Breaking News

Your Ad Spot

Mar 20, 2012

HOJA MTAMBUKA



Tuhuma za Wabunge hawa dhidi ya Mkapa ni za kijinga
Na Charles Charles 
SIKU moja baada ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kuzindua kampeni za mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha, Sioi Sumari, Mbunge wa Musoma Mjini, Mara, (Chadema) Vincent Nyerere alimtolea maneno yaliyokosa hata adabu ya kuigiza!

Chanzo cha yote ni kauli ya Mkapa, wakati akizindua kampeni za CCM, kusema hajawahi kusikia jina la Vincent katika familia ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“Nimefanya kazi na Mwalimu kwa miaka 25 nikiwa mwandishi wake (wa habari) na waziri. Katika muda huo wote nimemzika yeye, kaka yake na mama yake mzazi. Sijawahi kusikia jina la mtu huyo (akiwa na maana ya Vincent) katika familia hiyo”, alisema Mkapa ambaye pia ni Mwenyekiti Mstaafu wa CCM.

Yalikuwa maneno hayo sambamba na kuwataka wapinzani wazungumze kuhusu sera zao ili wananchi wawapime, ndicho kilichozua mtafaruku wa kijinga.

Akitumia mikutano ya kumnadi mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo hilo, 
Joshua Nassari siku moja baadaye, mbunge huyo alimtuhumu Mkapa kuhusika na 
kifo cha Baba wa Taifa kilichotokea katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini
 London, Uingereza, Alhamisi Oktoba 14, 1999.

“Umefika wakati sasa Mkapa atoke hadharani, afafanue alikuwa na nia gani
 kumlazimisha Mwalimu akatibiwe Uingereza wakati mwenyewe alikuwa 
amekataa kwa sababu ugonjwa uliokuwa unamsumbua, ulikuwa unajulikana na
 daktari wake
 alikuwa anamhudumia bila tatizo”, alisema.

Alimtuhumu pia kuwa ndiye chanzo cha umasikini hapa nchini ukiwemo ufisadi serikalini
 na katika CCM, akidai alileta ubinafsishaji ulioua misingi ya viwanda iliyowekwa na
 hayati Mwalimu Nyerere.

Aidha, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa naye alimtaka Mkapa, CCM na 
serikali yake, kumwogopa Mungu akidai aliwadanganya wananchi wa Arumeru Mashariki
 kuwa wakimchagua Sioi watarudishiwa ardhi inayomilikiwa “na walowezi”.

Huo ndio ulimbukeni na ushamba mkubwa kabisa wa kisiasa na hasa unapofanywa na wabunge wa kuchaguliwa kwenye majimbo yao.

Sioni kosa lolote kwa Mkapa kutomfahamu Vincent wala kusema jina hilo hakuwahi 
kulisikia katika familia ya Baba wa Taifa kwa miaka yote aliyofanya naye kazi, kwanza
 akiwa mwandishi wake wa habari na kisha waziri wa serikali yake.

Kana kwamba haitoshi, sioni uhusiano wowote uliopo kati ya Mkapa kutomjua mbunge
 huyo katika upande wa kwanza na ugonjwa uliosababisha kifo cha Mwalimu, sera ya taifa
 ya ubinafsishaji wala umasikini na ajira kwa vijana katika upande wa pili.

Mwaka 1995, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi 
(UVCCM), Sukwa Saidi Sukwa alisema ana mashaka na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Arusha Mjini kupitia chama cha NCCR – Mageuzi, Kapteni Makongoro Nyerere kama kweli ni mtoto wa Mwalimu Julius Nyerere.

Sukwa alitoa kauli hiyo baada ya Makongoro kumshambulia Mwalimu mkutanoni katika Viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, wakati akimnadi aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho cha NCCR – Mageuzi, Augustine Mrema.

Awali, kampeni za CCM zilizinduliwa na Baba wa Taifa katika viwanja hivyo na kuwataka wapiga kura nchini wamchague Mkapa, wito ambao Makongoro naye alipokwenda hapo ili kumnadi Mrema akautumia kumshambulia baba yake huyo.

“Alikuja hapa mzee mmoja mfupi, mwembamba, amechonga meno, ana mvi kichwa kizima
 na muda wote anatembea na kifimbo mkononi”, alitaja sifa zake bila ya kusema jina lake, kisha akawataka wapiga kura wampuuze kwa kusisitiza:

“Yule mzee ni mjanja sana, alikuja kuwauzia vipande vya chupa vinavyoitwa Mkapa huku akidai ni almasi. Msimsikilize”.  

Maneno hayo mazito ndiyo yalisababisha Sukwa amtilie mashaka endapo kweli ni mtoto
wa Baba wa Taifa kutokana na sababu fupi tu: alikuwa akiyajua vizuri maadili, nidhamu
na malezi waliyolelewa watoto wa Mwalimu Nyerere, hivyo hakutarajia kuona kama kuna wengine wanaweza kumkosea adabu hata mwenyewe, tena hadharani na kiasi hicho!

Akijibu mashaka hayo katika mkutano mwingine wa kampeni hizo, Makongoro alisema kwa hekima na siyo kijinga: “Wanaohoji kama mimi ni mtoto wa Mwalimu waende wakamuulize Mama Maria Nyerere atawaambia”, alijibu kwa kifupi sana na kuishia hapo.

Nilikutana kwa mara yangu ya kwanza na Makongoro wakati wote tukiwa katika kikosi
cha mizinga cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), 342 KJ kule Kunduchi, sasa 742 KJ,  Kigamboni jijini Dar es Salaam, hivyo namfahamu vizuri anavyojenga hoja, kushawishi na uzungumzaji wake usioishiwa mifano kuanzia ya kijeshi, kisiasa, kijamii na hata vinginevyo.

Anaweza kumkabili na kumwambia chochote mtu yeyote na mahali popote, wakati wowote
 na katika hali yoyote. Mmoja wa mashuhuda wazuri wa ujasiri alionao ni aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mwaka 1995, Kanali Abdulrahman Kinana aliyewahi kujionea mwenyewe wakati huo.

Hata hivyo, Makongoro kamwe siyo mgomvi. Hajidai wala hatumii wadhifa wake wowote au chochote ili kujionyesha kwa namna yoyote, kunyanyasa wengine na hata kutamba.

Ndiyo maana pia usingeweza kumtofautisha kwa namna yoyote ile kama mtoto wa Rais, wakati huo na tena enzi zile za chama kimoja na mtu mwingine yeyote.

Hata alipokuwa jeshini alikuwa hatumii kabisa jina la Nyerere ili watu wasijue baba yake mzazi ni nani hapa nchini au ana umaarufu gani duniani. Alijitambulisha mwenyewe kila anapokwenda hasa kwa watu wasiomfahamu, kwamba anaitwa Charles Makongoro.
Nafahamiana vizuri pia na dada yake, mtoto wa baba yake mdogo, hayati Joseph Nyerere anayeitwa Neema, mwalimu kitaaluma aliyeolewa nchini Nigeria.

Huyo naye, licha ya shuleni na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuandikishwa kwa majina matatu ya Neema Joseph Nyerere, lakini hata siku moja alikuwa hapendi kabisa ijulikane kwamba anatoka katika ukoo wa Nyerere ambao duniani ni mmoja tu.

Anataka wakati wote na mahali popote hata kwa marafiki zake aitwe Neema Joseph, naye kwa sababu hana majigambo yoyote, hapendi sifa na hajikwezi kwa mtu yeyote.

Wapo pia marafiki zangu kina Manyerere Jackton na mdogo wake, Kulwa Karedia ambao ingawa ni watoto wa mdogo wake na Baba wa Taifa, Mzee Jackton Nyerere wanayetoka tumbo moja na kwa baba pia mmoja, lakini nao hawapendi wajulikane hivyo.

Chukulia kwa mfano Manyerere aliyelelewa na Mwalimu – Ikulu na Msasani – jijini Dar es Salaam, akasoma shule akiwa hapo, akaanzia maisha yake hapo hadi akaondoka 
mwenyewe ili akajitegemee, kisha uniambie ni wangapi wanafahamu jambo hilo hata aliofanya nao kazi kwa miaka mingi.

Tofauti na Vincent ambaye pia ni mtoto wa mdogo wake tu Mwalimu, yeye angependa ajulikane kwamba ni mmoja kati ya wanafamilia ya Baba wa Taifa kama watoto wake halisi. Anataka awe kwenye orodha ya kina Andrew, Madaraka, Makongoro, Anna, Rosemary au Pauleta.

Ndiyo maana hata alipoulizwa ukweli juu ya mbunge huyo, Madaraka hakusema kwamba kati ya watoto waliozaliwa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na mkewe, Maria, mmoja wao ni mbunge huyo wa Musoma Mjini.

“Nataka kuthibitisha tu kuwa Mheshimiwa Vincent Nyerere ni ndugu yetu, mtoto wa marehemu baba yetu mdogo, Mzee Josephat Kiboko Nyerere”, alijibu na kuonyesha kiasi 
gani mbunge huyo asivyokuwa mtoto wa Mwalimu kama alivyomtilia shaka Mkapa.

Neno “ndugu yetu” maana yake “hatutoki naye tumbo moja au kwa baba mmoja”, badala yake anaweza tu kuwa “mtoto wa mama au baba mdogo ama mkubwa, mtoto wa shangazi 
au wa mjomba” na kadhalika.  

Kuhusu tuhuma alizotoa dhidi ya Mkapa, mbunge huyo ameonyesha kiasi gani alivyo limbukeni kichwani mwake, mtovu wa nidhamu, mjinga wa kufikiri na upeo wake wa 
kuelewa mambo na uongozi wa umma ni finyu kupindukia.

Haiwezekani katika hali yoyote kwa ile Mkapa kumlazimisha Baba wa Taifa alipokuwa hai kufanya kitu chochote bila yeye mwenyewe kutaka, badala yake angeweza tu kumshauri au kumuomba na siyo vinginevyo.

Mkapa alisoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Pugu ambako Nyerere alikuwa mwalimu darasani, akawa mwajiri wake serikali, Mwenyekiti wake katika Baraza la Mawaziri na katika CCM, baba wa taifa lake na sema kingine chochote unachokijua.

Katika hali hiyo hata wakati wote ambao Mwalimu alikuwa ameng’atuka nyadhifa zake zote serikalini na katika CCM, Mkapa asingeweza kumlazimisha chochote iwe kwenda kutibiwa Uingereza, Urusi, Kyuba na hata ndani ya Tanzania yenyewe. Alikuwa bosi wake siku zote tangu walipokutana mwanzoni mwa miaka ya 1950 hadi alipofariki dunia Oktoba 14, 1999.

Najiuliza bila kupata majibu kuwa kumbe nchi yetu ina wabunge “vichwa maji” wanaoweza kusema chochote hata bila ya kufikiri!

Sitaki kujibishana sana na mbunge huyo maana nitaonekana kuwa akili zangu pia ni tatizo, lakini sikubaliani na madai mengine kwa Mkapa kuwa amesababisha umasikini nchini kwa kuuza viwanda, mashirika na makampuni mbalimbali ya umma.

Ni uzoba kudai hivyo kwani hakuna kiwanda au shirika lolote lililouzwa ila kilichofanyika ni utekelezaji wa sera ya taifa ya ubinafsishaji, ile ambayo Rais huyo mstaafu haikuwa yake kama Benjamin Mkapa au na mkewe.

Iliwasilishwa bungeni na serikali ikiwa muswada, hivyo kama sheria hiyo imeleta umasikini, jambo ambalo pia siyo kweli basi anayepaswa kulaumiwa si Mkapa isipokuwa bunge. Hilo ndilo liliipitisha kwa kura walizopiga wabunge kwa niaba ya Watanzania nchini kote.

Sheria hiyo ndiyo iliyounda Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) na 
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kile ambacho kati ya mwaka 1996 – 2005 kilikuwa chini ya Mkurugenzi Mtendaji aliyekuja kuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samwel Sitta.

Ni sheria hiyo iliyoleta soko huru nchini ambapo leo hakuna tena kupanga foleni ya kununua unga, sabuni, mafuta ya kupikia wala kuomba vibali vya kununua vitu kama gari, pikipiki au kompuya.

Ndiyo iliyoleta televisheni kila mahali, vituo vya redio, simu za mkononi ambazo hivi leo wanazo mpaka wachunga ng’ombe, wachimbaji wa mashimo ya kutupia uchafu, wazoaji wa takataka na kuleta maendeleo yote ya kiuchumi na kijamii yaliyopo nchini wakati huu.

Hapo umasikini ulioletwa na Mkapa kwa kubinafsisha makampuni, mashirika na viwanda
 hivyo vya umma uko wapi? Anatetea ujinga wa baadhi ya vijana kushinda vijiweni mchana kutwa bila kufanya kazi wakati wana nguvu na mikono yao yote?

Au, mbunge huyo anataka serikali iajiri wafanyakazi wa kupita nyumba hadi nyumba kila asubuhi, wale ambao kazi yao itakuwa ni kugawa fedha za matumizi ya siku hiyo kwa kila familia kama siyo ujinga?

Sina sababu ya kumjibu Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ambaye najua “anavyonuka” matatizo kuanzia ofisini mpaka mtaani kwake kule Kihesa Kilolo, Barabara
 ya Dodoma.

Namjua kwa sababu nimekaa hapo kuanzia Oktoba Mosi, 2010 hadi Oktoba 9, 2011
 nikiwa Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo. Ndiyo maana alishangilia sana alipopata habari kwamba nimehama. Swali la kwa nini alisherehekea kiasi hicho Iringa “nzima” 
wanafahamu.

Sipendi nilumbane naye kwa sababu nitakuwa nabishana na mtu anayetumia mpaka 
dini 
kuwa kichaka cha maisha yake duniani, vinginevyo hakuna mchungaji aliyebobea kwa 
uzushi, uongo na uhuni mdomoni kama yeye.

Nahitimisha kwa kusema tu kuwa tuhuma zote zilizotolewa na wabunge hao wa
 Chadema dhidi ya rais huyo mstaafu zinatokana ni ujinga wa kufikiri!

Simu Na. 0713 676 000, 0719 822 344,  0762 633 244 na 0782 133 996

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages