Breaking News

Your Ad Spot

Jan 25, 2012

JK AENDA USWIS KUHUDHURIA MKUTANO WA ' WEF'

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete yuko  Davos, Uswisi, kuhudhuria mkutano wa mwaka huu wa Umoja wa Uchumi Duniani-World Economic Forum (WEF) unaoanza leo, Jumatano, Januari 25. Rais Kikwete na ujumbe wake waliondoka nchini jana jioni.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu mjini Dar es Salaam, imesema katika siku nne za mkutano huo, mbali na kuhudhuria mkutano wenyewe ambao hukusanya viongozi wakuu wa siasa, biashara, uchumi na jamii duniani, Rais Kikwete atakutana na mlolongo wa watu mbalimbali kujadili jinsi gani wanavyoweza kushiriki kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.

Shughuli ya kwanza ya Mheshimiwa Rais Kikwete mara baada ya kuwasili Davos ni kukutana na Bwana Robert Hormats, Naibu Waziri wa Uchumi, Nishati na Kilimo wa Marekani, ili kujadili ajenda ya Afrika itakayowasilishwa kwenye mkutano wa mwaka huu wa nchi tajiri zaidi duniani za G-8 utaoandaliwa na Marekani. Pia viongozi hao wawili watajadili uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Marekani.

Baadaye jioni atahudhuria halfa ya faragha ya ufunguzi wa mkutano wa WEF mwaka huu itakayoandaliwa na Mwanzilishi wa mikutano hiyo ya WEF, Profesa Klaus Schwab, na Alhamisi Rais Kikwete mbali na kushiriki shughuli za mkutano atakutana miongoni na viongozi wengine na Rais wa Benki ya Dunia, Bwana Robert Zoellick; Mwenyekiti wa Bill and Bellinda Foundation, Bwana Bill Gates na Waziri Mkuu wa Kenya, Bwana Raila Odinga.

 Mchana wa siku hiyo, Rais Kikwete atakuwa miongoni mwa wazungumzaji wakuu katika vikao viwili.  Katika kikao cha kuzungumzia jinsi ya kuongeza kasi ya uwekezaji katika kilimo barani Afrika, Grow Africa Partnership: Accelerating Investment in Africa Agriculture, Rais Kikwete anatarajiwa kuelezea maendeleo ya Mpango Kabambe wa Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania wa SAGCOT na baadaye atazungumza katika kikao kitakachojali hali ya baadaye ya Afrika – Shared Opportunities for Africa’s Future.

 Aidha, siku ya Ijumaa, Rais Kikwete atakuwa miongoni mwa wazungumzaji wakuu kwenye kikao cha kujadili visheni mpya ya kilimo ya Afrika – Realising a New Vision for Agriculture: An Action Agenda na baadaye atakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Bwana Kevin Ruud na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID) Bwana Raj Shah. Pia Rais Kikwete atakutana na Bwana Paul Walsh, mwekezaji katika Kampuni ya Bia ya Serengeti.

Kwenye siku ya nne na ya mwisho, miongoni mwa mambo mengine, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Yingluck Shinawatra, Waziri Mkuu wa Thailand kabla ya kundoka Davos kwenda Addis Ababa, Ethiopia ambako atahudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU).



No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages