Breaking News

Your Ad Spot

May 1, 2011

TANZANIA YAPIGIA DEBE MATUMIZI YA KISWAHILI UMOJA WA MATAIFA

Tanzania imeitaka  Idara ya Habari na Mawasilliano ya Umma  ya Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa  inaongeza  idadi ya waandishi katika Idhaa ya Radio ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa  ili iweze kutekeleza  kwa ukamilifu majukumu yake ya ukusanyaji,  utoaji na  usambazaji wa taarifa  zinazohusu  shughuli za   umoja huo.
Tanzania  imetoa wito huo wakati wa mkutano wa 33 wa  Kamati ya Habari ya Umoja wa Mataifa, ambapo pamoja na mambo mengine  Kamati hiyo iliyoanzishwa mwaka 1978 ikiwa na wajumbe 113 kutoka nchi wanachama  wa Umoja wa Mataifa, walipokea na kujadili taarifa ya katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa, kuhusu utendaji wa   Idara hiyo.
Akizungumza  kwa niaba ya  Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Afisa Ubalozi Mwandamizi, Bibi Maura  Mwingira amesema katika mkutano huo,   kwamba Tanzania  inafarijika na kuridhishwa   na namna ambavyo  lugha ya Kiswahili kupitia Radio ya Kiswahili ya UM imeendelea  kuwa kiungo mkuhimu cha mawasiliano, kupata umaarufu na  kuongeza idadi ya watumiaji wa taarifa za idhaa hiyo   licha ya kwamba ina wafanyakazi wachache.
Taarifa ya Katibu Mkuu wa UM iliyowasilishwa kwa wajumbe na Katibu Mkuu Msaidizi anayeongoza Idara ya Habari, Bw. Akito Akasaka, imeonyesha kuwa , katika eneo la  Radio ya Umoja wa Mataifa,  Radio hiyo ambayo hutoa taarifa zake  katika lugha sita  rasmi za UM, na lugha mbili za Kiswahili na Kireno, imekuwa  na mafanikio makubwa ambayo pia yamehusisha ongezeko la watumiaji wa taarifa zake.
Lugha rasmi za  Umoja wa Mataifa ni, Kiingereza, Kifaransa, Kiaarabu, Kirusi, Kichina na  Kihispania
Kwa upande wa Idhaa ya Kiswahili  Bw. Kiyo Akasaka amesema, Radio hiyo  ambayo ilianzishwa  mwaka 2006, watumiaji wa taarifa za idhaa hiyo imepanda kutoka asilimia moja wakati wa kuanzishwa kwake hadi kufikia asilimia 21, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa  kwa Radio  Maarifa FM iliyoko Tanzania.
  Haya si mafaniko madogo, ni mafanikio  makubwa ambayo  kila mmoja wetu anapashwa kujivunia na tunawapongeza wafanyakazi hao wawili kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya”. Akasisitiza Afisa Ubalozi.
Idhaa hiyo   ambayo inawafanyakazi wawili tu,  ikilinganishwa na idhaa nyingine ambazo zinawafanyakazi zaidi ya wanne.Inaongozwa na Mtanzania Bi Flora  Nducha. Ni kutokana na uchache huo wa wafanyakazi, ndio maana Tanzania imeitaka sekretarieti ya Idara hiyo ya Habari ya Umoja wa Mataifa kuangalia uwezekano wa kuongeza wafanyakazi .
Tanzania imewaeleza  wajumbe wa Mkutano huo  kuwa  Lugha ya Kiswahili ambayo inazungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 katika eneo la  Afrika ya Mashariki , Afrika ya Kati na  nje mipaka ya  ya maeneo hayo,  imekuwa chombo  na kiungo muhimu sana cha upashanaji wa habari hususani katika udhibiti wa migogoro na ujenzi wa amani.
 Ni kutokana na  umuhimu wa lugha hiyo,  Tanzania imesema, ndio  maana  Umoja wa Afrika uliamua kwa makusudi kabisa kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa  kati ya lugha rasmi za Umoja huo.
Tanzania ikasisitiza kwa kusema kuwa  kila mmoja anafahamu nvugu ya habari. Na kwa sababu hiyo,Kiswahili kina nafasi  ya kutoa mchango mkubwa  katika kufikisha ujumbe na kuwafikia watu wengi  kwa wakati mmoja.
“Kiswahili ni lugha muhimu sana kama chombo cha mawasiliano katika Umoja wa Mataifa, na  katika suala zima la  ulinzi, usalama  na ujenzi wa amani na maendeleo. Tunatambua changamoto ya ufinyu wa bajeti  inayoikabili   Idara ya Habari na Umoja wa Mataifa kwa ujumla wake.  Lakini bado tunaamini kwamba  mtafikiria suala la kuongeza idadi ya wafanyakazi katika idhaa hiyo hivi karibuni.” Akasisitiza  Afisa Ubalozi Mwandamizi
Na kuoongeza kuwa  Tanzania inaamini kuwa kwa  kuongeza idadi ya waandishi katika idhaa hiyo, siyo tu kutaboresha  kiwango na ubora wa habari zinazotolewa, kuwafikia watu wengi zaidi, lakini kitawapunguzia mzigo wa  kazi wafanyakazi  waliopo sasa.
IMETOLEWA NA UBALOZI WA TANZANIA KATIKA  UMOJA WA MATAIFA
NEW YORK

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages