Breaking News

Your Ad Spot

Feb 7, 2012

WASANII KUSHEREHEKEA MIAKA 50 YA UHURU MKURANGA

WASANII (wanachama wa SHIWATA) hawakuamini maelezo ya Mwenyekiti wao Mwalimu Cassim Taalib (Ticha) alipowataka kumkumbuka Baba wa Taifa, Mwl Julius Kambarage Nyerere kwa kurudi vijijini ili waweze kupata makazi bora na kutengeneza filamu zao na kazi nyingine mbalimbali pamoja na kilimo ili kujiendeleza kiuchumi na kujiondolea umasikini.

Shirikisho la wasanii Tanzania (SHIWATA) ambalo (Sasa Mtandao wa wasanii Tanzania) ni shirikisho la kwanza la Sanaa nchini ambalo lilianzishwa mwaka 2004 na kusajiliwa na Baraza la Sanaa la taifa (BASATA) kwa shughuli za sanaa Desemba 2005 na SHIWATA pia imesajiliwa na BRELA kama "SHIWATA COMPANY" kwa shughuli za kimaendeleo (KILIMO).

Kutokana na ukweli kwamba wasanii wengi huwa na maisha mabaya wanapostaafu au kuacha kazi zao za kuigiza, kupiga muziki, kuchonga, kuchora na kucheza ngoma hapa nchini, SHIWATA iliwashawishi wanachama wake kurudi vijijini ili kuunga mkono serikali katika juhudi zake za kupata makazi bora na kujiendeleza kiuchumi ili kujiondolea umasikini.

SHIWATA iliungwa mkono na kupongezwa na BASATA pamoja na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika mpango huo, waandishi wa habari na wanamichezo wengine (soka) walikaribishwa kujiunga na SHIWATA.

Mtandao wa SHIWATA ulitumia fedha zilizokusanywa kutokana na ada za kujiunga na uanachama katika kumwezesha kila mmoja wao aliyependa kujiunga na vijiji kununua shamba ili aweze kulima, kujenga na kujiendeleza kiuchumi.

SHIWATA ilikaribishwa vizuri katika kijiji cha Visegese Kisarawe na kupewa ekari 50 kwa ajili ya kilimo ambazo mpaka sasa eneo hilo bado ni mali ya wanachama.

Kati ya wanachama  5,000 wa SHIWATA tayari 1,000 ni wanakijiji wa kijiji cha Mwanzega, Mkuranga mkoa wa Pwani ambao wamefuata taratibu zote za kujiunga na kijiji hicho na ni wanakijiji halali.

Wanachama hao wamepania kufanya kazi kwa juhudi zote kwa kushirikiana na wanakijiji wenzao wa Mwanzega kuleta maendeleo ya kilimo na ujenzi wa nyumba bora za bei nafuu kijijini.

Nyumba tano za awali ambazo zimekamilika zimejengwa kwa njia ya kujichangisha kila mmoja.SHIWATA ilitoa ofa ya punguzo la sh. 1,250,000 kwa wanachama watakaokamilisha mchango wa sh.3,250,000 kati ya Septemba 10, 2011 na Desemba 31, 2011.

Kati ya wanachama wote ni wawili tu,Josephine Joseph Mushi ambaye ni mwandishi wa habari na Flora B. Kafwembe ambaye ni Msanii wa Kikundi cha JKT ambao wameibuka washindi baada ya kukamilisha michango yao kwa wakati.

Wanachama hao wawili watakabidhiwa nyumba zao wakati wa sherehe za uzinduzi ambazo zitafanyika hivi karibuni Mkuranga.

Baada ya kwisha kwa ofa hiyo nyumba tatu ambazo hazijagombolewa pamoja na nyingine ambazo zitajengwa zinagharimu sh. 5,848,000 kwa nyumba za tofali za simenti na sh. mil. 10,012,300 kwa nyumba za matofali ya kupachika (Interlocking Blocks).

Ujenzi wa nyumba hizi tano za awali umegharimu sh. mil. 32,148,100 na wanachama 180 walianza kuchangia ujenzi.

Hii ni historia kubwa kwa wasanii wa Tanzania, Afrika na dunia nzima kwani tunaamini kwamba haijawahi kutokea na ndiyo maana tumeamua kusherekea miaka 50 ya uhuru wa nchi yetu wa Desemba 9, 1961 sambamba na ukombozi wetu huo.

Sherehe hizi zitafanyika kijijini Mwanzega, Mkuranga Februari 28,2012.

Waandishi wa habari pamoja na viongozi mbalimbali Jumamosi ya Februari 11, 2012 watakwenda kukagua ujenzi huo kijijini Mwanzega.

Kutakuwa na mkutano wa wanachama wote Jumamosi ya Februari 18, 2012 makao makuu ya SHIWATA , Ilala saa 3 asubuhi ambako taarifa mbalimbali za maendeleo zitatolewa.
Nguvu ya wasanii ni Umoja 
Mwenyekiti wa SHIWATA
Cassim Taalib
0712 873509

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages