Mndeme |
SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC), limesema kuwa taarifa zilizochapishwa katika gazeti la moja la kila siku dhidi ya Postamasta Mkuu Deos Mndeme, hazina ukweli wowote na zimelenga kumchafua mbele ya jamii.
Awali, gazeti hilo lilichapisha habari zikidai kuwa Mndeme anakabiliwa na tuhuma nzito ikiwemo kuingia mikataba mibovu na kunyanyasa wafanyakazi wa chini, tuhuma ambazo halina ukweli wowote.
Pia, limesema kuwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa hahusiki kwa namna yoyote ile katika kufanikisha mkataba huo kwa kuwa ulifuata sheria, kanuni na taratibu zote za TPC.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na kusainiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TPC, Dk. Yamungu Kayandabila, imesema kuwa tuhuma zote zilizoelekezwa kwa Mndeme hazina ukweli na ni upotoshaji wa wazi.
Kuhusu mikataba iliyoingia TPC na kampuni binafsi, Dk. Kayandabila alisema kuwa shirika hilo ni wakala wa kampuni na taasisi mbalimbali ikiwemo TANESCO, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Vodacom, Tigo, Zantel na nyingine nyingi katika kushirikiana kutoa huduma kwa wananchi.
Alisema kwa kuzingatia kuwa shirika hilo lina mtandao mpana kwa kuwa na ofisi zake nchi nzima na kwamba, uhusiano huo si wa kukodisha majengo yake kama ilivyodaiwa na gazeti hilo.
Akitoa ufafanuzi juu ya wizi wa mamilioni ya shilingi kupitia huduma za usafirishaji fedha (EMS), Dk. Kayandabila alisema suala hilo limefikishwa katika ngazi husika na linafanyiwa kazi na iwapo tuhuma hizo zitadhihirika hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa.
"Shirika lina washirika wengi kibiashara ambao hutumia mtandao wake uliopo nchi nzima. Hii ni utekelezaji wa sera yake ya kuwa Multi Agent, hivyo uhusiano huo si majengo bali kihuduma," alisema katika taarifa yake.
Akizungumzia tuhuma juu ya Mndeme kuwa hana ushirikiano na watendaji wa chini yake, Dk. Kayandabila alisema vikao vya mara kwa mara hufanyika baina ya Postamasta Mkuu na watendaji wake vyenye dhana ya ushirikishwaji ili kujenga maelewano na kutoa maamuzi yenye mwelekeo wa kuboresha utendaji kazi.
Kuhusu tuhuma kuwa watumishi wa TPC wana maslahi duni, alisema kuwa ni vyema ieleweke kuwa maslahi kwa wafanyakazi wa shirika hilo yanatolewa kwa kuzingatia uwezo wake kiuchumi.
Alisema makubaliano kati ya Manejimenti na wawakilishi wa wafanyakazi na idhinisho la Bodi ya TPC, Msajili wa Hazina huzingatiwa na sio vinginevyo kama taarifa ilivyotolewa yenye lengo la kupotosha umma kuwa maamuzi yanafanywa na Postamasta Mkuu.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269