Na Mwandishi Maalum, New York
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amesema Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete imekuwa mstari wa mbele katika kusukuma mbele ajenda za Umoja wa Mataifa zikiwamo za Maendeleo na Ulinzi wa Amani.
Na kwa sababu hiyo, Mkuu huyo wa UM, anasema anaridhishwa na kufurahishwa sana na uhusiano wa karibu ulipo baina ya Tanzania na Umoja wa Mataifa.
Ameyaeleza hayo siku ya jumanne wiki hii, wakati alipokuwa akiagana na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ombeni Sefue aliyekwenda kumuaga rasmi baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Katika mazungumzo hayo, Ban Ki Moon, alishindwa kujizuia kuelezea hisia zake na mapenzi makubwa aliyonayo kwa Rais Jakaya Kikwete na Watanzania kwa ujumla.
“ Ninahisia za pekee kuhusu Tanzania, uhusiano wangu na Rais Kikwete ni wa aina yake, ninasikitika kwamba imekulazimu uondoke baada ya kukaa hapa kwa muda mfupi, lakini napenda niliweke hili wazi, kwamba ninafurahishwa sana na mchango wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa” akasema Ban Ki Moon
Na kuongeza, ninajua unakwenda kushika wadhifa mkubwa sana wa kumsaidia Rais Jakaya Kikwete, ambeye amejijenga heshima kubwa Barani Afrika na katika Jumuia ya Kimataifa. Nimekuwa nikiwasiliana naye mara kwa mara, amenisaidia sana katika masuala mengi likiwamo hili la mpango wa kimataifa kuhusu Afya ya Mama na Mtoto”.
Akasema ni matumaini yake kwamba, Balozi Sefue katika wadhifa wake mpya bado ataendelea kufuatilia kwa karibu masuala ya Umoja wa Mataifa kwa namna moja ama nyingine, na kwamba asisite wakati wowote kuwasiliana naye, ama kwa niaba ya Rais au katika nafasi yake ya Ukatibu Mkuu kiongozi. Na kwamba kwa upande wake bado ataendelea kuitegema Tanzania.
“ Katika muda mfupi uliokaa hapa, umepata fursa ya kufahamu mambo mengi ambayo nina hakika utayafuatilia na pengine utaendelea kutusaidia katika wadhifa wako mpya. Nipigie simu wakati wowote iwe kwa niaba ya Rais Kikwete au wewe mwenyewe nitafurahi sana kuwasiliana nawe” akasisitiza Ban Ki Moon.
Pamoja na kuelezea kuridhishwa kwake na mchango wa Rais Jakaya Kikwete na Tanzania kwa ujumla katika masuala ya Umoja wa Mataifa. Ban Ki Moon alitumia pia fursa hiyo kumshukuru Msaidizi wake wa karibu, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Asha-Rose Migiro.
Ban Ki Moon amemuelezea Asha- Rozi Migiro kama kiongozi mchapakazi sana na ambaye amekuwa msaada mkubwa wake, na anasikitika kwamba anaondoka .
Akadokeza pia kwamba amekwisha kufanya majadiliano ya karibu sana na ya kina na Naibu Katibu Mkuu wake kuhusu nani atakaye jaza nafasi yake na kwamba safari hii hatatoka Afrika.
Kwa upande wake, Balozi Ombeni Sefue ameshukuru Katibu Mkuu kwa ushirikiano mkubwa aliompatia wakati akiwa hapa Umoja wa Mataifa, na kwamba ingawa anaondoka lakini ataendelea kufuatilia masuala ya Umoja wa Mataifa, na kuangalia namna gani Tanzania itakavyoendelea kuchangia.
Akaongeza kuwa baadhi ya changamoto atakazofuatilia kwa karibu ni matatizo ya ajira kwa vijana na kuongezeka kwa pengo kati ya walionacho na wasionacho na kwamba masuala hayo mawili yasipotafutiwa ufumbuzi yataendelea kusababisha uvunjifu wa amani kwa kuwa ni masuala yanayozigusa nchi zote duniani.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269