Breaking News

Your Ad Spot

Jan 24, 2012

RAIS KIKWETE AKUTANA NA MKURUGENZI SUB SAHARAN DIVISION, WIZARA YA MAMBO YA NJE CUBA

Rais Kikwete akizungumza na Alberto.Kushoto ni 
Balozi wa Cuba  Gomez Diaz.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Januari 24, 2012, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masula ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Cuba, Bwana Alberto Velazco San Jose.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete na Bwana San Jose wamezungumzia masuala yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Cuba, masuala ya kanda ya Afrika na masuala mbalimbali ya kimataifa likiwamo lile la vikwazo ambazo Marekani iliiwekea Cuba tokea miaka ya 1960 na inaviendeleza.

“Uhusiano mzuri, wa karibu na wa miaka mingi ni kielelezo halisi cha jinsi nchi mbili ndogo na zinazoendelea zinavyoweza kushirikiana na kusaidiana kama ndugu,” Rais Kikwete amesema katika mazungumzo hayo na kuongeza, “Nipende pia kuishukuru Cuba na wananchi wa Cuba kwa kuunga mkono jitihada za maendeleo za nchi yetu miaka yote hii pamoja na kwamba mmeendelea kupambana na vikwazo vikubwa vya kila aina.”

Kwa miaka mingi, Tanzania na Cuba zimekuwa zinashirikiana katika masuala mengi na kusaidiana katika masuala ya kimataifa, na Cuba imeunga mkono jitihada za maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwamo za afya, elimu na michezo.

 Bwana Alberto Valazco San Jose amemjulisha Rais Kikwete kuhusu mageuzi ya kiuchumi ambayo nchi hiyo inayafanya kwa kufungua uchumi wake kutoka uchumi wa dola na kuuelekeza kwenye uchumi wa soko ambako watu binafsi wanapata nafasi kushiriki katika uchumi wa nchi yao.

“Tunafanya mageuzi makubwa katika uchumi wetu kwa kuutoa kwenye uchumi wa dola na kuruhusu sekta binafsi kushiriki kwenye ujenzi wa uchumi huo. Tunafanya mageuzi lakini hatuna haraka kwa sababu hatutaki kufanya makosa katika jambo hili,” amesema Mkurugenzi huyo.

Naye Rais Kikwete ametumia nafasi hiyo kumjulisha Mkurugenzi huyo kuhusu jitihada za Serikali yake katika kujenga mazingira ya kuwaletea maisha bora Watanzania kwa kumweleza jitihada za Serikali kupambana na ugonjwa wa malaria, kuongeza uzalishaji wa sukari, kuongeza uzalishaji wa umeme, kupanua na kuboresha elimu na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

 Cuba ni moja ya mataifa yanayoongoza duniani kwa uzalishaji wa sukari, na imekuwa inajenga kiwanda cha dawa ya kuua mbu katika jitihada zake za kuisaidia Tanzania kukabiliana na ugonjwa wa malaria.

 Rais Kikwete pia amemweleza mgeni huyo kuhusu jitihada za Serikali yake katika kuboresha miundombinu nchini kwa kuboresha usafiri wa reli, kukabiliana na matatizo katika usafiri wa anga, upanuzi na uboreshaji wa bandari za Tanzania na uendelezaji wa ujenzi wa barabara za lami nchini.

 Bwana Alberto Valelazco San Jose yuko katika ziara za nchi za Afrika akiwa njiani kwenda Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) utakaofanyika Januari 29-30 mwaka huu.

Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Kundi la Makampuni ya Frontline Development Partners ya Dubai inayotaka kuwekeza katika masuala ya maji, kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari, usafirishaji wa reli na uzalishaji wa umeme. 

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages