Nape Nnauye |
Na Mwandishi Wetu, Arusha
Waliokuwa wakisubiri kwa hamu hasa Mbunge wa Arusha mjini Gdbles Lema (CHADEMA) kumuona Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nauye anapanda kizimbani katika mahakama mjini Arusha wameangukia pua.
Hali hiyo imetokea baada ya ukweli kufichuka katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwamba Nape hakutamka maneno yaliyoandikwa na gazeti la Nipashe Jumapili ambayo mahakama hiyo imeyachukulia kuwa ni kuingilia uhuru wa mahakama.
Katika Mahakama hiyo Mhariri mtendaji wa gazeti hilo Flora Wingia alipanda kizimbani na kutamka kwamba yaliyoandikwa katika gazti hilo hayakuwa yametamkwa na Nape bali gazeti lilimlisha kwa makosa.
Kufuatia kauli yake Mhariri huyo aliomba kuiomba radhi mahakama hiyo, Nape pamoja na Godbles Lema ombi ambalo mahakama hiyo ililikubali. Wingia aliomba kuomba radhi na kukanusha katika ukurasa wa mbele wa gazeti hilo.
Awali akiongozwa na wakili Michael Ngalo anayemtetea mhariri huyo mahakamani hapo kutoa ufafanuzi wa habari iliyoandikwa na gazeti hilo ikimnukuu Nauye kuingilia kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi ya ubunge wa jimbo la Arusha inayoendelea mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa maelezo ya wakili wa Mbunge Lema, Method Kimomogolo alidai kuwa katika habari hiyo Nape alinukuliwa akisema kuwa ana uhakika wa kushinda kesi hiyo inayoendelea na kisha kulikomboa jimbo hilo kama ilivyokua Igunga.
Akitoa utetezi wake Mhariri huyo alisema mara baada ya kupitia habari hiyo iliyoandikwa na mwandishi wa kujitegemea Beatrice Shayo baada ya kupokea wito wa mahakama hiyo aligundua kuwepo kwa maneno aliyolishwa Nape ambayo hakuyasema katika hotuba yake.
Wingia aliongeza kuwa mbali ya kupata maelezo kutoka kwa mwandishi wake huyo pia alizungumza na waandishi wa magazeti ya Mzalendo na Mwananchi waliokuwepo siku ya tarehe 8 Oktoba katika mkutano wa mapokezi ya mbunge mteule wa jimbo la Igunga Dk.Dalali Kafumu uliofanyika Manzese jijini Dar es salaam ambapo walimueleza kuwa maneno hayo yanayolalamikiwa Nape hakuyazungumza.
Alisema kutokana na majibu hayo alilazimika kukubali kosa na kuomba radhi walengwa watatu ambao waliathirika na habari hiyo ikiwemo mahakama, Nape na Godbles Lema katika ukurasa aidha wa tano wa gazeti ambao ndiyo ulichapisgha habari hiyo au hata ukurasa wa mbele.
"mheshimiwa jaji baada ya kupokea wito huu nilipata nafasi ya kuzungumza na mwandishi huyu pamoja na wengine wa magazeti ya Mwananchi na Mzalendo ambao walikuwepo katika mkutano huo lakini waliniambia maneno hayo Nape hakutamka na ndiyo maana hata wao hawakuandika"alisema Wingia.
Aidha Wingia aliongeza kuwa kutokana na mapungufu hayo alikiri kuwepo kwa uzembe katika kutolewa kwa habari hiyo kwakua alipaswa kutafuta na upande wa pili ambao ni Nape ili kujua kama ni kweli aliyasema hayo au la.
Alisema uzembe huo ulitokana na kushindwa kumtafuta Nape kutokana na muda kuwa mfupi kwani habari hiyo waliipata majira ya jioni hali iliyomsababisha kushindwa kutafuta ukweli wa habari hiyo na kulazimika kuipeleka mtamboni.
Pamoja na kukiri huko kosa Jaji anayesikilizima kesi hiyo Aloyce Mujulizi aliamuru Mhariri huyo kuapishwa ili aweze kuhojiwa na mawakili ambapo alihojiwa na wakili Kimomogolo iwapo mhariri huyo alizungumza na Nape kujua kwanini alizungumzia suala la kesi ya Arusha wakati alikua katika mapoekezi ya mbunge wa Igunga swali ambalo Wingia alijibu kuwa hakumuuliza.
Pia Kimomogolo aliomba apewe muda wa kuzungumza na mteja wake Godbles Lema iwapo ameridhika na maamuzi hayo kwakua awali alisema kutokana na habari hiyo amepoteza imani na jaji anayesikiliza kesi hiyo na kupendekeza ajitoe.
Nae wakili wa serikali Angela Chacha alimuuliza Mhariri huyo iwapo tangu kuchapishwa kwa habari hiyo Nape aliwahi kuilalamikia swali ambalo Wingia alimjibu kuwa Nape hakuwahi kuilalamikia kwakua hakuwahi kuiona kwakua hakusoma gazeti hilo.
Nae wakili wa walalamikaji katika kesi hiyo Alute Mughwai akimuhoji mhariri huyo aliuza iwapo Nape aliwahi kuiona kabla ya kupokea malalamiko hayo ambapo alijibiwa kuwa Nape binafsi aliiona na kuisoma baada ya kupokea malalamiko hayo na kukana kuzungumza maneno hayo.
Aidhwa Mughwai alionya juu ya kuendelea kuvutana katika kesi hiyo na kusababisha kushindikana kuanza kusikilizwa kwake kutokana hoja za kumtaka jaji ajitoe kwakua malalamiko ya msingi na majibu yake yamemaliza vipengele vyote.
"mheshimiwa jaji nimkumbushe wakili mwenzangu kuhusu muda kwakua kutokana na kauli yake asije akaturudisha nyuma kwa hoja za kukutaka kujitoa katika kesi hii kwakua mhariri ameeleza kuwa aliipotosha habari hiyo hivyo suala la msingi lilikua hilo hivyo hakuna tatizo tena"alionya Mughwai.
Awali wakili Jerome Msemwa alimueleza jaji anayesikiliza kesi hiyo kuwa Nape alishindwa kufika mahakamani hapo kutokana na kupatwa na ugonjwa wa ghafla hapo jana muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kuja mkoani Arusha kuitikia wito wa mahakama.
Alisema Nape alikua tayari na tiketi ya ndege ya kampuni ya Precuision Air namba 432 iliyokua iondoke Dar saa 12.30 jioni na kufika Arusha saa 1.30 usiku lakini alishindwa kutokana na sababu hizo.
Alisema Nape baada ya kupatwa na ugonjwa huo wa ghafla alilazimika kulazwa katika hospitali ya Mission iliyoko MIkocheni jijini Dar es salaam kwaajili ya matibabu ambapo hadi muda anazungumza mahakamani hapo Nape alikua bado yupo hospitalini hapo.
Akiahirisha kesi hiyo Jaji Mujulizi alisema amejiridhisha na utetezi uliotolewa na mhariri huyo na kwamba amekubali ombi la kuomba radhi na kumtaka aombe radhi katika ukurasa wa kwanza wa gazeti hilo na kukanusha habari hiyo.
Aidha alivionya vyama vya siasa,wanasiasa na wanahabari kuacha utani na kuingilia mwenendo wa kesi mbalimbali hususani hiyo kwa kutamka au kuandika maneno yanayolenga kudharau na kwamba mambo hayo sio maigizo bali ni mambo yako hai na yanawahusu watu ambao wako hai.
Pia alisema ni zaidi ya uzembe kwa chombo chochote cha habari kushindwa kueleza habari ya ukweli kwa kushindwa kuipitia habari yake kwa kumtegemea mwandishi pekee.
Pia alionya juu ya suala la ucheleweshaji wa kesi hiyo kuanza kusikilizwa kuwakua awali walikubaliana kutokuwepo na upotezaji wa muda na kama kuna mtu bado ana madai ya kutaka jaji ajitoe ni vyema akaenda katika mahakama ya rufaa kwaajili ya hilo na sio kuzua mijadala mipya tena.
"mimi sitegemei kuwepo mtu yeyote atakayeleta utani katika usikilizaji wa kesi hiyo kila mtu anapaswa kuwa makini na muda tunaokwenda nao sasa sio tena tuje tarehe tutakayoapanga halafu mtu alete hoja yake hiyo"alisema Mujulizi.
Awali jaji Mujulizi alieleza mahakamani hapo kuingilia mahakama kwa kuandika habari zenye utata ni kosa la jinai ambalo iwapo mtu atapatikana na hatia hiyo atakabiliwa na hukumu ya kifungo cha miezi 6 jela au kutoa fidia ya shilingi 500,000 ambapo Nipashe imezikwepa hukumu hizo kwa kuamua kukiri kosa na kuomba radhi.
Aidha alisema kutokana na kipindi hichi kuwa mwisho wa mwaka ambapo shughuli zote za mahakama zinasimamishwa kwaajili ya mapumziko ya mwisho wa mwaka analazimika kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 6 mwaka 2012 ambapo shauri hilo litaanza kusikilizwa mahakamani hapo. UHURU, NOV 17
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269