Na Mwandishi Maalum, New York
Imeelezwa kwamba linapokuja suala la ukofesu wa ajira, vijana ndio wanaoathirika zaidi ikilinganishwa na watu wazima.
Akifungua mkutano wa 50 wa Tume ya Maendeleo ya Jamii ya Umoja wa Mataifa, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro (pichani kushoto) amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, linapokuja tatizo la ajira, vijana huadhirika mara tatu zaidi ya watu wazima.
“ Takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO)zinaonyesha kwamba mtu mmoja katika kila watu watatu,duniani ama hana ajira au anaishi katika umaksini. Hii ni sawa na zaidi ya watu bilioni moja”. Anasema Naibu Katibu Mkuu na kuongeza.
“Lakini vijana hasa ndio walioathirika zaidi. Ukosefu wa ajira kwao ni mara tatu zaidi ya watu wazima na kwa mwaka jana tu vijana milioni 75 walikuwa hawana ajira” anasema Migiro.
Tume ya Maendeleo ya Jamii ya Umoja wa Mataifa ambayo imeanza mkutano wake siku ya jumatano itakutana kwa siku kumi hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Pamoja na kupokea taarifa mbalimbali, wajumbe wa Tume watajielekeza zaidi katika kujadiliana na kuweka mikakati na mipango madhubuti ya kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana, upunguzaji wa umaskini, mdororo wa uchumi na athari zake kwa maendeleo ya watu na hasa watu maskini na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tunaishi katika nyakati za mashaka, mdororo wa uchumi unaendelea kuchukua mkondo wake. Na matokeo yake ni kuendelea kujengeka kwa chuki miongozi mwa jamii”. anabainisha Naibu Katibu Mkuu.
Kama hiyo haitoshi, Migiro anasema , pengo kati ya matajri na maskini linazidi kuongezeka na , umaskini unaongeza shinikizo katika familia nyingi.
“ katika familia ambayo kuna uhaba mkubwa wa chakula na fedha ni chache, ni wazi kwamba hali ya uvumilivu hutoweka na mifarakano hujitokeza.Lakini pia matukio ya watu kujiua huongezeka, matumiziya dawa za kulevya yamekithiri huku vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto navyo vikiongezeka”.
Akasema vijana ambao ndio tegemeo kubwa hivi sasa wanashindwa kujua nini hatima yao, hawana matumaini tena na wanazidi kukata tamaa ya maisha.
Akaongeza kwamba, maskini wanataka kujinasua kutoka katika dimbwi la umaskini, ni kwa sababu hiyo Umoja wa Mataifa kupitia Tume hiyo inatakiwa kwa kweli, kuwa na sera za kuilinda jamii. Kwa maana ya kuwa na uhakika wa kuwa na chakula, elimu na huduma za msingi hasa kwa maskini.
“Maskini wanataka kujisaidia wao wenyewe na familia zao, tunatakiwa kuwajengea fursa nzuri za ajira.
anasisitiza.
anasisitiza.
Kwa upande wake Rais wa Baraza la Uchumi na Jamii Maendeleo la Umoja wa Mataifa, (ECOSOC) Balozi Milos Koterec, akizungumzia kuhusu ukosefu wa ajira kwa vijana.
Yeye amesema katika mkutano huo pamoja na mambo mengine, Tume ya Maendeleo ya Jamii itatoa kipaumbele maalumu kwa vijana na hususani changamoto ya ukosefu wa ajira.
Akasema katika nchi zilizoendelea katika kila vijana wanne mmoja hana ajira. Ili hali idadi kubwa ya vijana katika nchi zinazoendelea wanajaribu kubangaiza kwa kujiajiri katika sekta zisizo rasmi.
“ Dunia inashuhudia mgogoro mkubwa wa ukosefu wa ajira kwa vijana, ukosefu unaochangia katika uvunjifu wa amani na tishio la usalama katika jamii”. Akasisitiza Balozi Koterec..
Aliongeza kwamba ukosefu huo wa ajira kwa vijana, kunawasukuma kujiingiza katika vitendo vya kudai demokrasia, fursa sawa na kazi zenye tija.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269