Breaking News

Your Ad Spot

Jan 4, 2012

CUF YAJIVUA GAMBA, YAMFUKUZA HAMAD RASHID, DOYO NA WENGINE KADHAA

Wajumbe wanne wa Baraza Kuu la chama cha CUF akiwemo Mbunge wa Wawi Hamad Rashid (pichani) wamefukuzwa uanachama wa chama hicho.

Akitangaza uamuzi huo leo Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara) kijana Julius Mtatiro amesema viongozi hao wamefukuzwa na Baraza Kuu la CUF baada ya kubainika kwamba wamepoteza sifa za uongozi wa kutaka kukisaliti chama na kusababisha migogoro ndani yake.

Amesema Baraza kuu la CUF limewafukuza viongozi hao baada ya kupata baraka kutoka kwa kikao cha baraza hilo na kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa bara na theluthi mbili kutoka katika wajumbe wa baraza kuu kutoka Zanzibar.

Kwa mujibu wa Ntatiro kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe 56 ambao kati yao 47 ndio walipiga kura.

Mtatiro aliwataja wengine waliofukuzwa kuwa ni, mjumbe wa baraza kuu la CUF Doyo Hassan Doyo kutoka katika mkoa wa Tanga, Juma Sanani ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, na Shoka Khamis Juma ambayewahi kuwa mbunge wa Micheweni kwa tiketi ya CUF kipindi kilichopita huku Yasin Mrotwa akipewa onyo kali  kwa ajili ya chunguzwa.

Hatma ya wajumbe wengine itajulikana baadaye baada ya kujadiliwa na vikao mbali mbali vya  chama cha CUF kwa sababu wengine ni wanachama wa kawaida na sio wajumbe wa baraza kuu ambacho ni chombo cha juu chenye maamuzi.

 Akizungumzia hatua hiyo, Hamad Rashid amepinga uamuzi wa kufukuzwa katika chama cha CUF na kumuita  Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ni dikteta mkubwa na kiongozi asiyeheshimu maamuzi ya mahakama.

Kwa mujibu wa Hamadi Rashid, uamuzi huo umekuja wakati Hamad na wenzake wakiwa tayari wameweka  pingamizi kutoka mahakama kuu kupinga maamuzi ya mkutano wa Baraza Kuu na hati ya mahakama ipo mikononi wa  CUF.

Hamad alisema watakwenda tena mahakamani Februari 14 kusikiliza pingamizi la kikao hicho, ambapo hata hivyo alipoulizwa Mtatiro kuhusu hati ya mahakama kama wanayo alikataa na kusema hawakubaliani nayo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages