Breaking News

Your Ad Spot

Sep 21, 2011

IGUNGA: CHADEMA WADAIWA KUCHOMA MOTO NYUMBA YA KATIBU WA CCM

Makala (kulia) akimuonyeha Mukana nyumba yake iliyote
ketea kwa kuchomwa moto na wanaosadikiwa kuwa wafuasi
wa CHADEMA
NA BATESI  KASHINDI, IGUNGA
Watu wasiojulikana wanaoaminika ni wafuasi wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) wameichoma moto nyumba ya katibu wa CCM kata ya Nyandekwa wilaya ya Igunga, Hamis Makala.

Tukio hilo lilitokea saa 8:00 usiku wa kuamkia jana ambapo katibu huyo na familia yake walinusurika kwa kuwa walikuwa wakiishi katika nyumba kubwa iliyopo jirani na nyumba hiyo iliyokuwa ikitumiwa kama jiko.

Katibu mkuu wa CCM, Wilson Mukama na viongozi wengine wa CCM leo walitembelea eneo la tukio kwa lengo la kumfariji mwana-CCM huyo ambapo Mukama alimpatia msaada wa fedha taslimu sh100,000.

Makala alimweleza Katibu mkuu huyo kuwa kuna kila dalili kuwa tukio hilo lilipangwa na kutekelezwa na wafuasi wa Chadema kutokana na kukasirishwa na kampeni zake zinazokifanya chama hicho kikose watu.

Akisimulia mkasa huo, Makala alisema alipotoka nje alikuta nyumba hiyo ikiteketea na ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada na majirani wengi walijitokeza lakini hawakufanikiwa kuudhibiti moto huo.

“baada ya moto kuzimika na kwa kuwa ilikuwa bado ni usiku sana na niliamua kulala hadi kesho yake watu wengi zaidi walikuja kunipa pole ndipo tukaona karatasi imechomekwa kwenye nyumba”alisema.

Alifafanua kuwa karatasi hiyo ambayo tayari imechukuliwa na polisi kwa ajili ya upelelezi ili kuwa na ujumbe unaosomeka “Chadema sisi ni wajanja”, hali inayofanya tukio hilo lihusishwe na chama hicho.

Alisema kuwa mbali na ujumbe huo, lakini katika ofisi za kata za CCM katika kata hiyo ulipatikana ujumbe mwingine unaosomeka” hatuyataki mabango ya CCM nyinyi ni majizi tu pamoja na Diwani wenu mtakunya tunasema wajanja wako Chadema na namba zetu hizi hapa”.

Makala alisema katika tukio hilo la nyumba yake kuchomwa moto, kuku 15 kati ya 21 ambao jioni huwalaza katika nyumba hiyo walikufa kwa moto huo ambao anadai ulikuwa mkubwa kiasi cha kushindwa kuudhibiti.

Akizungumzia tukio hilo, Mukama alilaani vikali tukio hilo akisema” tukio hili ni lazima lilaaniwe kwa sababu kwanza halitoi taswira sahihi ya maana ya demokrasia ya vyama vingi vinavyotakiwa kushindana kwa sera”.

Aliongeza kusema”vyama vyetu vinatakiwa vishindane kwa ubora na sera…hatushindani kwa vitisho, hatushindani kwa ngumi wala kumwagiana tindikali au kuwachomea watu nyumba zao”.

Mukama aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kunadi sera na mipango ya vyama vyao katika mikutano yao ya kampeni kisha waachie wananchi wa Igunga waamue wenyewe siku ya kupiga kura Oktoba.

Alisema tukio hilo limesaidia kuwaonyesha Watanzania Chadema ni chama cha aina gani na kuwataka wananchi Igunga kuhakikisha wanakiadhibu kwa kukinyima kura ili iwe fundisho kwao.

Mukama alivitaka vyombo vya dola kuhakikisha vinawasaka na kuwatia nguvuni wale wote waliohusika na tukio hilo na baadae kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria ili waadhibiwe kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa chama cha wananchi (CUF) kata ya Nyandekwa,Emanuel Ezekiel aliyefika sambamba na Mukama kutoa pole, alilaani tukio hilo akisema linatishia mustakabali wa amani ya Igunga.

Naibu kamishina wa polisi ambaye ndiye msemaji wa matukio yote ya uhalifu yanayotokea Igunga, Isaya Mngulu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema tayari polisi wameanza upelelezi na kuwasaka waliohusika.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages