Na Charles Charles |
Dk. Wilbroad Peter Slaa alinukuliwa na gazeti moja la siku hiyo akidai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimetenga mamilioni ya fedha ili kuwanunua wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani waliopo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Alisema kuwa tayari CCM imefanikiwa kuwanunua viongozi wote wakuu wa Chadema wilayani Sengerema kwa shilingi 400,000 tu, lakini chama hicho kikatibua mpango wa kumnunua mbunge wake ambaye hata hivyo alishindwa kumtaja jina wala jimbo lake, kwa bei kubwa ya shilingi milioni 323!
“Nasikitika sana na mipango hii haramu, CCM siyo chama makini (na) ndiyo maana kinatumia fedha kuwanunua viongozi wa upinzani. Sisi Chadema tutaendelea kujiimarisha kwa kuwafikia wananchi”, alisema kama ilivyonukuliwa na gazeti hilo lenye uhusiano wa moja kwa moja na familia ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Nimewahi kuandika huko nyuma nikionya kuhusu tabia hii ya uongo na uzushi aliyonayo padri huyo wa zamani wa Kanisa Katoliki anayesemekana alifukuzwa, yule ambaye inawezekana alishindwa kuifanya kazi hiyo maana siku zote alilazimika kusoma Biblia Takatifu anapozungumza kanisani na siyo kutunga hadithi.
Alishindwa kwani asingeweza kuwadanganya waumini wa kanisa hilo kwa mfano kwamba madhehebu ya Kilokole yanayozidi kuenea nchini huwanunua Wakatoliki, hivyo akaamua kuvunja kwa makusudi miiko ya upadri huo kusudi atimuliwe.
Alitaka apate nafasi atakayoitumia wakati wowote na mahali popote kwa jambo lolote kuhubiri uzushi na uongo, hivyo alipokwenda Chadema na hatimaye akaukwaa Ukatibu Mkuu alionao mwaka 2004 ikawa ndoto yake imetimia.
Anadai kuwa CCM imetenga mamilioni ya fedha za kuwanunua wanachama na viongozi wa Chadema katika kanda hiyo, lakini anasema hivyo huku akijua ukweli kwamba zaidi ya nusu ya wanachama na viongozi wake walihamia huko wakitokea vyama vingine na mifano iliyo hai ipo ya kutosha.
Mathalani, yeye mwenyewe alikuwa mwanachama wa CCM hadi mwaka 1995, akajitosa kwenye kura za maoni za ndani za kuwania uteuzi wa kugombea ubunge wa jimbo la Karatu mkoani Arusha, lakini Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ilipotumia mamlaka iliyopewa na Ibara ya 107(13)(g) ya Katiba ya Chama hicho kwa kutomteua akaenda zake Chadema.
Huko alipanda ngazi moja baada ya nyingine akianza na ubunge aliogombea mwaka uleule na kushinda. Baadaye akawa Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa kabla ya mwaka 2004 kuwa Katibu Mkuu akishika nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Amaan Walid Kabourou.
Huyo naye alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti na hatimaye akajiuzulu kwa kukerwa na siasa za chama hicho za ukabila, ukanda na ukoo na kuhamia CCM.
Mbali na Dk. Slaa mwenyewe, mwingine aliyekimbilia Chadema aliposhindwa kwenye kura za maoni za ndani ya CCM za kuwania uteuzi wa kugombea ubunge ni mkewe anayedaiwa kumtelekeza mkoani Manyara, Rose Kamili, ambaye naye sasa ni Mbunge wa Viti Maalum.
Kana kwamba haitoshi, orodha hiyo ina Mbunge wa Mpanda Mjini katika mkoa wa Rukwa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Tanzania Bara), Saidi Arfi na Mbunge wa Maswa Magharibi mkoani Shinyanga, Magalle John Shibuda ambao nao walitoka CCM mwaka 2005 na 2010.
Wabunge wengine waliokimbilia Chadema na vyama walivyotoka likionyeshwa kwenye mabano ni Mbunge wa Kisesa, Meshack Opulukwa (UDP); Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylivester Kasulumbai (Chausta) na Wabunge wa Viti Maalum ambao ni Susan Kiwanga (TLP), Rachel Mashishanga na Leticia Nyerere waliokwenda huko wakitokea CCM.
Wengine ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (TLP); Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Kiboko Nyerere (CCM); Mbunge wa Bukombe, Profesa Kalikoyele Kahigi (CCM); Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini; Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa pamoja na Mbunge wa Viti Maalum, Chiku Abwao ambao walitokea NCCR – Mageuzi.
Mbali na wabunge hao angalau baadhi yao, Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema pamoja na maofisa mbalimbali ambao pia wametokea vyama vingine ni Profesa Abdallah Safari na Msafiri Mtemelwa (CUF), Profesa Mwesiga Baregu, Mabere Nyaucho Marando, Anthony Komu na Ali Chitanda (NCCR – Mageuzi), Mwita Waitara (CCM), Hemed Sabula (TLP), Erasto Tumbo na Benson Kigaila waliotoka UDP na kadhalika.
Nimetoa orodha hiyo fupi ya viongozi wa juu wa Chadema waliotoka katika vyama vingine nikianza na Dk. Slaa mwenyewe, hivyo namwomba awaambie Watanzania kuwa kila mmoja alinunuliwa shilingi ngapi ili kumng’oa katika chama alichotoka.
Atuambie yeye mwenyewe alinunuliwa na Chadema kwa bei gani, na pia atufahamishe mkewe, Rose Kamili naye alihongwa kiasi gani mwaka 2010 ili ang’olewe CCM alikokuwa Diwani wa Kata ya Basuto iliyopo Hanang’ mkoani Manyara.
Ni matusi kwa watu wanapohamia CCM kwa matakwa yao wenyewe kudai wamenunuliwa kama bidhaa, lakini kwa sababu huenda Dk. Slaa anasahau kama kuku wa kisasa, tayari hakumbuki kuwa yeye mwenyewe ni mhamiaji aliyekwenda Chadema kutokana na uchu wa kutaka awe mbunge kama alivyofanya pia mkewe na wabunge takribani wote waliobaki.
Kama nilivyobainisha mapema katika makala hii, Dk. Slaa amebobea kwa uzushi na uongo. Ndiyo maana alishindwa kumtaja jina mbunge aliyedai kuwa CCM ilijaribu kumnunua kwa shilingi milioni 323 ili aondoke Chadema na kuhamia chama hicho kilichopo madarakani.
Natambua kuwa uongo wake huo utatetewa kwa nguvu nyingi na baadhi ya wapambe wake wakiwemo waliopo radhi na tayari hata kukesha wakipambana kwa ajili hiyo, wale ambao utadhani wamekula yamini kwamba wasipofanya hivyo wanakwenda kaburini!
Hawawezi kukubali kuwa wanachama na viongozi wanaoondoka Chadema wanafanya hivyo kutokana na kukerwa na uongozi wa juu wa chama hicho kwa mapungufu yake mengi.
Badala ya kufanya siasa kistaarabu au kwa haki kwa mfano, viongozi hao akiwemo Dk. Slaa siku zote wamekuwa wakihamasisha fujo na vurugu kila mahali, jambo ambalo kwa wakazi wa jiji la Arusha wana uzoefu nalo wa ghasia zilizoanza tokea Januari 5, 2011 na kurejewa mara nyingi.
Viongozi wanaofanya uchochezi wa aina zote ukiwemo uvunjifu wa amani wakidai hakuna kulala mpaka kieleweke, lakini wanafanya hayo yote kwa hasira baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2010.
Walifanya kosa la kiufundi kuwadanganya wanachama na kikundi kidogo cha wafuasi wao kuwa Dk. Slaa angekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uongo uliokwenda sambamba na ahadi ‘hewa’ eti kwamba hata katiba ya nchi ingeandikwa upya ndani ya siku 100.
Wakaahidi kushusha bei ya saruji kutoka shilingi 11,500 za wakati huo hadi shilingi 5,000 tu, jambo ambalo hata kwa akili za kitoto kamwe lisingewezekana kwani hata gharama za kutengenezwa kwake kiwandani zilikuwa shilingi 8,000 kwa mfuko.
Pamoja na uongo huo wote, wapiga kura waliodhaniwa hawana akili timamu walikataa katakata kudanganywa kama watoto wa chekechea wala kufanywa kuwa wendawazimu, hivyo wakaipa CCM ushindi wakianzia kwa mgombea wake wa urais, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete hadi kwa wanachama wake waliogombea ubunge na udiwani.
Ushindi huo wa kishindo ndio uliwaachia kiwewe viongozi hao wa Chadema na kufanya jaribio lao la kwanza la vurugu hapo Novemba 18, 2010 walipotoka nje ya bunge wakidai Rais Kikwete eti hakushinda, badala yake alizawadiwa nafasi hiyo na Tume ya Uchaguzi ya Taifa kwa kumpora haki hiyo Dk. Slaa.
Lakini kwa vile hakuna uongo usiogundulika baadaye, Chadema walewale wakiongozwa na Mbowe yuleyule aliyewatoa mkuku kutoka bungeni siku hiyo ndio walewale waliokuja tena mwaka jana, kutangaza kwa vinywa vyao wenyewe kumtambua Rais Kikwete kuwa ndiye alishinda kihalali mwaka 2010 na siyo Dk. Slaa kama walivyodai mwanzo.
Wakaenda hadi Ikulu kumbembeleza atumie mamlaka aliyopewa na wananchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutengua maamuzi halali ya bunge baada ya kurudia tena uhuni wa kutoka nje ya ukumbi wakati wa kujadili Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2011.
Juhudi zao zilipogonga mwamba huku Watanzania wengi wakionyesha kutowaunga mkono ndiko kumewafanya watunge uongo mpya kuwa CCM imetenga mamilioni ya fedha, yale ambayo kazi yake kubwa ni kuwanunua wanachama na viongozi wa Chadema wa Kanda ya Ziwa.
Ni jambo lisiloweza kuingia akilini hata kwa mwendawazimu anayepata angalau nafuu ya vipindi kukubaliana na madai kwamba eti CCM ilijaribu kumnunua mbunge mmoja tu wa Chadema kwa shilingi milioni 323 ili akihame chama hicho.
Ndiyo maana nasema hakuna mwenye akili timamu anayeweza kukubaliana na uongo huo kwani hata kwa masikini biashara hiyo haina faida yoyote kisiasa na wala vinginevyo.
Haiwezekani fedha hizo zote zitumike kumnunua mtu hata kama ingekuwa wabunge wote wa Chadema ili wahamie CCM, vinginevyo ni ujinga wa kufikiri kudhani kuwa watu wote unaweza kuwadanganya kama watoto wa chekechea.
Kama Dk. Slaa mwenyewe na mkewe Rose, wabunge, viongozi, maofisa au wanachama mbalimbali wakiwemo niliowatolea mfano walivihama vyama vyao vya zamani na kwenda Chadema kwa kununuliwa kama bidhaa basi atuambie bei gani, lakini CCM kamwe haina wendawazimu huo!
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0719 822 344 na 0782 133 996
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269