Breaking News

Your Ad Spot

Oct 8, 2011

SERIKALI YAWAONYA WACHIMBAJI WADOGO GEITA KUHUSU VURUGU

Na mwandishi wetu
SERIKALI imeowaonya wachimbaji wadogo wilayani Geita kuacha mara moja vurugu na kuvamia kuchimba dhahabu maeneo ambayo hawajaruhusiwa.
Imesema itawachukulia hatua kali wafanyabiashara wanachochea wachimbaji wadogo kuvamia maeneo ya machimbo pamoja na kufanya vurugu katika maeneo mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa Mwanza, Evarist Ndikilo alipozungumza na kundi la wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyaruyeye kilichopo kata ya Nyarugusu, ambao juzi walifanya vurugu pamoja na kuvamia kituo cha Polisi.
Pia, alibaini kuwa machimbo hayo yanamilikiwa kihalali na Kampuni ya Mawe Meru Resources, ambayo kwa sasa imeingia mkataba wa ubia kuratibu na kusimamia shughuli za uchimbaji.
Katika vurugu hizo mtu mmoja aliuawa kufuatia kundi la wachimbaji zaidi ya 500 kuvamia kituo cha Polisi kwa lengo la kuteka askari, ambapo jitihada zilifanyika na kudhibitiwa kwa kutumia mabomu ya machozi.
Ndikilo alisema taratibu za kuchimba dhahabu katika eneo waliovamia wachimbaji hao hazijakamilika na kwamba, wanapaswa kuwa na subira kwani vurugu zao zinaweza kuifanya serikali kusitisha mchakato huo.
“Hatutavumilia vurugu zenye kuhatarisha amani, naomba vurugu zikome mara moja na tuwe na subira wakati taratibu za kisheria za uchimbaji katika eneo hili zikiendelea,” alisema Ndikilo.
Habari kutoka eneo la tukio zimesema, wachimbaji hao waliondolewa katika machimbo ya Nyaruyeye wiki tatu ilizopita baada ya kuvamia eneo hilo na kuanza kuchimba dhahau bila kibali.
Wachimbaji walivamia wakati machimbo hayo yakiwa chini ya ulinzi wa polisi ili kutoa fursa za taratibu za kisheria kukamilika ikiwa ni pamoja na kuomba kibali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwa, eneo hilo lipo kwenye hifadhi ya misitu.
Amri ya kuondolewa kwa wachimbaji hao ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Geita Philemon Shelutete, baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama kufikia uamuzi huo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Baraka Nyandu, alisema kuwa mchakato wa kukamilisha taratibu za uchimbaji kwenye eneo hilo zimekamilika.
Nyandu, ambaye ni mbia aliyepewa mamlaka ya kusimamia uchimbaji katika machimbo hayo na mmiliki mwenye leseni halali Kampuni ya Mawe Meru Resources, alisema tayari mkataba wa shughuli katika eneo hilo umekamilika.
Alisema kuwa kinachosubiriwa kwa sasa ni kibali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na kwamba, eneo hilo lina vibali vyote halali kutoka serikalini.
“Hapa tunavyozungumza niko katika ofisi za Maliasili kufuatia kibali na taratibu zote zimekamilika hivyo, nawaomba wachimbaji wenzangu watulie ili tukamilishe taratibu zote,” alisema.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwepo kwa wafanyabiashara wa madini wanachochea vurugu hizo kwa maslahi binafsi kwa kufadhili maandamano.
Tayari serikali mkoani hapa na vyombo vya usalama vimesema kuwa inawatambua wafanyabiashara hao na kwamba, haitakuwa na simile ni lazima hatua za kisheria zichukuliwe.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages