Breaking News

Your Ad Spot

Oct 13, 2011

VODA YATANGAZA ZAWADI ZA MWANZA OPEN CYCLE CHALLENGE

Waandaji na wadhamini wa mbio za baiskeli zijulikanazo kama “Vodacom Mwanza Open Cycle Challenge” wametangaza zawadi zitakazotolewa kwa washindi mbalimbali watakaoshiriki mashindano ya mbio hizo zitakazofanyika kuanzia Shinyanga mjini mpaka jijini Mwanza mwezi huu,Mashindano hayo yanagharimu zaidi ya shilingi milioni 50.

Akizungumza naWaandishi wa Habari, Jijini leo, katika makao makuu ya Vodacom Tanzania yaliyopo Mlimani City Meneja Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Rukia Mtingwa alisema kwamba mashindano ya mwaka huu yameboreshwa zaidi na kuwaomba waendesha baiskeli kujitokeza kwa wingi.

“Mashindano haya yameboreshwa kwa upande wa zawadi, ubora na viwango,” alisema.

Aidha alifafanua kuwa mashindano hayo yatafanyika kwa siku moja yaani October 22  mwaka w huu na kwamba tarehe 22 itakuwa maalumu kwa mashindano ya kilomita 196 kwa wanaume, 80 kwa wanawake ambapo kwa upande wa walemavu ni Kilometa 15 kwa walemavu wanaume na Kilomita 10 kwa walemavu wanawake.

Akitangaza zawadi hizo kwa washiriki wa mbio za kilometa 150 Mtingwa alisema mshindi wa kwanza atajipatia shilingi 1,500,000, wa pili kiasi cha 1,000,000, wa tatu 700,000, ambapo mshindi wa nne hadi wa kumi kila mmoja atajipatia shilingi 500,000 kila mmoja. Aidha kwa upande washindi wa 11 hadi 20 kila mmoja atajinyakulia kitita cha 250,000 kila mmoja, na kuanzia mshindi wa 21 hadi wa 30 watapatia shilingi 150,000 kila mmoja.

Kwa upande wa mbio za mita 80 kwa wanawake mshindi wa kwanza pia atajipatia zawadi ya shilingi milioni 1,100,000, wa pili 800,000, mshindi wa tatu 600,000, wakati washindi wa nne hadi wa kumi kila mmoja atazawadia kiasi cha shilingi 350,000 kila mmoja. Vilevile washindi watakaoshika nafasi ya 11 hadi ya 20 katika mbio hizo  watazawadiwa 130,000 kila mmoja, na kuanzia mshindi wa 21 hadi wa 30 watapatia shilingi 100,000 kila mmoja.


Mbali na hayo Mtingwa alibainisha kwamba kwa upande wa mbio za kilometa 15 ambazo zitawashirikisha watu wenye ulemavu alisema washindi wa kwanza wawili kila mmoja atajipatia jumla ya shilingi 500,000.

Kwa washindi wa pili wawili nao watajishindia kiasi cha shilingi 250,000 kila mmoja, washindi wa tatu wawili kila mmoja atapewa kiasi cha 150,000 kila mmoja wakati washindi wa nne wane  hadi wa kumi watajipatia kitita cha 100,000 kila mmoja.Na watakaoshika nafasi ya 11 hadi ya 20 katika mbio hizo  watazawadiwa kiasi cha shilingi 70,000

Vile vile, Mtingwa alisema kuwa katika kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Vodacom itatoa zawadi maalum kwa mshiriki atakaekuwa na umri wa miaka 50 kwenda mbele atakaemaliza mbio ndani ya washiriki 50 wa kwanza. Upande wa wanaume atajipatia sh laki 3 na sh laki 2 kwa wanawake.                                           

Aidha alifafanua kuwa mashindano ya mwaka huu ya Vodacom Mwanza Open Cycle Challenge yameandaliwa na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania kwa takribani miaka sita sasa na mwaka huu yamedhaminiwa na Serengeti Breweries kwa kupitia kinywaji chake cha Malta na CloudsFM.

“Shindano hili la Vodacom Mwanza Open Cycle Challenge ni mahususi kwa kukuza mchezo huu hapa nchini kwa lengo la kupata wawakilishi bora katika mashindano mbalimbali ya kimataifa,” alifafanua.

Alisema kampuni yake imekuwa ikidhamini michezo mbalimbali kama vile Soka, Riadha, kuogelea, mashindano ya boti, mashindano ya Mbuzi, Vodacom Miss Tanzania, Tenisi na mingine mingi ili kuhakikisha kwamba taifa linafanya vizuri katika tasnia nzima ya michezo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages