Breaking News

Your Ad Spot

Jul 4, 2011

WAZIRI MKUU KWENDA KOREA KUSINI KESHO

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda anatarajiwa kuondoka nchini kesho (Jumanne, Julai 05, 2011) kwenda Korea Kusini ambako atazindua meli ya uchimbaji mafuta iitwayo Poisedon ambayo inajengwa katika bandari ya Geoje.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, uzinduzi huo utafanyika Ijumaa, Julai 8, 2011 katika mji wa Busan ambao uko kusini mwa nchi hiyo.

Meli hiyo inajengwa na kampuni ya Petrobas kutoka Brazil na inatarajiwa kuja kufanya kazi ya kutafiti na kuchimba gesi na mafuta katika pwani ya Tanzania kuanzia Agosti, mwaka huu. Meli hiyo baada ya kuzinduliwa, itapelekwa nchini Singapore kuwekewa vifaa maalum kabla ya kuwasili nchini Tanzania kuanza kazi.

Akiwa katika Jamhuri ya Korea, Alhamisi, (Julai 7, 2011) Waziri Mkuu Pinda atatembelea eneo la viwanda vya kujenga meli (ship building area) ili kuona hatua mbalimbali za ujenzi wa meli. Mchana siku hiyohiyo, atatembelea kiwanda cha kusindika bidhaa za baharini (marine products processing factory) kilichopo katika mji wa Geoje. Ijumaa asubuhi atazindua meli ya Poseidon na kuhutubia washiriki wa hafla hiyo. Alasiri siku hiyo atatembelea eneo la Georim lenye viwanda vya kusindika mazao ya kilimo katika mji huo huo wa Geoje.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu anatajiwa kufuatana na mkewe Mama Tunu Pinda, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, na viongozi waandamizi wa Serikali. Akiwa huko ataungana na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Bibi Salome Sijaona.

Waziri Mkuu anatarajiwa kuondoka Korea Kusini Jumamosi jioni na kuwasili nchini Jumapili, Julai, 10, 2011 na kisha kurejea Dodoma kuendelea na ratiba za Bunge.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
DAR ES SALAAM
04.07.2011

Irene K. Bwire,
Cell:+255-784-365-214,
Email:
irenekaki@yahoo.com
"If you can't feed a hundred people then feed just one" - Mother Theresa

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages