Breaking News

Your Ad Spot

Sep 3, 2011

MAZISHI YA MTOTO ALIYEGONGWA NA LORI IGUNGA: CCM YATOA UBANI SH. MILIONI MOJA, CHADEMA LAKI MOJA NA ISHIRINI ELFU

NA NKOROMO DAILY, IGUNGA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) leo kilikuwa mstari wa mbele katika maandalizi na mazishi ya mtoto aliyegongwa na lori mjini hapa jana.

Katika msiba huo CCM imetoa rambi rambi ya sh. milioni moja, CHADEMA  nao wakitoa sh. laki moja na elfu ishirini na vyama hivyo viliwakilishwa na uongozi wa kitaifa, wakati CCM ikiongozwa na Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Mwigulu Nchemba CHADEMA waliwakilsihwa Mwita Mwikwabe ambaye ndiye mratibu wa Kampeni za chama hicho jimboni hapa.

Peter Ezekiel  (12) alikufa papo hapo baada ya kugongwa na lori la mizigo lililokuwa likitokea Nzega kwenda
Singida, alipojaribu kukatiza barabara akitokea katika umati wa wananchi waliokuwa wakisubiri msafara wa
mgombea ubunge jimbo la Igunga kwa tiketi ya CCM,  Dk. Peter Kafumu.

Dk. Kafumu na msafara wake akiwemo mratibu wa kampeni za CCM jimboni humo, Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Mwigulu Nchemba walikuwa wanatokea Singa kwenda kuchukua fomu kwa Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Igunga.

Baada ya mtoto huyo kugongwa na kufariki papo hapo mgombea huyo na msafara wake waliamua kusitisha
kwa muda kazi aliyokuwa amefuata ya kuchukua fomu hizo na badala yake wakashiriki kuuchukua mwili
kutoka eneo la tukioo kuupeleka hospitali.

Katika mazishi mgombea wa CCM, Viongozi wote wa CCM na wilaya ya Igunga na mamia ya wanachama
walishiriki tangu kuandaa mazishi ikiwemo kununua sanduku la kuhifadhia mwili hadi kuupeleka mwili makaburini.

Akizungumza wakati wa mazishi hayo yaliyofanyika katika makaburi yaliyopo nje kidogo ya mji wa Igunga,
Kulwa Mpina ambaye  ni mama mdogo wa marehemu, alisema wamefarijika sana na hatua iliyochukuliwa na
CCM kusaidia katika msiba huo mzito.

"Kwa kweli sisi familia yetu tutampigia kura mgombea wa CCM ili ashinde katika uchaguzi huu na kuwa
kumbukumbu ya marehemu mtoto wetu", alisema huku akibubujikwa machozi.

"Tunajua CCM haikuhusika kwa vyovyote na kifo hiki, lakini imeamua kuchukua jukumu la kuwa karibu nasi
kwa  sababu mbali na kwamba tulikuwa naye katika kusubiri  msafara wa mgombea lakini sisi na mtoto huyu ni wakazi wa jimbo hili", alisema Kashinde Raphael aliyejitambulisha kuwa ni mwanafamilia ya marehemu.

Katika uchaguzi mdogo jimbo la Igunga CCM imemsimamisha Dk. Kafumu kugombea katika uchaguzi huo
ambao unafanyika kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Rostam Aziz (CCM) baada ya kujiuzulu.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu baada ya kampeni zitakazorindima kwa wiki
kadhaa baada ya kuanza rasmi Septemba 7, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages