Breaking News

Your Ad Spot

Jun 7, 2011

VIJANA NGUZO MUHIMU KATIKA KUUKABILI UKIMWI-MIGIRO

Naibu Katibu  Mkuu wa UN,  Dk. Asha-Rose Migiro,
Bi Christine Roqriquez  na Bw, Michel Sidibe wakiwa
wameshika Ripoti baada ya uzinduzi.
Na Mwandish Maalum, New York
Wakati viongozi wakuu wa  nchi na serikali wakitarajiwa kukutana kwa siku tatu  hapa Umoja wa Mataifa kujadiliana, kubadilishana mawazo, uzoefu na kuweka mikakati na maazimio mapya ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha- Rose Migiro anasema  vijana  ni nguzo muhimu katika  mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Asha- Rose Migiro ameyasema hayo mwishoni mwa wiki  mbele ya waandishi wa habari,wakati wa uzinduzi wa ripoti  ya maendeleo ya  mataifa kuhusu vita dhidi ya ugonjwa wa ukimwi. Ripoti hiyo ambayo inasema  miaka 30 ya ukimwi,  mataifa bado  njia panda, imeandaliwa na  Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya ukimwi (UNAIDS) .
Ujumbe wa Tanzania  katika Mkutano huo viongozi utakaoanza siku ya  jumatano, utaongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dkt. Mohammed Gharib Bilali.
Migiro anasema  anaamini  vijana wakisaidiwa na kujipanga vizuri  ni nguzo muhimu sana kwa sababu amejionea  kwa macho yake kile kinachofanywa na  vijana wa  Tanzania kupitia mtandao wao wa  Tanzania  Youth Alliance .
Anasema  vijana wale wanaukabili vilivyo ugonjwa huo kwa kusaidiana wenyewe kwa wenyewe, katika namna ambayo hata watu wazima hawezi kufanya hivyo.
   Nimeyaona haya nchini kwangu mwenyewe nilipokuwa huko miezi michache iliyopita,  nilivutiwa sana na vijana wale namna  wanavyosaidiana  kwa  kuhamasishana, wanaelimishana kwa uwazi na ukweli njia sahihi na salama, na kwakweli wanasaidia sana katika kupunguza kasi ya ugonjwa huu”.anasisitiza Naibu katibu Mkuu.
Akabainisha kuwa  juhudi za vijana wale wa Tanzania kupitia mtandao wao,  zinaweza kuonekana kama tone la maji katika ndoo. “ Lakini kukiwa na matone mengi, matone hayo yanaweza kuzalisha mawimbi , mawimbi ya  mageuzi na hili ndilo linalosisitizwa katika ripoti hii”
Akizungumzia zaidi  kuhusu ugonjwa wa ukimwi, Naibu katibu mkuu anasema, miaka 30 iliyopitia wanasayansi waligundua  ukimwi, ulikuwa ugonjwa wa ajabu, unaoua na kusambaa.
“ Miongo  mitatu baadaye , sasa  watu wengi zaidi wanafursa ya kupata dawa, maambukizi yanapungua, na idadi kubwa ya wanawake wajawazito wanaoishi na virusi vya ukimwi wana nafasi kubwa ya kuwakinga watoto wao dhidi ya  ugonjwa huo” akasema migiro.
Na kuongeza kuwa  mafanikio hayo na mengine mengi dhidi ya ugonjwa wa ukimwi ni matokeo ya ushirikiano wa wadau mbalimbali, zikiwamo serikali, wataalam wa afya, taasisi binafsi,na mashirika ya kimataifa.
“Lakini pamoja na yote hayo, ni  mchango  mkubwa uliotolewa watu wenyewe wanaoishi na virusi , au wanaishi katika mazingira hatarishi. Hawa walisimama kidete na kujitokeza hadharani na kuzungumza na wakasikika, harakati zao ndizo zimetufikisha hapa tulipo leo hii ingawa bado tunasafari ndefu.” akasisitiza Naibu Katibu Mkuu.
Akizungumzia mkutano wa viongozi wakuu wa nchi na serikali, Naibu katibu mkuu anasema  viongozi hao kupitia mkutano huo wanatarajiwa kutoa tamko jipya la namna gani wamepanga kuchukua hatua kama nchi mojamoja na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuukabili ukimwi miaka 10 ijayo.
“tunatarajia watueleze  juhudi watakazochukua kama nchi moja moja, lakini pia kwa kushirikiana na  Umoja wa Mataifa, mashirika ya  kimataifa, asasi zisizo za kiserikali ili  dunia ifike mahali pakuwana   na kiwango sifuri cha maambukizi, kiwango sifuri cha unyanyapaa na kiwango sifuri cha vifo vitokanavyo na  ukimwi”. Anasema Migoro.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages