Na Mwandishi Maalum
New York
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, limelaani vikali mapinduzi ya
kijeshi yaliyofanywa na askari wa chache dhidi ya serikali ya kidemokrasia
nchini Mali. Na limewataka wanajeshi hao kuachana na vitendo vya kihalifu na
fujo na kurejea katika makambi yao.
Taarifa iliyotolewa na Rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa
Marchi Balozi wa Uingereza Bw. Mark Lyall Grant (pichani) amesema.
“ Baraza la Usalama linalaani mapinduzi
hayo na linawataka wanajeshi kurudi katika makambi yao na linatoa wito
wa kurejeshwa kwa utaratibu wa
Katiba na kufanyika kwa uchaguzi
kama ilivyokuwa imepangwa.
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana
siku ya jumatatu ambapo lilijadili kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu
katika Kanda ya Afrika ya Sahel, ambapo lilisema kwamba kuongezeka kwa
makundi yenye silaha na magaidi pamoja
na kuzagaa kwa silaha kumeongeza hali ya wasiwasi katika kanda hiyo.
Wiki iliyopita
baadhi ya wanajeshi wa nchi Mali wakiongozwa
Kapteni Amadou Haya Sanogo walitangaza kuipindua serikali ya Rais Amadou
Toumani Toure ambaye mpaka sasa hajulikano aliko.
Katika mkutano huo ambao uliwahusisha wajumbe 15
wanaounda Baraza Kuu la Usalama, Baraza hilo pia limelaani vitendo
vinavyofanywa na baadhi ya makundi ya waasi ya kuvivamia vikosi vya serikali na
kuwataka waasi hao kusitisha aina zote
za vurugu na kutafuta ufumbuzi wa amani
kwa njia ya mazungumzo ya kisiasa. Aidha Baraza
hilo limesisitiza haja ya kuzingatia na kuheshimu uhuru, umoja na
mipaka ya nchi.
Tayari Umoja wa Afrika ( AU) umekwisha kutanga
kutoyatambua mapinduzi hayo, huku baadhi
ya nchi ikiwamo Marekani
ikitangaza kusudio la kusitisha
misaada kw anchi hiyo , nchi ambayo uchumi wake kwa asilimia kubwa unategemea sana misaada kutoka nchi wahisani.
Kuhusu hali tete ya kanda ya Sahel, Baraza
limebainisha kuwa hali ya ukame , uhaba wa chakula na kurudi kwa maelfu ya watu kutoka Libya kumeongeza hali
ugumu wa maisha kwa watu wa eneo hilo. Hali ambayo imesababisha maelfu ya
wananchi wa eneo hilo kukimbilia katika nchi za jirani kutafuta hali bora ya
maisha.
Kutokana na hali hiyo, Baraza Kuu la
Usalama la Umoja wa Mataifa,
limetoa wito kwa mamlaka za kitaifa
na kimataifa, kikanda na masharika ya misaada ya
kibinadamu kuchukua hatua za
haraka kuimarisha juhudi za kuwasaidia wananchi wa eneo hilo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269