HOSPITALI MPYA YA RUFAA YA MKOA:
Sekretarieti ilitembelea mradi mkubwa wa ujenzi wa Hospitali Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Singida. Hospitali ya mkoa wa singida ilijengea mwaka 1954 wakati huo wakazi wa mkoa huo walikuwa ni 300,000 tu. Kutokana na sensa ya mwaka 2002 idadi ya wakazi ilikuwa 1,294,584 ambalo ni ongezeko la asilimia 400. Kutokana na hali hiyo Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kwa kushirikiana na wananachi waliamua kujenga Hospitali ya Rufaa Mandewa kwa ajili ya kulaza wagonjwa 1,000. Mradi huo unatarajiwa kuwa na majengo 37 kwa ajili ya vitengo mbalimbali ambayo itagharimu kiasi cha shilingi 80,000,000,000/=. Mradi ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2008/09 kwa kutafuta na kupata kiwanja chenye hekta 125, utafiti wa hali ya matetmeko ya ardhi, utafiti wa maji chini ya arhi, Upimaji wa sura ya eneo, Upimaji wa miliki, michoro ya awali, kupeleka huduma ya umeme na huduma ya maji.
Ujenzi huo utaendelea kukamilishwa kwa awamu mpaka hapo utakapo kamilika. Mara mradi ukikamilika utakuwa na uwezo wa kutoa huduma bora za kibingwa za Tiba na Kinga kwa Wananchi katika Mkoa wa Singida, utaboresha mazingira ya kazi kwa watoa huduma za Afya, utasaidia kutoa huduma zote za rufaa kwa Wananchi wa Mkoa wa Singida na Mikoa jirani hivyo kupunguza gharama za rufaa, itatoa huduma za utafiti na mafunzo na utatoa huduma za ushauri wa kitaalam na usimamizi wezeshi kwa Halmashauri Mkoani.
Katika bajeti ya mwaka 2008/09 serikali ilitenga shilingi 2,087,000,000.00 na kwa mwaka 2009/10 imetenga shilingi 2,027,436,000.00 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Kwa mwelekeo huu wa bajeti itachukua miaka 40 kukamilisha mradi huu. Kwa hiyo Sekretarieti inaiomba Serikali kutafuta fedha kutoka kwenye vyanzo vingine ili Hospitali hiyo ikamilike mapema ikiwezekana iwe ndani ya miaka 20 au chini ya hapo.
4. MRADI WA UBORESHAJI HUDUMA YA MAJI SAFI NA SALAMA SINGIDA MJINI:
Sekretarieti pia ilitembelea mradi wa uboreshaji huduma ya maji safi na salama Singida Mjini. Mamlaka ya Maji Singida (SUWASA) imebahatika kupata mkopo nafuu toka Benki ya Kiarabu (BADEA) na Shirika la Mafuta Ulimwenguni (OFID) kwa ajili ya kujenga mradi wa uboreshaji wa huduma ya majisafi Singida Mjini. Mradi huo utagharimu jumla ya dola za Kimarekani milioni 17.2(25,800,000,000.00) kwa mchanganuo ufuatao; BADEA dola milioni 5.5 ( Tsh. 8,250,000,000.00) OFID dola milioni 5.0 (Tshs. 7,500,000,000.00), Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) dola milioni 4.77(Tsh. 7,155,000,000.00) na Serikali ya Tanzania dola milioni 1.93(Tsh.2,895,000,000.00).
Mradi huu ni mkubwa sana na mara utakapokamilika tatizo la maji Singida Mjini litakuwa historia. Mradi utakuwa na visima 10, na mpaka sasa visima 4 vimekwisha jengwa na kila kisima kinauwezo wa kutoa lita 200,000 kwa saa.
Mradi huu utakapo kamilika utakuwa na uwezo wa kutoa lita 8,000 kwa siku, wakati mahitaji ya maji mji wa Singida ni lita 7,000 kwa siku. Hivyo basi mradi ukikamilika unategemewa kumaliza kabisa tatizo la maji mjini Singida.
5. MIRADI YA BARABARA:
Aidha Sekretarieti ilikagua ujenzi wa barabara ya Singida – Arusha, pamoja na barabara nyingine zinazoufanya mkoa wa Singida kufikika kwa urahisi. Barabara hizo ni ile ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Mwanza. Upembuzi wa barabara ya Itigi – Chunya, Itigi, Tabora, Kigoma na hiyo ya Singida – Arusha.
6. HITIMISHO:
Pamoja na shughuli nyingi za kisiasa zilizofanywa katika ziara hiyo ni vema Sekretariati ya Halmashauri Kuu ya Taifa itoe tamko la kuipongeza Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi kwa jinsi kinavyowajali wananchi wake kwa kutatua kwa haraka kero zinazowakabili. Miradi hii ni ishara tu ya shughuli nyingi ambazo Serikali yetu inazifanya kuwahakikishia wanachi wanapata maisha bora. Kwani miradi hii mikubwa ya Barabara imeifungua Singida na kuongeza fursa za uwekezaji Mkoani Singida na hivyo kuongeza ajira na kukuza Uchumi. Uwepo wa uhakika wa Maji na Hospitali siyo tu unawasaidia wakazi wa Mkoa wa Singida na Mikoa ya jirani bali pia inawavutia wawekezaji ambao kwao upatikanaji wa huduma za jamii ni moja kati ya vigezo muhimu kwa uwekezaji.
Tunawaomba wawekezaji wa ndani na nje watumie fursa hii kuwekeza katika Mkoa wa Singida kwani unasifa zote za kuwekezwa.
Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
17/05/2011
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
17/05/2011
Twashukuru mkuu kwa taarifa hii
ReplyDelete