Breaking News

Your Ad Spot

Nov 16, 2011

SERIKALI YATOA TAMKO VURUGU ZA MBEYA NA TABORA

Serikali imetoa tamko kuhusu vurugu zilizotokea mjini Mbeya na Tabora na kusema haitavumilia vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani nchini.

Tamko hilo lilitolewa Bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Kagasheki,, alipotoa kauli ya serikali kuhusu vurugu hizo zilizotokea mwishoni mwa wiki iliyopita.

Alisema vurugu haziwezi kuwa njia ya kuondoa migogoro au kumaliza matatizo na kuwa  serikali haitavumilia vurugu, nchi  inaongozwa kwa sheria na kuwataka wananchi kufuata sheria bila shuruti.

Baada ya Kagasheki kuwasilisha tamko hilo la serikali, John Mnyika (Ubungo-CHADEMA), alisimama na kumwomba spika wabunge wajadili tamko hilo.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alimtaka kuwasilisha hoja hiyo kwa utarabu mwingine, ambao hakuufafanua.

Mnyika alitaka kuungwa mkono ili tamko hilo lijadiliwe, hata hivyo, aliungwa na wenzake wa CHADEMA tu.

Kagasheki alisema vurugu zilizotokea Mbeya Ijumaa na Jumamosi iliyopita zilisababisha mtu mmoja kufariki dunia na wengine 14 kujeruhiwa wakati mgambo walipokuwa wakiwaondoa machinga katika eneo la Mwanjelwa.

Alisema wakati mgambo wakiteke agizo la Halmashauri ya Jiji la Mbeya, wafanyabiashara hao na vijana wengine waliwazingira na walipozidiwa waliomba msaada polisi.

Naibu waziri alisema vurugu zilisambaa, ambapo barabara ya Mbeya –Iringa ilifungwa kwa muda kwa magogo na mawe. Alisema watu 350 walikamatwa kutokana na vurugu hizo, ambapo baada ya kuhojiwa 34  walifikishwa mahakamani na wameachiwa kwa dhamana.

Kuhusu vurugu za mkoani Tabora zilizotokea Jumamosi iliyopita, alisema zilisababishwa na mmoja wa wanafunzi wa uaskari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kambi ya Msange.

Alisema askari huyo alikwenda soko kuu la Tabora ambako alipenda nguo ya sh. 20,000, ambapo aliomba apunguziwe bei na alipokataliwa alisema imefanana na sare ya jeshi hivyo kuondoka nayo.

Kagasheki alisema mwenye duka aliomba msaada kwa wenzake na kumnyang’anya nguo hiyo, ambapo askari huyo alikwenda kuwaita wenzake waliofika na kushambulia wananchi.

Kutokana na vurugu alisema vibaka na watu wasio waaminifu waliiba bidhaa, ambapo watuhumiwa 90 walikamatwa na katika gwaride la utambuzi askari 51  walitambuliwa na katika la pili walitambuliwa tisa, ambao wote wamefikishwa mahakamani.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages