Breaking News

Your Ad Spot

Dec 29, 2011

RAIS KIKWETE ATOA SALAM ZA RAMBIRAMBI KIFO CHA HALIMA MCHUKA

Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkurugenzi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Clement Mshana, kufiatia kifo cha mtangazaji maarufu wa siku nyingi wa  shirika hilo, Halima Mohammed Mchuka ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia leo, Alhamisi, Desemba 29, 2011 kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
“Nimepokea kwa huzuni habari za kifo cha Halima Mohammed Mchuka. Nakutumia wewe Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) salamu za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo hiki. Nakuomba, kupitia kwako, uniwasilishie salamu zangu kwa wafanyakazi wenzake katika TBC ambao wamempoteza mwenzao na rafiki yao.” Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam, imesema ikimkariri Rais.
“Aidha, nataka kupitia kwako niwatumie salamu zangu za rambirambi wana-familia, ndugu na jamaa wote za marehemu. Wajulishe kuwa niko nao katika wakati huu wa maombolezo na kwamba msiba wao ni msiba wangu pia. Nawaomba wawe na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi ya Mungu. Naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amen.” amesema Rais.
 Rais amesema kuwa Mchuka ametoa mchango mkubwa katika nyanja ya utangazaji nchini. “Sote tutaendelea kukumbuka weledi wake, uzalendo wake na ujasiri wake katika utangazaji uliomsukuma kuwa Mwanamke wa Kwanza katika Tanzania kutangaza mechi za mpira wa miguu”.

Amesema ni dhahiri kuwa nyanja ya utangazaji imeondokewa na mtu muhimu na namna nzuri zaidi ya kumuenzi  Mchuka ni kwa watangazaji waliobakia kuendelea kuiga mfano wake katika ubora wa utangazaji nchini mwetu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages