Breaking News

Your Ad Spot

Mar 20, 2012

ETI CHADEMA WAMETAKA KUMUUA MAJIMAREFU LEO, KAMBINI KWAO ARUMERU


Na Charles Charles, Arumeru    
Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani aka Profesa Majimarefu, leo, Machi 20, 2012, amedai kunusurika kuchomwa moto akiwa hai, kufuatia amri iliyotolewa na mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.



Majimarefu (pichani) aliyejiunga leo hii na timu ya kampeni za mgombea ubunge wa CCM, Sioi Sumari, anadai kukumbwa  na mkasa huo mida ya saa 3.30 asubuhi.

Alisema akiwa nje ya hoteli ya Elephant iliyopo Usa River aliyofikia juzi alikutana na wabunge wenzake wawili: Vincent Nyerere wa Musoma Mjini, Mchunga Peter Msigwa wa Iringa Mjini na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana 
la Chadema (BAVICHA), John Heche na kuanza kutaniana nao kwa vijembe vya kawaida vya kisiasa kama watu wanaofahamiana.


Wakati akiongea nao huku wakimuuliza katika hali hiyo ya utani kuwa nani amemleta Arumeru, mbunge huyo wa Korogwe Vijijini aliwaona waandishi wa habari wakiwa wamesimama karibu yao na kuamua kwenda kuwasalimia.

Ilikuwa wakati huo ndipo Nassari alipotokea na kuanza kumhoji akitaka kujua amefuata nini hapa Arumeru, lakini kabla hajajibiwa chochote akawaita vijana wa Chadema waliokuwa jirani na kuamuru mbunge huyo wamchome moto.

Wakati mgombea huyo wa ubunge wa Chadema akiagiza hivyo, ghafla akatojikea mzee mwingine na kumtuhumu Majimarefu kwamba juzi asubuhi alitaka kumuua lakini bila ya kusema wapi, madai yaliyomuacha Majimarefu akishangaa kwa vile alikuwa hajafika Arumeru.

Hata hivyo, agizo la kuchomwa kwake moto lilikwama kutekelezwa baada 
ya kukingiwa kifua na wabunge hao wawili pamoja na waandishi wa habari aliokuwa akisalimiana nao mahali hapo.

Kunusurika kwake huko kulitokana na wabunge hao pia, kuhofia kuwa tukio hilo lingeandikwa na kutangazwa kwa uhalisi wake wote na waandishi hao wa habari, hali ambayo ingemweka matatani Nassari mwenyewe na kuharibu sifa na uhalali mzima wa Chadema kama chama cha siasa.

Baada ya kuokolewa, Majimarefu aliondoka katika eneo hilo na kwenda moja kwa moja kuungana na viongozi wenzake waliopo katika timu ya kampeni za Sioi, Gateway Lodge na ndipo akawaambia waandishi wa habari aliowakuta wakiwa katika hoteli hiyo iliyopo eneo la Leganga.

Dakika chache baadaye, Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere alipiga simu yake ya mkononi akimuomba asiende kutoa taarifa polisi kwa vile suala hilo lingeweza kuharibu taswira nzima ya kampeni za Chadema kuonekana kuwa za ghasia, ubabe na dalili za vitendo vya kigaidi.

“Sijaenda popote, naendelea na shughuli zangu za kawaida”, alisikika akisema na baada ya kukata simu akaeleza kwamba aliyekuwa akiongea naye kwenye simu hiyo ni Vincent Nyerere. “Ananiomba nisiende kutoa taarifa polisi”, alisema.

Uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki unafanyika Aprili Mosi na tayari mwenendo wa kampeni zake unaonyesha dalili zote za kuelemewa kwa Nassari. 

Kutokana na hali hiyo, wafuasi wa Chadema wameingiwa woga wa kushindwa kwa mgombea wao na kuanza fujo dhidi ya wana CCM. 

Jumapili jioni, gari aina ya Landcruiser Hardtop lenye usajili namba T 655 BEW likiwa limewachukua waandishi wa habari, lilishambuliwa kwa chupa na vijana wa Chadema, saa 12.45 jioni, likidhaniwa kuwabeba wana CCM waliokuwa wakitoka kumnadi Sioi katika vijiji vya Shishton, Leguruki na Maji ya Chai.

Tukio hilo lilifanyika mbele ya Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na gari hilo lilikuwa limesimama, kupisha gari jingine lililokuwa likiingia barabarani.

Alipoulizwa kama tukio hilo angelitolea taarifa polisi, Majimarefu alisema alikuwa hajaamua, lakini ikibidi angefanya hivyo ili kuweka kumbukumbu sawa endapo hali hiyo itajitokeza tena.

Wiki chache kabla ya kuanza kwa kampeni, Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba alitishia chama hicho, kutumia vijana wa kikosi cha Red Brigade ili pamoja na mambo mengine, kuwapa mkong’oto wana CCM katika kampeni hizo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages