Na Mwandishi Maalum
New York
Mkutano Mkuu wa 65 wa Umoja wa Mataifa, jana julai 14 umeipitisha kwa kauli moja Jamhuri ya Sudani ya Kusini kuwa mwanachama mpya wa 193 wa Umoja wa Mataifa.
Tukio hilo la kihistoria lililokuwa na msisimko wa aina yake, lilitanguliwa kwanza kwa kusomwa kwa tamko maalum lililoandaliwa na Kundi la nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa, tamko liloinadi Sudani ya Kusini ili iweze kuingizwa kuwa mwanachama wa UM.
Bw. Jeffrey Thamsanqa Rabede, Waziri wa Sheria na Katiba kutoka Afrika ya Kusini, ndiye aliyesoma Tamko hilo ambalo baadaye lilipitishwa kwa kauli mmoja na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Akizungumza mara baada ya Jamhuri ya Sudani ya Kusini kukubaliwa rasmi kuwa mwanachama wa 193 wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon alisema.
“ Katika muda huu na mahali hapa, dunia imekusanyika na kutamka kwa kauli moja, karibu Sudani ya Kusini. Karibu katika Jumuia ya Umoja wa Mataifa” .
Akaendelea kusema “ kwa pamoja hebu na tuwaambie wananchi wa taifa hili jipya. Sasa mnakaa miongoni mwetu na tunasimama pamoja nanyi”
Naye Rais wa Mkutano wa Mkuu wa 65 Bw. Joseph Deiss amesema, siku ya julai 14 ilikuwa ni siku muhimu sana kwa Afrika na kwa Jumuia ya Kimataifa
Akaelezea matumaini yake kwamba Sudani ya Kusini itaendeleza juhudi za kuhimiza amani, ulinzi, maendeleo , urafiki na ushiriiano baina ya mataifa mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya serikali mpya ya Jamhuri ya Sudani ya Kusini ambayo ilijipatia uhuru wake rasmi julai tisa, makamu wa Rais wa nchi hiyo Bw. Riek Machar,ambaye ndiye aliyeongoza ujumbe wa chini yake, katika tukio hilo alikuwa na haya ya kusema.
“Ninajisikia mwenye heshima na fahari kubwa kusimama mbele yenu na kuwasilisha salamu za serikali yangu na watu wake. Kwa kukubali kwenu kulikaribisha taifa hili jipya kuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Akiongea kwa hisia , Makamu hiyo wa Rais alisema, harakati za nchi yake za kudai uhuru wake zimegharimu maisha ya mamilioni ya watu ya, na kwamba kujitoa kwao mhanga hakutasahaulika kamwe.
“ Tulipoanza safari yetu hatukujua, licha ya matumaini makubwa tuliyokuwa nayo wakatu ule, kama tungefikia hatua hii ya leo. Tunachotakiwa sasa ni kusonga mbele ili tuweze kutimiza mataratijo ya watu wetu”
Makamu huyo wa Rais alitoa wito kwa nchi za Eritrea, Ethiopia na Somalia kutumia njia za majadiliano ili kumaliza migogoro inayoendelea katika nchi hizo. Aidha aliitaka jumuia ya kimataifa kukishughulikia kikundi cha Lord’s Resistance Army , kikundi ambacho kimekuwa kikiendesha mapigano na vitendo vya kikatili nchi Uganda na katika baadhi ya nchi nyingine.
Aidha wawakilishi wa makundi ya nchi za Afrika, Asia, Ulaya Mashariki, Amerika ya Latini, Ulaya ya Magharibi na nchi nyingine, pamoja na nchi mwenyeji Marekani nao walitoa hotuba za kulikaribisha taifa hilo jipya.
Baada ya Mkutano Mkuu kukamilisha shughuli hiyo kulifuatiwa shughuli ya kupandisha bendara ya Taifa ya Jamhuri ya Sudani ya Kusini.
Nchi ya mwisho kujiunga na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa ilikuwa ni Montenegro iliyojiunga June 28 mwaka 2006 na kuwa nchi ya 192 baada ya kupata uhuru wake kutoka Serbia
Ujumbe wa taifa jipya la Jamhuri ya Sudani ya Kusini, ukiwa umekaa rasmi katika sehemu yake ndani ya ukumbi Mkuu wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, baada ya kupitishwa kwa kauli moja kuwa mwanachama wa 193 wa Umoja wa Mataifa.
Walinzi wa Usalama wa Umoja wa Mataifa wakijiandaa kuipandisha rasmi bendara ya Jamhuri ya Sudani ya Kusini.
Viongozi wakuu wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Bendara ya Jamhuri ya Sudani ya Kusini kupandishwa rasmi katika Umoja wa Mataifa. Kutoka Kushoto ni Rais wa Mkutano Mkuu wa 65 Bw. Joseph Deiss, Makamu wa Rais wa Sudani ya Kusini, Bw. Riek Machar, Ban Ki Moon, Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa na Dkt. Asha-Rose Migiro, Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa.
Mjumbe huyu wa Serikali ya Sudani ya Kusini, alishindwa kabisa kujizuia, akaamua kuserebuka kivyake vyake, akifurahia kupandishwa rasmi kwa bendera ya nchi yake, na kuwa bendara ya 193.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269