Mhe. Ombeni Sefue, |
Na Mwandishi Maalum, New York
Wakati maandalizi ya mkutano wa kimataifa kuhusu Maendeleo Endelevu ( United Nations Conference on Sustainable Development) maarufu kama RIO+20 yakiwa yanaendelea, Afrika imetoa vipaumbele vyake ambavyo inataka vizingatiwe wakati wa mkutano huo unaotarajiwa kufanyika mwezi Juni,2012, Rio de Janairo, Brazil.
Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe.Ombeni Sefue (pichani) akizungumza kwa niaba ya kundi la nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa. Amesema vipaumbele hivyo vinapashwa kuzingatiwa kwa kuwa ni muhimu katika kufikia malengo ya kuondoa umaskini hasa kwa Afrika kupitia mkakati mpya wa uchumi wa kijani.
Anavitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na, uboreshaji wa uzalishaji wa kilimo na usalama wa chakula, kupambana na kudhibiti kuenea kwa jangwa na uharibifu wa ardhi, usimamizi wa mazingira ya bahari, uimarishaji wa matumizi endelevu ya maliasili ikiwa ni pamoja na maji safi, misitu na viumbe hai.
Vipaumbele vingine ni kukuza matumizi na uzalishaji endelevu na maendeleo ya viwandani na kuhakikisha usimamiaji wa kemikali taka, kukuza utalii endelevu na kuhakikisha upatikanaji wa nishati salama na endelevu.
Kwa siku mbili wadau mbalimbali wakiwamo mabalozi walikutana katika majadiliano ya ya siku mbili hapa Umoja wa Mataifa ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili maandalizi ya mkutano huo muhimu na ambao utawakutanisha wadau mbalimbali kutoka duniani kote, wakiwamo wakuu wa nchi na serikali, wanadiplomasia, wanasiasa, wataalamu wa masuala ya maendeleo endelevu, mazingira , tasisi binafsi na za kiraia.
Balozi Sefue anasema ni matarajio ya Afrika kwamba, washiriki wa mkutano huo siyo tu watajituma bali pia wataonyesha utashi wa kisiasa katika kuhakikisha kwamba mkutano huo unafanikiwa na kutoka na malengo yanayotekelezeka na ambayo yatakuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo.
“Kundi la afrika linatoa wito kwa jumuia ya kimataifa kuonyesha dhamira na utashi wa kisiasa ili katika mkutano huo wa RIO+20 tuwezwe kutoka na habari yenye matumaini kwa vizazi vijavyo .
Afrika pia inapenda kukaribisha kuanzishwa kwa mfumo ambao utasimamia na kufuatilia makubaliano yatakayofikiwa na, pamoja na utekelezaje wake kama suala la dharura” akasema Balozi Sefue.
Akitilia mkazo wa vipaumbele vya Afrika katika suala zima la maendeleo endelevu, Balozi Ombeni Sefue ambaye kwa miezi miwili mfululizo, Tanzania imekuwa Mwenyekiti wa Kundi la Nchi za Afrika.
Anasema mtizamo wa Afrika ni kutaka kuona kwamba nguzo kuu tatu muhimu kwa maendeleo endelevu zinapewa umuhimu unaolingana bila ya mmoja kupewa uzito wa kipekee.
Anasema “ Afrika inapenda kutoa wito na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa uwiano katika nguzo hizo tatu hasa nguzo ya kuondoa umaskini, bila ya kuongeza mzigo wa ziada kwa nchi zinazoendelea au kuwekwa vikwazo au kuhoji kuhusu matarajio yetu ya maendeleo”
Akaongeza Afrika ingepeda kuona pia kwamba harakati zozote za kubadili mifumo ya kiutendaji ya taasisi za Umoja wa Mataifa ikiwamo ile ya mazingira UNEP inazingatia maslahi ya Afrika.
Wakati maandalizi ya mkutano huo yakiendelea, kumejitokeza dalili za waziwazi ambapo nchi zilizoendelea zimekuwa zikilipa uzito wa aina yake nguzo ya mazingira na kutoa mkazo kidogo katika nguzo ya kuondoa umaskini na hasa ikizingatiwa kwamba nguzo ya mazingira inalenga kuwanufaisha zaidi nchi zilizoendelea kuliko nchi zinazoendelea ambazo kwao nguzo ya muhimu zaidi ni kuondokana na umaskini.
Nembo ya mkutano wa Rio+20 |
Mkutano wa RIO+20 utafanyika ikiwa ni miaka 20 kupita tangu mkutano mwingine kama huo uliobeba ajenda ya Mazingira na Maendeleo maaruku kama (Earth Summit) ulipofayika mwaka 1992 huko huko Rio de Janairo. Mkutano wa mwakani utatoa fursa ya kufanya tathmini ya makubaliano yaliyofikiwa mwaka 1992, kipi kimefanyika, wapi pameshindikana na kwa nini na hali kadhalika kutoa mwekeleo wa miaka 20 ijayo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269