Nape akizungumza na waandishi leo, Dar es Salaam |
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye amesema leo jijini Dar es Salaam, kwamba kikao hicho chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kimeamua upigaji kura huo urudiwe kwa kuwa katika matokeo ya upigaji kura uliopita, hakuna mgombea aliyepata kura zinazovuka asilimia 50 ya kura zote.
Nape alisema, watachuana kwenye marudio hayo ni wagombea wawili, Wiliam Sarakikya na Sioi Solomon ambao waliwashinda wenzao wote katika kura za maoni za awali.
Kulingana na kumbukumbu ambazo mtandao huu unazo ni kwamba katika kura za maoni zilizopita, Sioi aliongoza kwa kura 361 wakati Sarakikya aliyeshika nafasi ya pili akipata kura 259 huku watatu Elishilia Kaaya akipata kura 176.
Nape alisema uchaguzi huo wa kura za maoni utarudiwa Machi 1, 2012 yaani Alhamisi wiki hii, na wapigakura ni wale wale wa Mkutano Mkuu wa jimbo walioshiriki uchaguzi wa kura za maoni uliopita.
Alisema, uchaguzi huo utasimamiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Mzee Pius Msekwa , Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) Kapteni Mstaafu, John Chiligati na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera, Costancia Buhiye.
Nape alisema siku itakayofuata yaani Machi 2, 2012, (Ijumaa), Kamati ya siasa ya wilaya itapitisha majina ya wagombea hao na baadaye siku hiyo hiyo jioni kamati ya siasa ya mkoa itapitia mapendekezo ya wilaya kabla Kamati Kuu kupitisha rasmi jina la mgombea Machi 3, 2012.
Akijibu maswali ya waaandishi wa habari, Nape alisema, hatua hiyo ya Kamati kuu ni ya utaratibu wa kawaida na haikuchukuliwa kwa dharura yoyote lakini ni katika kutekeleza moja ya kanuni za uchaguzi ndani ya CCM na umewahi kutumika.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, uchaguzi mdogo jimbo la Arumeru Mashariki utafanyika Aprili Mosi mwaka huu, baada ya vyama vitakavyoshiriki kwenye uchaguzi huo kuchuana katika kampeni ambazo kipyenga chake kitapulizwa rasmi Machi 9, mwaka huu.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia jimbo hilo kubaki wazi baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremiah Sumari kufariki dunia hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269