Breaking News

Your Ad Spot

Jan 4, 2012

RAIS KIKWETE AONGOZA MAMIA KUMZIKA BALOZI MHINA

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Januari 4, 2012, ameungana na mamia ya wananchi kumzika aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuia ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Athuman Mhina katika mazishi yaliyofanyika kijijini kwao, Mnyuzi, Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga.
Rais Kikwete amewasili kijijini Mnyuzi kiasi cha saa sita mchana kujiunga na mamia ya waombolezaji akiwamo Rais Mstaafu William Benjamin Mkapa, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara) Mzee Pius Msekwa na Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye tayari kwa mazishi ya Ndugu Mhina ambaye alifariki dunia saa tatu usiku wa kuamkia jana, Jumanne, Januari 3, 2012 nyumbani kwake Madale, Dar Es Salaam, kwa matatizo ya ugonjwa wa moyo.
Viongozi wengine ambao wamehudhuria mazishi hayo ni pamoja na wenyeviti wa CCM wa mikoa, wabunge na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kupitia Jumuia ya Wazazi, wawakilishi kutoka mikoa 11 ya Tanzania Bara na Visiwani, viongozi wa Jumuia hiyo, mawaziri, wabunge, wakuu wa wilaya na viongozi wengine wa CCM kutoka mikoa ya jirani na Tanga.
Baada ya kumalizika kwa taratibu za dini na Chama cha Mapinduzi, safari ya mwisho ya Ndugu Mhina ilianza na mwili wa marehemu uliteremshwa kaburini, pembeni kwa nyumba yake, kiasi cha saa saba na dakika 17 mchana.
Wakati anafariki dunia, Ndugu Mhina alikuwa na umri wa miaka 72 na mbali ya kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuia ya Wazazi pia alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.
Ndugu Athuman Mhina ambaye alizaliwa mwaka 1940 na kupata shahada ya kwanza ya ualimu mwaka 1974 kabla ya kupata shahada ya uzamili katika fani hiyo hiyo kutoka Uingereza mwaka 1991 alishikilia nafasi nyingi za uongozi katika maisha yake.
Kati ya mwaka 1971 na 1973 alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na kati ya mwaka 1975 na 1980 alikuwa Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wazazi Taifa. Kwa miaka 10 kuanzia 1977 hadi 1987 alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, na kati ya mwaka 1980 na 1980, alikuwa Mbunge wa Korogwe kabla ya kuteuliwa kuwa Mwambata wa Elimu katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza kati ya 1985 na 1991.
 Mheshimiwa Rais Kikwete amerejea Dar es Salaam baada ya mazishi hayo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages