Breaking News

Your Ad Spot

Mar 27, 2012

TUWE MACHO NA ONGEZKO LA AINA MPYA YA UTUMWA NA UBAGUZI WA RANGI- MIGIRO

Kikundi cha Utamaduni cha Cameroon kilitumbuiza katika maadhimisho hayo, kwenye Ukumbi Mkuu wa Mikutano wa  Baraza kuu la  Umoja wa Mataifa

Na Mwandishi Maalum
New York
Ikiwa ni zaidi ya miaka 200 imepita tangu biashara ya utumwa na utumwa ulipokomeshwa. Jumuiya ya Kimataifa, imetakiwa kuwa macho  dhidi  ongezeko kubwa la   aina mpya ya utumwa unaojikita katika misingi ya  ubaguzi wa rangi, biashara haramu ya binadamu, utumwa wa madeni, unyanyasaji  na udhalilishaji wa kijinsia, ndoa za utotoni  na utumiaji wa watoto katika vita.

Tahadhari hiyo imetolewa  siku ya jumatatu wiki hii na   Naibu   Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha- Rose  Migoro wakati Umoja wa Mataifa ulipoadhimisha siku ya kimataifa ya  ukomeshaji wa biashara ya utumwa na utumwa, maadhimisho ambayo hufanyika   Marchi 25 ya kila mwaka.

Kauli mbiu ya mwaka  huu katika maadhimisho hayo ni “kuwaenzi  mashujaa , wapinzani  na waathirika wa  biashara ya   utumwa”. Pamoja   hotuba  maadhimisho hayo  yalipambwa  na kikundi cha utamaduni kutoka nchini Cameroon.

Migiro amesema, licha ya kwamba  kumekuwapo na sheria mpya na mbinu mpya  na bora za kukabiliana na vitendo vya   ukiukwaji wa haki za binadamu. Hata hivyo anasema. “  Ni lazima tukubali kwamba   kunaongezeko la vitendo vinavyoashiria wazi kuwapo kwa ubaguzi kwa misingi ya rangi katika maeneo mengi duniani”.

Na kuongeza kwamba  kauli zinazoashiria ubaguzi wa rangi  zimekuwa zikiongezeka kupitia  majukwaa  ya kisiasa, katika baadhi ya vyombo vya sheria, mashirika na katika matumizi ya teknolojia za kisasa za mawasiliano ambapo  vyombo hivyo vimekuwa vikitumika kueneza dhana hasi ya kwamba rangi moja ni bora dhidi ya rangi nyingine.

 Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa  kila mtu anao wajibu wa pamoja  wa kuwa macho juu ya ongezeko la vitendo hivyo vya  ubaguzi wa rangi na aina mpya ya utumwa.

Akabainisha kwamba maadhimisho hayo licha ya kuwakumbuka mamilioni ya waafrika walioathiriwa na  janga  la kutisha la biashara ya utumwa na utumwa. Maadhimisho  hayo ni  lazima pia yatumike kama sehemu kujifunza sababu na matokeo ya biashara ya utumwa, ukandamizaji na  ubaguzi wa rangi. ubaguzi ambao uliifanya  rangi  moja ya  binadamu kujiona kuwa ni bora zaidi dhidi ya rangi nyingine.

Akamaliza kwa kusema “ kwa kupitia  siku hii basi sote tuonyeshe dhamira ya kukabiliana na kupambana na ubaguzi wa rangi na kujenga jamii bora kwa kuzingatia usawa , haki na mshikamano”.

Pamoja na   Naibu Katibu Mkuu  kuzungumza katika maadhimisho hayo, Rais wa  Baraza  Kuu la 66 la  Umoja wa Mataifa, Bw. Nassir Abdulaziz Al-Nasser naye alizungumza ambapo kama ilivyo kuwa kwa Naibu Katibu Mkuu, alisisitiza haja na umuhimu wa  Jumuia ya Kimataifa kuunganisha nguvu dhidi ya aina mpya ya utumwa.

Akasema  jumuia ya kimataifa inapashwa kujifunza  kutoka yale yaliyojitokeza katika biashara ya utumwa na utumwa na kuhakikisha  matukio yale ya kutisha yalioathiri na kuudhalilisha utu  na hadhi ya Mwafrika  hayajirudi   kwa namna  moja ama nyingine au katika mfumo wowote ule.

Akabainisha kwamba mwaka 2007 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  liliitenga  Marchi 25 ya kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya kuwakumbuka  wa Wafrika zaidi ya milioni 28 walioathirika na  janga kubwa la  biashara ya utumwa na utumwa kupitia  bahari ya  Atlantik.

Aidha Bw. Al- Nasser amezikumbusha nchi wanachama ambazo   hazijachangia mfuko wa ujenzi wa mnara wa kudumu wa kumbukumbu ya utumwa kufanya hivyo.

Mbali ya Rais wa Baraza   Kuu la Umoja wa Mataifa, wazungumzaji wengine katika maadhimisho hayo walikuwa ni  Balozi Chitsaka Chipaziwa  wa  Zimbabwe aliyezungumza kwa niaba ya nchi za Afrika,  Balozi Jane Chigiyai  wa Micronesia aliyezungumza kwa niaba ya nchi za Asia na Pacific, Balozi Petrika Jorgji wa Albania aliyezumgumza kwa  niaba ya nchi za  Ulaya  Mashariki na Balozi Dessima Williams ambaye alizungumza kwa niabya ya  nchi za  America ya Latini na Visiwa vya  Caribbean.

Wengine waliozungumza ni Balozi Daniele Bodini wa San Marino aliyezungumza kwa niaba ya nchi za Ulaya Magharibi na nchi nyingine, na Balozi Rosemary DiCarlo aliyezungumza kwa niaba ya Marekani. Wakati  Dkt. Rick kittles  ambaye ni Mkurugenzi wa African Ancestry,Inc yeye alitoa mada kuhusu historia ya utumwa na madhira yake kwa mtu  mweusi na matumizi ya vinasaba katika  kuwasaidia wamarekani  wenye asili ya Afrika  kutambua asili ya kule walikotoka.
Maadhimisho  hayo ya  kumbukumbu  ya  biashara ya utumwa na utumwa yanafanyika kwa juma zima  yakihusiaha pia, midahalo ya wanafunzi, asasi zisizo za kiserikali, maonyesho ya sanaa mbalimbali zinazohusiana na utumwa, filamu makala mbalimbali  pamoja na vyakula vya asili ya Afrika.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages