Breaking News

Your Ad Spot

Mar 23, 2012

SEKONDARI YA ACTAS DAR YASITISHA KWA WIKI MBILI HUDUMA YA BWENI KWA BAADHI YA WANAFUNZI

Na mwandishi wetu
UONGOZI wa Sekondari ya Actas iliyopo Mbezi Jogoo mjini Dar es Salaam, umesitisha huduma ya bweni kwa baadhi ya wanafunzi wake kwa muda wa wiki mbili.

Wanafunzi hao ni wale wanaoishi jijini Dar es Salaam huku kwa wale wanaotoka nje ya jiji wataendelea kupatiwa huduma hiyo kamakawaida.

Hatua hiyo inatokana na ukarabati wa baadhi ya mabweni na uhaba wa maji shuleni hapo na maeneo jirani, kufuatia kuharibika kwa miundombinu ya usambazaji.

Akizungumza na waandishi wa habari mjiniDar es Salaam, jana Meneja wa Shule hiyo Chacha Mghituti, alisema huduma za chai na chakula cha mchana kwa wanafunzi hao zitaendelea kutolewa kama kawaida.

Alisema huduma ya bweni kwa wanafunzi hao itasitishwa kwa wiki mbili ili kutoa fursa kwa shule kufanya marekebisho kwa lengo ili kuboresha mazingira na kuendelea kutoa huduma bora zenye viwango vya juu.

Alisema huduma ya bweni imesitishwa kuanzia juzi na kwamba, itarejea tena Aprili 16, mwaka huu.

“Tumesitisha huduma ya bweni kwa baadhi ya wanafunzi waishio hapa Dar ili tupate fursa ya kufanyia ukarabati baadhi ya majengo na kuboresha huduma za maji. Kuna tatizo la maji katika maeneo ya shule na jirani hivyo, ni lazima tuchukue hatua ili kudhibiti hatari inayoweza kutokea,” alisema Mghituti.

Alisema tayari wamewasiliana na wazazi, ambao wameafiki na kupongeza uamuzi huo wenye lengo la kulinda afya za wanafunzi.

Alisema ukarabati huo unaendelea kufanyika kwa kasi ili wanafunzi waweze kurejea kwa muda uliopangwa.

“Tunajali afya za wanafunzi na walimu wetu, kuna tatizo la maji kutokana na miundombinu kuharibika, hivyo wanafunzi waishio hapa mjini watakuwa wakitoka nyumbani kuja shuleni, lakini huduma za chakula zitaendelea kamakawaida,” alisema.

Baadhi ya wazazi na majirani wanaozunguka shule hiyo, wamesema kumekuwepo na tatizo kubwa la maji katika maeneo hayo na kwamba, uamuzi wa shule ni muafaka.

“Hawa wanajali afya za wanafunzi, wamechukua uamuzi mzuri na hawana budi kupongezwa kwani, ingekuwa wengine wangeendelea kuwajaza wanafunzi ili wapate fedha wakati kuna matatizo,” alisema Benson John, mkazi wa Mbezi.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages