Breaking News

Your Ad Spot

Jun 23, 2011

VYOMBO VYA HABARI NI WADAU WAKUBWA WA MAFANIKO YA UONGOZI WA CCM: NAPE


Nape akiwa katika studio za TBC Taifa, leo. Kushoto ni watangazaji
Joyce Kingalame na Shaaban Kisu wakimhoji.
                                                                                                                                                     KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinzduzi (CCM) Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amesema vyombo vya habari nchini ni mdau mkubwa aliyechangia mafanikio yaliyofikiwa na CCM hadi sasa.       Amesema bila vyombo vya habari, ingekuwa vigumu CCM kufukisha malengo na utekelezaji wa ilani zake kwa wananchi kwa miaka yote, hasa wale walioko  vijijini.
      Nape alisema hayo LEO alipozungumza kwa nyakati tofauti na wakuu wa vyombo vya habari vya TBC1, TBC Taifa na magazeti ya IPP, akiwa katika ziara ya kujitambulisha kwenye vyombo vya habari ambayo aliianza jana.
      Alisema, mbali na kufikisha malengo na utekelezaji wa ilani kwa wananchi, vyombo hivyo pia vimekuwa dira nzuri kwa Chama katika utendaji wa kazi zake za kujenga taifa.
      Alivitaka vyombo vya habari nchini, kuendelea kufichua watendaji wabovu serikalini na Katika Chama Cha Mapinduzi, lakini kwa nia ya kujenga nchi na si kwa lengo la kubomoa kama ambavyo baadhi ya vyombo vimekuwa vikijaribu kufanya.
      "Ninyi mmekuwa muhimili muhimu sana kwa mafanikio ya CCM, hivyo tutaendelea kuwafanya sehemu ya kutega masikio yetu kama Chama tawala ili kuweza kuyasikia na kufahamu yale ambayo katika njia ya kawaida hatuwezi kuyapata ili kutatua kero za wananchi", alisema.
       "Ninyi ndiyo sauti za wananchi, wapo watu hasa vijijini ambao wanakuwa na mengi moyoni wanayotaka yajulikane ili yapatiwe ufumbuzi, wasiposemea kwenu watakaa nayo mwiso yawazidi na kuamua kuyatoa kwa njia zisizostahili zenye kusababisha uvunjivu wa amani", alisema.
        Alirejea kauli yake ya kuvitaka vyombo vya habari kuweka uzalendo mbele kwa kuzipa umuhimu habari ambazo zinalijenga taifa, badala ya kujaribu kuandika habari za uchochezi kwa lengo la kibiashara.
Kuhusu dhana ya CCM kujivua gamba, Nape alisema, wanasema lengo ni kuwalenga watu fulani ili kuwahujumu kisiasa, alisema si kweli bali lengo la msingi la mabadiliko hayo ni kujenga taswira bora ya CCM kama Taasisi ya umma.
       "Wenye madai hayo kwamba kuna wanaolengwa ili kuhujumiwa kisiasa ni wale wanaokwepa kuwajibika kuhusiana na maamuzi yaliyopitishwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kilichofanyika Dodoma, Aprili mwaka huu", alisema Nape akijibu swali la mwandishi wa habari wa Nipashe, Joseph Mwendapole aliyetaka kujua kama kuna walengwa maalum katika dhana hiyo ya kujivua gamba.
       Mapema akiwa akizungumza na Mkurugenzi wa TBC, Clement Mshana, alitoa changamoto kwa vyombo vya habari kama TBC Taifa na TBC1, kutunza hotuba, filamu na matukio mbalimbali ya kitaifa ili visipotee.
        Kwa upande wake, msanifu mkuu wa kurasa a Guardian, Wence Mushi aliomba CCM kufungua milango ya mawasiliano ili kuepusha upotoshaji wa taarifa mbalimbali.
         Nape aliahidi kutoa ushirikiano saa 24 kwa vyombo vya habari kwa lengo la kuvipatia habari vyombo hivyo pale itakapokuwa inahitajika kufanya hivyo, kwa lengo la kulijenga taifa.

1 comment:

  1. Kweli mkuu, vyombo vya habari vinaweza kumwangusha mtu au kumsimamisha akakubalika kwa jamii!

    ReplyDelete

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages