Breaking News

Your Ad Spot

Feb 28, 2012

HOJA MTAMBUKA

Na Charles Charles
 CHADEMA KUTUMIA RED BRIGADE ARUMERU???
Kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha, zinaanza Machi 9, mwaka huu, lakini uchaguzi wake umepangwa kufanyika Aprili Mosi.

Tayari Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kwamba kinaweza kutumia kikundi kinachoitwa Red Brigade katika jimbo hilo ili kutembeza kipigo, jambo ambalo limeelezwa kwa kisingizio cha kumjibu Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye.

Akiandika makala yake kwenye gazeti moja litolewalo kila siku nchini Jumatano, wiki jana, Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba alimuonya Nape kuwa Arumeru Mashariki siyo Igunga, kisha akafichua hatari inayoweza kutokea huko.

Nataka pia kuutolea majibu utapeli uliokusanya hadithi nyingi zilizosheneza uzushi, uongo, uchochezi na ulimbukeni wa madaraka ya kisiasa unaotengenezwa maalum ili Chadema ikishindwa huko Arumeru Mashariki watu wawe wamejengewa mazingira ya kutokubali kupokea matokeo hayo!

Inaletwa hadithi kuwa Nape anataka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Peter Slaa akagombee ubunge katika jimbo hilo, uongo ambao asiyekuwa mwathirika wa siasa za vurugu hawezi kuuandika mpaka gazetini.

Mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo hilo mwaka 2010, Joshua Nasari alitangaza kwamba kuna watu wanataka Dk. Slaa agombee nafasi hiyo mwaka huu, jambo ambalo pia lilibarikiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, Freeman Mbowe akisema hawana pingamizi lolote kama yeye mwenyewe angeridhia.

Kauli hizo ndizo zikazungumziwa na Nape kuwa CCM iko tayari kupambana naye huko, na kwamba huo utakuwa mwisho wa ndoto zake kuwania tena urais mwaka 2015.

Hata hivyo, Nape kamwe hakuzungumzia suala hilo kwa kuita waandishi wa habari ila kwa kuulizwa, tena ilikuwa na gazeti linalomilikiwa na familia ya Mbowe ambaye ndiye bosi wa juu kuliko wote kwa Chadema. Hivyo, inashangaza kwa Mwigamba kutaka kueneza uongo wa makusudi kwa watu.

Kama kuna tatizo kuhusu Dk. Slaa kutaka akagombee ubunge katika jimbo hilo hapo wanasiasa wambeya ni Nasari na bosi wake Mbowe. Hao ndio watu ambao Mwigamba anapaswa kuwashushua na siyo kudandia mgongo wa Nape kama mlevi wa gongo.

Anadai eti CCM mwaka huu “itagaragazwa” huko Arumeru Mashariki, ndoto iliyoota usugu kwa viongozi kama yeye na siyo ngeni miongoni mwa Watanzania.

Ilihubiriwa kila mahali ulipotokea uchaguzi mdogo wa Igunga, Tabora. Mmoja wa viongozi wa Chadema aliyekuwa akitangaza hadi anataka kulazimisha watu waamini hivyo alikuwa Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Taifa wa Chama hicho, Mwita Mwikwabe Waitara.

Mwingine alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi (wakati huo), Erasto Tumbo, wale ambao pia walianza kampeni hata kabla ya tarehe rasmi iliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa wakisingizia eti wanafungua mashina ya chama chao.

Mwigamba na kalamu yake hakuandika chochote kuhusu ukiukaji huo wa sheria na kanuni, hivyo Watanzania hawashangai kumuona leo naye akitangaza utabiri wa mizimu kama vile mganga wa mitishamba kwa kusema CCM itashindwa vibaya huko Arumeru Mashariki.

Anafikiri kila Mtanzania ni mjinga kiasi kiasi kwamba anaweza kudanganywa kwa urahisi kama mtoto wa chekechea. Anadhani kuwa kura zinapigwa kwa makala za uzushi na uongo magazetini!

 Anadai kuwa Dk. Slaa alipoteuliwa kugombea urais mwaka 2010 ilibidi apelekwe kwanza Karatu ili wananchi wa jimbo hilo wakaulizwe endapo walikuwa radhi au hawataki, kisha akapelekwa kwenye Viwanja vya NMC mjini Arusha, pale ambako watu kutoka wilaya zote za mkoa huo walikusanyika na wao wakaulizwa kama wanaridhia na wao pia wakaruhusu.

Anadhani hatuelewi ilivyokuwa kazi ngumu kumshawishi agombee nafasi hiyo akisema asingeweza kumshinda mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete hata kama angekesha anachezeshwa maruhani ya kwao.

Ili aweze kukubali baada ya mvutano mkali ofisini, Chadema ililazimika kumlipa mshahara mkubwa kupindukia na usiokatwa kodi, posho za kufuru na pensheni inayokaribia shilingi milioni 100 mwaka 2015.

Lakini akihofia kupewa ahadi hewa na chama hicho chenye misingi ya ukabila, ukanda, ukoo na ufamilia, kasisi huyo wa zamani aliyeshindwa kuumudu utakatifu kanisani naye alishinikiza waandikishiane mkataba wa kisheria ili baadaye asije “akarukwa”.

Huo ndio uongo wa Mwigamba kutaka kuwadanganya Watanzania eti kuwa wana Arusha wamemtoa Dk. Slaa kwa ngazi ya kitaifa, lakini hata alipokuwa Mbunge wa Karatu alikuwa pia ni Katibu Mkuu wa Chadema.

Inawezekana Mwigamba hajui kama Katibu wa Wilaya ni wa ngazi ya wilaya yote, halafu yule wa mkoa naye eneo lake ni mkoa na Katibu Mkuu anakuwa wa nchi nzima na siyo wa wa mkoa wala jimbo moja. Ndiyo maana Dk. Slaa kamwe hajaanza miaka miwili iliyopita kuwa wa kitaifa ila tangu mwaka 2004.

Kuhusu “mtiti” wa Chadema uliokuwepo Igunga hapo mwaka jana kama ilivyobainishwa na Mwigamba hata miye nakubali.

Ulikuwa “mtiti” wa kumwagia tindikali watu na kuwatia vilema vya maisha kutokana na siasa tu za kishamba, na pia ulikuwa “mtiti” wa kujaribu kuwateka wabunge wa CCM baada ya kuona hali inazidi kuwa ngumu kupindukia.

Ulikuwa “mtiti” wa kuhubiri uzushi, uongo na uchochezi wenye kila aina ya majungu, wivu, chuki na hasira za kuhofia kushindwa licha ya kwenda katika jimbo hilo kwa mbwembwe na vitisho kama “chinjachinja”.

Kama anavyosema tena Mwigamba kuwa “mtiti” wa Igunga ulikuwa kama “trela” ila wa Arumeru Mashariki utakuwa ni “kiboko”, hapa pia nakubali kwa asilimia 100.

Nazingatia hulka za viongozi wa Chadema ambao siku zote kazi yao ni kuchonganisha watu ili wafarakane, wanuniane, wavurugane, wapigane, waumizane, wachomeane mali zao kama ilivyokuwa Arusha Januari 5, mwaka jana na ikiwezekana, wengine wapoteze mpaka maisha yao kwa kutolewa “sadaka” au kafara kwa ibada za kishetani.

Ametumia nafasi yake kama Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha kutangaza kuwa “mtiti” wa Arumeru Mashariki utakuwa mkubwa kuliko wa Igunga, lakini hizo ni juhudi

za kuwatisha watu ili wasifuatilie kampeni za uchaguzi huo mdogo pindi zikianza na hivyo washindwe kutenganisha mchele na pumba.

Anataka Nape aulize “mtiti” wa Chadema katika mkoa wa Arusha kwa aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM wa jimbo la Arusha Mjini mwaka 2010, Dk. Batlida Burian au Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck ole Medeye kusudi wamwambie ukoje.

Viongozi wa CCM kama Nape kamwe hawafanyi siasa za “mititi” anazohubiri Mwigamba, hivyo hata kumjibu kamwe hawezi kupoteza muda wake maana yupo “bize” anashughulikia itikadi na kueneza chama chake kistaarabu na siyo kwa “mtiti”.

 Anataka pia Nape amuulize Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Luteni Yussuf Makamba kuhusu “mtiti” wa Chadema ulivyokuwa katika uchaguzi mdogo wa Tarime mwaka 2009, kisha atakachoelezwa akizidishe mara moja na nusu ili kujua “mtiti” gani utakuwepo huko Arumeru Mashariki.

Kama Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Mwigamba ameonyesha kuwa chama chake hakiendi Arumeru Mashariki kushindanisha sera, ilani za uchaguzi wala vinginevyo, badala yake kinakwenda kwa “mtiti” wa vurugu au vita vya silaha na umwagaji wa damu.

 Anafahamu kuwa chama chake hakiwezi kushinda kama ilivyokuwa pia mwaka 2010 wakati mgombea wake wa kiti cha ubunge katika jimbo hilo, Joshua Nasari alipotupiliwa mbali na Jeremiah Sumari wa CCM, yule ambaye sasa ni marehemu na Mungu amrehemu!

Anatangaza vita mapema kwamba wana “jeshi” linalokwenda Arumeru Mashariki kufanya “mtiti” mkubwa zaidi kuliko wa Tarime na Igunga.

Anasema watatumia “kikosi” cha Red Brigade ambacho “askari” wake watano watakuwa “wanamshughulikia” mwana CCM mmoja, kazi ambayo ni kumpa mkong’oto ili kutafuta ushindi kwa kuwatisha watu.

Hayo ndiyo maandalizi ya kigaidi yanayofanywa na viongozi wa Chadema, yale ambayo yanaweza kusababisha kuzuka kwa mauaji ya kikatili kwa kisingizio cha kuwadhibiti vijana wa CCM wasinyanyase wananchi wa Arumeru Mashariki!

Yanaweza kuwa ni mauaji mabaya zaidi baada ya mwaka jana kule Igunga, mwana CCM mmoja kumwagiwa tindikali usoni na kupelekwa hadi India ili kufanyiwa upasuaji.

Akitengeneza mazingira mengine ya siasa za kitapeli na kijinga, Mwigamba anadai kwamba anajua CCM itakwenda Arumeru Mashariki kumtumia Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Lyatonga Mrema ili kuisaidia ishinde.

Anasema katika uchaguzi mdogo wa Igunga, mwaka jana, na Uzini uliofanyika wiki mbili zilizopita, CCM ilimtumia Naibu Katibu Mkuu wa chama cha Civic United Front (Tanzania Bara), Julius Mtatiro na mwenzake wa Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu.

Kama Tanzania imewahi kuwa na Wenyeviti wa Mikoa wa vyama vya siasa wazushi kupita kiwango basi Chadema inaongoza katika sifa hiyo ya ovyo kupindukia.

Sifahamu kama Mwigamba alitaka CUF isishiriki chaguzi hizo ndogo ila Chadema peke yake, na pia sijui endapo anadhani kuwa vyama vingine vya upinzani nchini havipaswi kugombea nafasi yoyote ile ya uwakilishi wa umma katika vyombo vya dola kama Bunge, Baraza la Wawakilishi Zanzibar au nafasi za udiwani.

Ni ujinga kwa mtu kusema kuwa Mtatiro na Jussa walikwenda kuisaidia CCM ili ishinde huko Igunga na Uzini wakati CUF ilikuwa na wagombea wake yenyewe.

Kama viongozi wa CUF hawakupaswa kwenda kuwanadi wagombea wa chama chao katika jambo hayo yote, ukuwadi huo pia ulifanywa na viongozi wa Chadema akiwemo Mbowe na Dk. Slaa maana pia walikuwa Igunga na Uzini wakifanya kampeni.

Mbona hasemi kwamba nao walikwenda huko kuisaidia CCM ili ishinde dhidi ya wagombea waliosimamishwa na CUF kama siyo wendawazimu wa kufikiri?

Inawezekana Mwigamba amevamia siasa ukubwani huku akidhani kuwa ni ugomvi, na pia huenda akawa limbukeni wa madaraka aliyonayo akiwa Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa.

Ni ujinga kusema viongozi wa CUF wanapokwenda kuwanadi wagombea ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar au nafasi za udiwani wanatumiwa na CCM, lakini wanachofanya ni kilekile kinachofanywa na viongozi wa Chadema wakati uleule na sehemu ileile!

Akihutubia taifa kwa njia ya redio Januari, 1979 kuhusu Vita vya Kagera, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (wakati huo), Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alimshangaa aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Kanali Muammar al Qadaffi.

Mwalimu alisema wakati vikosi vya Tanzania vinapambana na majeshi ya serikali ya aliyekuwa Kiongozi wa Kijeshi wa Uganda, Field Marshal Idi Amina katika ardhi ya nchi hii, Qadaffi alikuwa akifahamu kila jambo, lakini hakusema lolote wala kufanya chochote.

Lakini pale majeshi ya Amin yalipopigwa na vita hivyo kuingia katika ardhi ya Uganda, Qadaffi alimtuma balozi wake hapa nchini, kumuomba Mwalimu aviondoe vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ndani ya nchi hiyo ambayo sasa inaongozwa na Luteni Jenerali Yoweri Kaguta Museveni.

Pamoja na kuwasilisha ombi hilo, Qadaffi alikwenda mbali zaidi akimtishia Mwalimu kuwa kama angekataa kuviondoa vikosi vyake katika ardhi ya Uganda, nchi yake nayo ingeingiza jeshi lake kwenda kuyasaidia majeshi ya Amin.

“Nilimwambia balozi yule akamwambie Qadaffi kwamba vita vinavyopiganwa sasa katika ardhi ya Uganda ndiyo vilevile vilivyokuwa vinapiganwa katika ardhi ya Tanzania”, alisema Mwalimu na kuongeza:

“Kama vita vile vilikuwa halali wakati vinapiganwa katika ardhi ya Tanzania haviwezi kugeuka na kuwa haramu wakati vinapiganwa katika ardhi ya Uganda. Ni vita vilevile”.

Nimetumia mfano huo kuonyesha ujinga wa kufikiri walionao baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema, wale wanaodhani kuwa ni halali chama chao kushiriki chaguzi za uwakilishi wa wananchi katika vyombo vya dola, lakini ni haramu kwa CUF na TLP kufanya hivyo wakati pia vimesajiliwa kwa sheria ileile ya vyama vya siasa nchini, katiba ileile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kanuni zilezile zilizopo.

 Kuhusu madai kwamba Nape na wajumbe wenzake wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM iliyoteuliwa Aprili 11, mwaka jana, walipita katika mikoa yote ya Tanzania isipokuwa Arusha pekee pia ni uzushi, uongo na uzandiki uliopitiliza mpaka miguuni.

 Ni ujinga wa aina yake kiongozi wa kisiasa kutaka kudanganya hata kwa jambo linalohitaji kuliona kwa macho, lakini anataka kuwafanya watu wote ni vipofu “tititi” isipokuwa yeye peke yake.

Nape na wajumbe wenzake wa Sekretarieti ya Taifa ya CCM hawakwenda mikoa yote 26 ya Tanzania kama anavyodai Mwigamba ila walifanya hivyo kwa mikoa mitatu tu.

Walianzia Dodoma kwa kutambulishwa kwenye Uwanja wa Nyerere Square uliopo mjini humo, kisha wakaenda Dar es Salaam walikotambulishwa kwenye Viwanja vya Bakhresa, Manzese wilayani Kinondoni.

Hata hivyo, safari ya kuelekea Dar es Salaam iliwapitisha pia Morogoro na kisha Chalinze katika mkoa wa Pwani, kule ambako walikuta maelfu ya wananchi wakiwasubiri ili angalau wawasalimie peke yake, ukweli ambao Mwigamba angependa aupotoshe kwa nguvu zake zote. 
 
Mbali na Dodoma na Dar es Salaam, ziara hiyo ya kutambulishwa pia ilifanyika katika mkoa wa Mjini Magharibi huko Zanzibar na huo ndio ukawa mwisho wa zoezi hilo.

Walitambulishwa katika mikoa hiyo mitatu kwa sababu tatu peke yake. Kwanza walianzia Dodoma kwa vile ndipo yalipo Makao Makuu ya CCM, pili wakaenda jijini Dar es Salaam ambako kuna Ofisi Ndogo ya Makao Makuu pale Lumumba na tatu, ziara yao iliishia mkoa wa Mjini Magharibi kwa sababu hapo ndipo ilipo Afisa Kuu ya Chama hicho kwa Zanzibar.

Ilikuwa ni lazima wakaonyeshwe ofisi zao kila baada ya kupewa mapokezi ya halaiki kutoka kwa wananchi na kuwahutubia angalau kwa dakika chache tu.

Katika hali hiyo, hakuna ziara hata moja ya pamoja waliyofanya katika mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Kagera, Kigoma, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Mtwara, Morogoro,  Iringa, Lindi, Pwani, Tanga, Kaskazini Pemba, Kusini Pemba, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja au Kilimanjaro.

Viongozi wa CCM hawarundikani kwenye ziara moja kiasi cha kufunga hadi ofisi kama wa Chadema, jambo ambalo Mwigamba akiwa Mwenyekiti wa Mkoa analifahamu.

Anajua kuwa ziara za Chadema huwakusanya pamoja Mwenyekiti wa Taifa, Makamu Wenyeviti wake wote, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu wote, Wakurugenzi wa Taifa wa Idara zote za Makao Makuu, wabunge wote wa kuchaguliwa kwenye majimbo, wabunge wote wa Viti Maalum na watendaji wote waandamizi wa taifa na kila mkoa wanaokwenda.

Wanalazimika kufanya hivyo kwa sababu akienda mmoja peke yake hawezi kupata watu mkutanoni na maandamano yake yanaweza kuwa ya vibaka tu.

Inabidi wafuatane kwa sababu kuna watu hujitokeza kuandamana au kwenda mkutanoni ili pengine kuiona sura ya “Ze Komedi” kama Dk. Slaa, Mwenyekiti wa Taifa “aliyemezwa”

na Katibu Mkuu wake, Freeman Mbowe au Tundu Lissu, mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuwachonganisha wananchi na serikali yao.

Kila mmoja husubiri mtu wake asimame na kusalimia au kuzungumza hata kama msema ovyo na akimaliza tu unaona wengine wanaondoka, jambo lililowahi kumtokea Mbowe kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Mlandege iliyopo Iringa mjini, mwaka jana.

Nasema tena ni ujinga kutumia jina la Nape kutengenezea uongo, tatizo linalokuwa kubwa maradufu linapofanywa kwa makusudi hasa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama chochote kile cha siasa! 

Upeo mwingine finyu wa masuala ya kisiasa aliouonyesha Mwigamba ni kudai Chadema “haikamatiki” kwa mkoa wa Arusha, neno ambalo kwa tafsiri ya kawaida maana yake ni “kutowezekana”.

Mkoa wa Arusha una majimbo saba ya uchaguzi ambayo ni Arumeru Magharibi, Arumeru Mashariki, Arusha Mjini, Karatu, Longido, Monduli na Ngorongoro.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, CCM ilinyakua majimbo matano ya Arumeru Magharibi, Arumeru Mashariki, Longido, Monduli na Ngorongoro huku Chadema ikishinda mawili ambayo ni Arusha Mjini na Karatu.

Kama Chadema ingekuwa “haikamatiki” katika mkoa huo ingeshinda yote na siyo mawili peke yake, vinginevyo ingepata angalau sita na kushindwa moja tena kwa taabu, hivyo kutamba kwa Mwigamba inaonyesha jinsi gani alivyokosa hata aibu ya kufikiri kichwani.

Anajishaua akidhani watu hawaelewi au akili zao haziko timamu, hivyo kwa muda wote na mahali popote zinasubiri kuhubiriwa uongo na viongozi wa Chadema kama yeye.
 
Pamoja na uzushi wote alionao, lakini inawezekana akisema chama hicho “hakikamatiki” katika mkoa wa Arusha anamaanisha kuwa hakiwezekani kwa uchochezi, vitisho, vurugu, ghasia, majungu, uongo, uzandiki, inda, chuki, uzabina, umbeya na sema kingine chochote unachojua kuhusu uharamia na ugaidi mkubwa kabisa wa kisiasa duniani. 

Mungu Ibariki Tanzania! 

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM. Anapatikana kwa Simu Na. 0719 822 344 na 0782 133 996

2 comments:

  1. kiongozi nimeikubali HOJA MTAMBUKA inaweka uelewa sawa.

    Viongozi fanyeni utafiti hawa jamaa CDM hawaeleweki sijui wana agenda ya siri?

    Wanazuoni hawaoni sisi wananchi wa kawaida tunahisi.

    zamani kwenye somo la siasa tulieleweshwa kuhusu maadui wa ndani na wa nje ilikuwa inachanganya lakini kwa sasa naona dhahiri

    Lakini nasita kuwaita maadui wa ndani kwani ina hitaji utafiti

    ReplyDelete
  2. hoja mtambuka ni bomba hutoka kila baada ya muda gani?

    nakupongeza kiongozi tupe vitu zaidi

    ReplyDelete

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages