UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898 E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com Fax: 255-22-2113425 | | PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Jakaya Kikwete akiwa na kamati ya Okoa maisha Somalia |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Ijumaa, Septemba 2, 2011, amezindua rasmi Kamati ya Kitaifa ya Misaada ya Kibinadamu kwa Somalia ijulikanayo kama “Kamati ya Okoa Maisha Somalia” katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Katika shughuli hiyo, Rais Kikwete amewashukuru wajumbe wa Kamati hiyo kwa kukubali kuongoza operesheni ya kuchangisha misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wananchi kiasi cha milioni 3.5 wanaokabiliwa na njaa katika Somalia, kati yao 400,000 wakiwa mjini Mogadishu.
Inakadiriwa kuwa wastani wa watu kati ya 50 na 100, wengi wao wakiwa watoto na akinamama, wanapoteza maisha yao katika nchi hiyo kwa sababu ya balaa hilo la njaa kila siku.
Wajumbe wa Kamati hiyo ambao wote ni wafanyabiashara maarufu ni Bwana Reginald Mengi, Bwana Saidi Bakharesa, Bwana Gulam Dewji, Bwana Haruna Zakaria na Balozi Saidi Shamo, ambao kwa pamoja wameanzisha michango hiyo ya misaada kwa wao kutangaza michango yao binafsi mbele ya Mheshimiwa Rais Kikwete.
Akitangaza michango yao mbele ya Mheshimiwa Rais, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bwana Mengi amesema kuwa yeye atachangia kontena moja ya maji safi ya kunywa, Bwana Bakhressa atatoa tani 50 za unga wa ngano, Balozi Shamo atatoa biskuti maalum za kushibisha kiasi cha tani tano, Bwana Zakaria atatoa tani 50 za mafuta ya kupikia na tani 50 za sabuni ya unga ya kufulia na Bwana Dewji atatoa tani 50 za unga wa mahindi.
Bw. Mengi amemwambia Mheshimiwa Rais Kikwete kuwa misaada hiyo ya wafanyabisahara hao watano itaweza kujaza makontena 11 ya futi 20 kila moja ambayo yako tayari kusafirishwa wakati wowote kuanzia sasa kupelekwa Somalia.
Chimbuko la Kamati hiyo ni mwito wa Mheshimiwa Rais Kikwete alioutoa wakati alipomwandalia futari ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan Rais wa Somalia, Mheshimiwa Sheikh Ahmed Sheikh Shariff wakati alipotembelea Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku moja mwezi uliopita.
Mheshimiwa Sheikh Shariff ambaye alikuwa nchini kumweleza Rais Kikwete kuhusu hali ilivyo katika Somalia na balaa ya kibinadamu linaloikabili nchi hiyo, pia aliomba msaada kutoka kwa Tanzania na wananchi wa Tanzania katika kukabiliana na balaa hilo.
Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Rais Kikwete alitangaza msaada wa tani 300 za mahindi zenye thamani ya kiasi cha dola za Marekani 200,000 kwa wananchi hao na Somalia na pia alitoa mwito kwa Watanzania wenye uwezo, na hasa wafanyabiashara, kujitokeza kutoa michango na misaada ya kibinadamu ili kusaidia ndugu zetu wa Somalia.
Akizungumza na wafanyabiashara hao, Rais Kikwete amewaambia: “Mmetupa heshima kubwa sana. Kwa hakika kutoa ni moyo. Tunawaomba msaidie kuendesha operesheni hii ya kukusanya misaada mbalimbali kutoka kwa wananchi na sisi katika Serikali tutafanya utaratibu wa kuifikisha misaada hiyo Somalia. Kuanzia dakika hii Kamati yenu sasa inatambuliwa rasmi kama kamati ya taifa letu kwa ajili ya misaada kwa ndugu zetu wa Somalia.”
Kwa hatua hiyo, Tanzania inaungana na nchi chache duniani, ikiwamo Afrika Kusini, ambazo zimeanzisha michango kwa ajili ya misaada ya kukabiliana na zahama la kibinadamu katika Somalia
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
Dar es Salaam.
02 Septemba, 2011
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269