Jeshi la Polisi mkoani Kigoma linawashikilia watu 52 kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za ujambazi wa kutumia silaha na wizi wa vocha za simu za mkononi zenye thamani ya karibu shilingi milioni 63.2.
Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma ACP Fraisser Kashai, amesema kuwa watuhumiwa 21 wamekamatwa katika wilaya ya Kigoma mjini, watuhumiwa 18 wamekamatwa katika wilaya ya Kasulu na wengine 13 katika wilaya ya Kibondo.
Amesema watuhumiwa wote hao wamekamatwa katika Operesheni maalum inayoendelea katika wilaya zote za mkoa huo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupambana na vitendo vya kihalifu vikiwemo vya ujambazi wa kutumia silaha, utekaji wa magari na uporaji wa mizigo na fedha za abiria.
Kuhusiana na wizi wa vocha za simu, Kamanda Kashai amemtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Itochiman Sebeha (27), mkazi wa Katubuka mjini Kigoma ambaye alikuwa ni msimamizi na mfanyakazi wa Kampuni ya Shivacom iliyopo chini ya Kampuni ya Simu za mkononi ya VODACOM mkoani humo.
Amesema kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na taarifa zilizokuwa zikikusanywa na Makachero wa Polisi mkoani humo waliokuwa wakifuatilia nyendo za mfanyakazi huyo ambapo mara baada ya kumtia nguvuni, Polisi waliwasiliana na uongozi wa Kampuni ya Shivacom Jijini Da es Salaam ambapo walitumwa wakaguzi wa mahesabu mkoani humo na kubaini kuwa fedha za vocha za milioni 63,199,000 za kampuni hiyo zilikuwa hazijapelekwa benki na hazijulikani zilipo.
Hata hivyo Kamanda Kashai amesema kuwa wakati wa ufuatiliaji wa nyendo za mtuhumiwa huyo, Makachero wa Polisi mkoani Kigoma wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa wilaya ya Kigoma mjini ASP Mohammed Kilonzo, walifanikiwa kupata maboksi mawili yaliyojaa vocha za Vodacom yakiwa yamefichwa porini jambo ambalo limewaongezea mashaka katika ufuatiliaji wa nyendo za mtuhumiwa huyo.
Baada ya kuyafanyia ukaguzi maboksi hayo, Makachero hao walibaini kuwa yalikuwa na vocha mchanganyiko za Kampuni ya Simu za Mkononi ya VODACOM zikiwemo za shilingi 5,000 kwa kila moja, shilingi 2,000 shilingi 1000 na shilingi 500.
Baada ya kuwasili kwa maafisa wa Kampuni ya Shivacom mkoani Kigoma wakitoka Makao Makuu ya Kampuni hiyo Jijini Dar es Salaam, walibaini kuwa maboksi hayo pamoja na vocha hizo, zilikua ni sehemu ya zile alizopewa mtuhumiwa huyo kwa ajili ya kuwasambazia wauzaji wa vocha za jumla mkoani Kigoma.
Kamanda huyo amesema bado Polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba pamoja na mambo mengine, pia wanashirikiana na wenzao wa Uhamiaji ili kubaini uhalali wa uraia wa mtuhumiwa huyo.
Kamanda Kashai amesema kuwa watuhumiwa wengine 18 walikamatwa Wilayani Kasulu kwa tuhuma mbalimbali na wengine wawili, mmoja alikamatwa na kiasi kikubwa cha pombe haramu ya gongo na Bangi na mwingine anashikiliwa kwa tuhuma za kuingia nchini isivyo halali.
Katika Wilaya ya Kibondo Polisi wamekamata watuhumiwa 13 kwa makosa mbalimbali ambapo watatu kati yao wanatuhumiwa kwa kuingia nchini isivyo halali na wengine kumi wanashikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya unyang’anyi wa kutumia silaha na utekaji wa magari ya abiria.
Bangi iliyokamatwa |
Hata hivyo Kamanda Kashai amewaomba wananchi kuendelea na juhudi za kutoa taarifa Polisi kila wanapobaini kuwepo kwa vitendo vya kihalifu ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu hutuma zinazowakabili.
Mhina Zanzibar 0784 886488/ 0715 886488/ 0767 886488
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269