Breaking News

Your Ad Spot

Jul 29, 2011

CCM DAR YALAANI WABUNGE KUDHARAU BUNGE

NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam, kimelaani vitendo vya baadhi ya wabunge wa CHADEMA kuendeleza tabia ya kulikosea heshima bunge.
      Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa CCM wa mkoa huo, Kilumbe Ng'enda alisema, pamoja na vitendo vya wabunge hao kuaibisha taifa, lakini wanawaaibisha zaidi vyama vyao na wananchi waliowachagua.
       Kauli hiyo ya kulaani imetolewa na CCM mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni siku mbili baada ya baadhi ya wabunge wa CHADEMA wakiwemo Mbunge wa Nyamagana Ezekiel Wenje, Tundu Lissu (Singida Mashariki),Godbless Lema (Arusha Mjini) na Mchungaji Peter Msigwa kufukuzwa katika ukumbi wa Bunge na Naibu Spika Job Ndugai kwa kulikosea heshima bunge,juzi.
       "Hali ya vurugu, utovu wa nidhamu, jazba na ubabe vinavyojitokeza kwa baadhi ya wabunge katika kikao kinachoendelea mjini Dodoma, haionyeshi kuwa dhana ya kuwapata wabunge wenye sifa imezingatiwa. Hawa wanaofanya vitendo hivi bungeni wanatutia aibu wanasiasa wote ukiacha tofauti zetu za kiitikadi", alisema N'genda.
        Alisema, baada ya ushindani katika uchaguzi mkuu wa 2010,kuzaa wabunge 166 wa majimbo kutoka CCM, CUF (24), CHADEMA (23) NCCR-MAGEUZI (wanne) na TLP na UDP mbunge mmoja kila chama, ilitarajiwa kila chama kimetoa mchango wa wabunge wenye sifa za uongozi na Utumishi wa umma wenye hekima,busara na malezi ya Kitanzania yanayojali utu na heshima kwa wengine,kuheshimu mawazo ya wengine na utii katika sheria na taratibu, lakini kinachoonekana sasa kwa upande wa CHADEMA.
        "Ni imani yangu kuwa katika dunia watu wanatambulika katika makundi yao ya kazi, ukiacha namna nyingine ya kumtambua mtu mmoja mmoja, hivyo sisi kama wana siasa, wanasiasa wenzetu hawa wanatutia aibu! Lakini zaidi wanakitia aibu chama chao, na wananchi wa majimbo yao", alisema Ng'enda.
         Ng'enda alisema, hatua hiyo ya wabunge kukosa nidhamu ya kutofuata taratibu walizojiwekea ni kielelezo cha wazi kuwa vyama vyao havikuwachuja vizuri na wananchi hawakupata walichokusudia.
        Alisema, hapa shaka kuwa CCM na serikali yake inayo madhaifu yake kwa kuwa haiwezi kuyakosa ikiwa inaongozwa na binadamu ambao si malaika, lakini kutokana na yanayojitokeza bungeni ni dhahiri wengi wa viongozi wa CHADEMA na wabunge wao wana mapungufu yaliyopita kiwango cha ubinadamu wa kawaida.
        "Kwa kutazama Mawaziri wa serikali na wale Mawaziri Kivuli wa kambi ya upinzani, utakapota kuunda serikali yako unayotaka uwe makini, ukiletewa Waziri wa Mambo ya Ndani Shamsi Vuai Nahodha na Waziri Kivuli wa wizara hiyo kambi ya upinzani Godbless Lema,unaweza kumfanya Lema awe waziri na mambo yakawa shwari kwa anavyoonekana kuweka mbele jazba, kiherehere na ubabe?" alihoji Ng'enda.
       Ng'enda alisema wanachofanya baadhi ya wabunge wa CHADEMA kuendekeza jazba, kiherehere na ubabe ni kusaka sifa na umaarufu ili waonekane bora, bila kukumbuka kwamba tabia hiyo ya kusatafuta heshima kwa nguvu itawapatia dharau kwa urahisi zaidi.
      Aliwapongeza wabunge wa CCM na viongozi wote wa Bunge, Spika, Naibu Spika na Wenyeviti kwamba wanajitahidi kutekeleza amajukumu yao bila woga na kumtaka Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akidhi hadhi yake ya kuwa kiongozi wa wapinzani kulaazni vitendo vya wabunge kukosa nidhamu.
      "Namkubusha mhe. Mbowe awe kweli kiongozi wa wapinzani na kuongoza maana yake kuonyesha njia, lazima alaani vitendo vya wabunge kukosa nidhamu", alisema Ng'enda.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages