Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Afrika imeridhishwa na msimamo wa Jumuia ya Madola kuendelea kuhakikisha kuwa suala zima la maendeleo linabakia sehemu ya ajenda kuu ya Jumuia hiyo.
“Sisi wanachama wa Jumuia ya Madola kutoka Afrika, na kwa hakika Bara zima la Afrika, tumeridhishwa na yaliyojadiliwa na kukubaliwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuia ya Madola ya Madola (CHOGM) mwaka huu kuhusiana na umuhimu wa suala zima la maendeleo,” Rais Kikwete amesema kwenye mkutano wa waandishi wa habari wa kufunga mkutano wa CHOGM mwaka huu mjini Perth, Australia.
Rais Kikwete alikuwa mwakilishi na msemaji wa nchi wanachama wa Jumuia ya Madola kutoka Afrika kwenye mkutano huo wa waandishi wa habari ambako amejiunga na Waziri Mkuu wa Australia, Mama Julia Gillard ambaye alikuwa mwenyeji wa CHOGM mwaka huu na mwenyekiti mpya wa Jumuia hiyo.
Viongozi sita wamehutubia mkutano huo wa waandishi wa habari wengine wakiwa Waziri Mkuu wa Trinidad na Tobago Mheshimiwa Kamla Persad-Bissessar ambaye ndiye mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Waziri Mkuu wa Visiwa vya Samoa Mheshimiwa Tuilaepa Lupesoliai Sailele Malielegaoi, Rais wa Visiwa vya Maldives Mheshimiwa Mohamed Nasheed na Katibu Mkuu wa Jumuia, Mheshimiwa Kamaleshi Sharma ambaye ameongezewa kipindi kingine cha miaka minne cha kuongoza Jumuia hiyo kwenye CHOGM ya mwaka huu kuanzia Aprili mwakani.
Rais Kikwete amesema kuwa nchi za Afrika na zile zote zinazoendelea ndani ya Jumuia ya Madola zimeridhishwa na msimamo wa CHOGM wa kuibakiza ajenda ya maendeleo kwenye ajenda kuu ya Jumuia hiyo.
Rais Kikwete alikuwa ameulizwa kama nchi masikini zaidi na ndogo zaidi ndani ya Jumuia zimemeridhishwa na ajenda zilizowekewa mkazo katika CHOGM ya mwaka huu na hasa ajenda ya maendeleo.
Rais amesema kuwa ajenda ya maendeleo lazima iendelee kubakia ajenda kuu ya Jumuia ya Madola kwa sababu sehemu kubwa ya wanachama wa Jumuia hiyo ni nchi masikini na zinazoendelea.
Kwenye mkutano huo, viongozi hao wameelezea mambo makubwa yaliyokubaliwa katika mkutano huo ikiwa ni pamoja na kufanya mageuzi makubwa ndani ya Jumuia hiyo kuhakikisha kuwa Jumuia hiyo inabakia taasisi yenye nguvu, yenye kutumikia kiasi cha kuridhisha mahitaji ya nchi wanachama wake na yenye uwezo wa kupambana na changamoto za karne ya 21.
Moja ya mageuzi yaliyokubaliwa yafanyike ni pamoja na kuimarisha kundi la kusaidia utendaji ndani ya Jumuia ambalo linaundwa na mawaziri la Commonwealth Ministerial Action Group (CMAG) na Tanzania imeteuliwa kuwa katika kundi hilo kwa miaka miwili ijayo.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingine zitakazounda CMAG kwa miaka miwili ijayo mpaka mkutano ujao wa CHOGM ni Australia, Bangladesh, Canada, Jamaica, Maldives, Sierra Leone, Trinidad na Tobago na Vanuatu.
Viongozi hao wamesema kuwa katika CHOGM ya mwaka huu viongozi wa Jumuia ya Madola wamekubaliana kuendelea kutetea, kulinda na kudumisha misingi mikuu ya Jumuia hiyo ambako viongozi wamepitisha ma kukubali mapendekezo 30 kati ya 105 yaliyopendekezwa na Kundi la Watu Maarufu (Eminent Persons Group) wa Jumuia hiyo.
Viongozi hao pia wamewaambia waandishi wa habari kuwa CHOGM imekubaliana kuelekeza nguvu zaidi kwenye mahitaji ya maendeleo ya nchi wanachama ambako suala la usalama wa chakula litatiliwa mkazo mkubwa.
Waziri Mkuu Gillard ambaye ameongoza mkutano huo wa waandishi wa habari amesema pia kuwa CHOGM imekubaliana kushirikiana na washirika wa kimataifa wa Jumuia ya Madola katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo makubwa ya kiuchumi yanayoikabili dunia kwa sasa.
Mama Gillard pia amesema kuwa viongozi wamekubaliana kuongeza nguvu zao katika kutafuta usawa wa jinsia na kuwasaidia vijana kuwa na sauti kubwa zaidi ndani ya Jumuia hiyo.
Aidha, amesema kuwa viongozi wa Jumuia ya Madola wamekaribisha nia ya Sudan Kusini kutaka kujiunga na Jumuia na wametaka Makao Makuu ya Jumuia ya Madola kufuatilia suala hilo.
Pia, Mama huyo amesema kuwa wakuu wa CHOGM wameridhishwa na mazingira yanayojengeka kutaka kuikaribisha tena Zimbabwe kwenye Jumuia hiyo na wamezipata pande zote nchini humo kuendelea kutekeleza makubaliano ya kuleta maridhiano nchini humo ya Global Political Agreement (GPA).
Waziri Mkuu huyo pia amesema kuwa CHOGM imekubaliana kumpongeza Mkuu wa Jumuia ya Madola, Malkia Elizabeth wa Uingereza, kwa kufikisha miaka 50 ya uongozi wake wa Jumuia mwaka ujao. CHOGM imekaribisha wazo la kuanzisha taasisi iitwayo Queen Elizabeth Diamond Jubilee Trust ambayo kazi yake kuu itakuwa kugharibia miradi ya kibinadamu kama vile maradhi, kuendeleza elimu na utamaduni na shughuli nyingine za kipaumbele za Jumuia ya Madola.
Mama Gillard pia amewaambia waandishi wa habari kuwa CHOGM imeridhia kuwa mkutano wake ujao ufanyike Sri Lanka mwaka 2013, unaofuata ufanyike Mauritius mwaka 2015, na unaofuata ufanyike Malaysia mwaka 2019.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269