Breaking News

Your Ad Spot

Jun 18, 2011

RAIS KIKWETE KUTUA MALAYSIA JUMAPILI ASUBUHI KUSHIRIKI MKUTANO WA SMART PARTNERSHIP DIALOGUE


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete (pichani) anatarajiwa kuwasili mjini Kuala Lumpur, Malaysia kesho, Jumapili, Juni 19, 2011, asubuhi,  kuungana na viongozi wenzake kutoka nchi mbali mbali katika mkutano wa mwaka huu wa Smart Patrnership Dialogue.
Mkutano huo ambao umekuwa unafanyika kila mwaka kwa miaka 16 sasa tokea mwaka 1995 unatokana na maamuzi ya wakuu wa nchi za Jumuia ya Madola uliofanyika Cyprus mwaka 1993 na kuzinduliwa rasmi katika mkutano wa wakuu hao uliofanyika Auckland, New Zealand mwaka 1995.
Mkutano huo huzungumzia masuala mbali mbali ya maendeleo na hasa umuhimu wa uhusiano mzuri kati ya Serikali, sekta ya umma na sekta binafsi katika kuleta maendeleo.
Mkutano wa mwaka huu umepangwa kufanyika katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Putrajaya (PICC) kilichoko katika mji mpya wa shughuli za Serikali ya Malaysia ulioko Patrajaya, nje kidogo ya mji wa asili wa Kuala Lumpur.
Nchi ya Malaysia imewaalika wakuu 25 wa nchi mbali mbali duniani kushiriki katika mkutano huo hata kama haitarajiwi kuwa wote watashirki mkutano huo. Kutoka Afrika wamealikwa Rais Kikwete, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Rais Omar El Bashir wa Sudan na Waziri Mkuu wa Lesotho.
Rais Kikwete atawasili Malaysia kuhudhuria mkutano huo wa siku tatu akitokea Shelisheli ambako usiku wa leo, Jumamosi, Juni 18, 2011, atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za Siku ya Taifa ya Shelisheli.
Mbali na kuhudhuria mkutano huo ambako atazungumza kwenye kikao cha ufunguzi na pia kwenye kikao kitakachozungumzia namna mbadala na za ubunifu zaidi za kupata fedha kwa ajili ya maendeleo, Rais Kikwete pia atakuwa na shughuli nyingine muhimu za kikazi.
Miongoni mwa shughuli hizo ni Rais Kikwete kukutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Malaysia, Dato’ Sri Mohammed Tun Abdul Razak, kukutana kwa mazungumzo na aliyekuwa waziri mkuu wa Malaysia, Mheshimiwa Tun Dkt. Mahathir Mohamad, Rais wa Heshima wa Taasisi ya Uongozi ya Perdana Leadership Foundation.
Rais Kikwete pia atakutana na kula chakula cha usiku na wenyeviti, marais na watendaji wakuu wa makampuni makubwa ya Malaysia wakiongozwa na Mheshimiwa Mahathir Mohamed.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages