.

HOJA MTAMBUKA

Apr 25, 2012


UFISADI HUU NI HUJUMA KWA RAIS KIWETE NA CCM, ZICHUKULIWE HATUA STAHIKI
Rais Jakaya Kikwete
Na Mwandishi Wetu
WAKATI anaingia madarakani mwaka 2005, Rais Jakaya Kikwete aliahidi Maisha Bora kwa kila Mtanzania, lakini kimsingi ahadi hii haikuwa yake binafsi, ilikuwa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kilichompa tiketi ya kugombea urais.
       Wakati anakaribia kumaliza awamu yake hii ya pili ya urais, tayari yamezuka maneno kwa minong'ono na wazi kwamba ahadi hiyo haijatekelezeka.
       Wanaosema hivyo wanatumia vigezo mbalimbali ambavyo baadhi vinakubalika lakini vingine ni majungu yanayopikwa na wenye malengo yao binafsi mabaya hasa ya kisiasa.
       Suala la majungu si la ajabu sana, kwa sababu, upo ushahidi wa wazi kwamba baada ya Rais Kikwete kushika hatamu za uongozi, wapo wapinzani wake  ambao waliomba dua zao usiku kucha na wanaendelea kuomba hadi leo ahadi hiyo isifanikiwe ili aonekane hafai.
      Hata baadhi ya viongozi wa upinzani hasa Chadema wamewahi kusema kwamba watahakikisha nchi haitawaliki ikiwa na maana kwamba watafanya hila za kila aina Rais Kikwete aonekane ameshindwa kutawala nchi.
      Zaidi ni kwamba wakati wapinzani wao wamejiapiza namna hiyo wazi wazi, wapo wanaokula njama za chini chini, na hawa si ajabu kuwemo hata ndani ya CCM na watumishi wa umma ambao hawajipambanui kwa vyama vya siasa.
       Lakini kilicho kibaya zaidi wote hawa hawaishii kusema na kula njama tu, lakini huzua mbinu mbali mbali kila kukicha kuhakikisha azma hiyo mbaya inatimia.
      Wakati njama nyingi za wapinzani ni zile za dhahiri, njama mbaya zaidi ni zinazofanywa na 'kikulacho' ambao kwa abahati mbaya imekuwa vigumu kwa Rais Kikwete kuwajua kwa urahisi kiasi kwamba anawapanga hadi kwenye kusimamia mipango ya kutimiza ahadi yake ya Maisha bora kwa kila Mtanzania ambao badala ya kumsaidia wanakwamisha makusudi utekelezaji wa ahadi hiyo!
      Zipo kadhia nyingi ambazo zinaonyesha kabisa kwamba hazikufanywa na watu wajinga, ila wenye akili timamu lakini kwa nia ya kuangusha utendaji wa Rais Kikwete. Mfano mmojawapo ni huu wa kadhia uliobainika juzi juzi kufuatia ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
      Kudhihirisha kwamba, watu hao ni 'kikulacho', katika ripoti hiyo ambayo pia imewasIlishwa Bungeni mjini Dodoma, imebainishwa kuwa katika fedha alizowakabidhi Rais mwenyewe  kwa lengo safi la kuboresha maisha ya Watanzania alizoziita 'Mabilioni ya JK'  kati yake Sh. bilioni 21, zimeyeyushwa bila kufika kwa walengwa!.
      Wakati zikitajwa 'kuliwa' hizo sh. bilioni 21 za Mabilioni ya JK, orodha nyingine ya utumiaji hovyo wa fedha ambayo imetajwa na kuwaacha watu midomo wazi, wakiulizana, je waliopewa dhamana na Rais kusimamia fedha hizo zitumike vizuri walikuwa likizo au walikuwepo, imetajwa.
       Fedha hizo (kwenye mabano) na maeneo yaliyohusika ukiacha za Mabilioni ya JK, kwa mujibu wa mkaguzi  mkuu wa hesabu za serikali ni, Wizara ya Afya (Sh. bilioni 10), Maliasili na Utalii (sh.  milioni 874.9), Shirika la Viwango-TBS (Sh.  Dola milioni 18.3), Bodi ya Pamba (sh. bilioni 2) na Ukwepaji kodi (sh. bilioni 15.4.
       Maeneo mengine ni Magari ya serikali (sh. trilioni 5), Mishahara hewa (Sh. bilioni 1.8), ununuzi tata (sh. bilioni 8), Kiwanja CHC (sh. bilioni 3), Idara ya Mhasibu Mkuu (sh. bilioni 49), Udhamini wa serikali (sh. trilioni 3) na Tanesco (sh. bilioni 600).
       Hapana shaka sisi wengine na bunge wamepata mtiririko huu baada ya Rais Kikwete kuwa tayari ameshapaupata kwa sababu ripoti yenye 'madudu' hayo ilikabidhiwa kwake na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Rudovick Uthoh mapema zaidi.
       Naamini Rais Kikwete, atachukua hatua za dhati dhidi ya waliohusika, lakini naamini pia kwamba hatua atakazochukua si kutokana na shinikizo la yeyoye kwa kuwa  atakuwa alikwisha dhamiria kufanya hivyo tangu siku ile alipopokea ripoti yenye madidu hayo.
       Tangu kadhia hiyo ilipofika bungeni na kushika kasi, wapo watu ambao  wameibuka na maoni kwamba kwa nini Rais Kikwete hakuwachukulia hatua mapema?
        Bila shaka alivuta subira kwa makusudi ili jambo hilo lifike bungeni kwanza, wananchi wapate kulijua kinaga ubaga, kwa sababu angechukua hatua kimya-kimya  wapo pia ambao wangeibuka na hoja kwamba waliohusika wameonewa.
        Hata hivyo nawashangaa sana wale wa upande wa pili waliowahi kusema kwamba nchi haitatawalika, Dk. Wildrod Slaa na Freeman Mbowe wa CHADEMA ambao eti wao wanasema kelele zilizopigwa na wabunge wa CCM na hatua zikichukuliwa kwa waliohusika haitakuwa dawa ya ufisadi nchini.
        Eti wanasema kwamba walikwishasema siku nyingi kuwa ufisadi upo hapa nchini. Sawa, tukubali kuwa walisema, je walisema peke yao? viongozi wa CCM kina Dk. Harrison Mwakyembe, Mama Anna Kilango Malecela, Christopher Ole Sendeka, Samwel Sitta na wengine kadhaa hawajawahi kusema?
       Kwani wahubiri wa dini hawajawahi kusema katika nyumba za ibada na hata kwenye miskusanyiko ya kidini na hata kwenye mazishi, kwamba kutenda dhambi ni dhambi? mbona bado wapo watu wanaoendelea kufanya dhambi? 
       Si kweli kwamba, Rais Kikwete akichukua hatua au mawaziri kujiuzuru kwa kadhia hiyo, haitasaidia lolote kusafisha nchi eti mpaka CCM iondoke madarakani! Mbona huo ni uongo wa mchana kweupe? Yaani eti Chadema ikishika nchi ndiyo Tanzania iwe kama peponi kusikokuwa na dhambi?
        La msingi ni kwamba chama chochote kikiwa madarakani, ni lazima uongozi wake uwe mkali, kufuatilia na kuwachukulia hatua wanaobainika kutapanya mali za umma, basi.
        Lakini kuhadaa watu kwamba ni aina ya chama fulani ndicho kitaleta uongofu wa milele, si kweli kabisa, labda ikubalike kwamba kauli hiyo ya kila Dk. Slaa ni ya kujaribu kuwateka watu wakati huu ambapo miluzi ni mingi, maana wakati miluzi inapokuwa mingi ndipo mbwa hupotea mawindoni.
       Kwa dhati kabisa namtakia kila la kheri na ujarisi usio kifani Rais Kikwete, kuhakikisha kadhia hiyo ya upetevu wa matrilioni ya fedha anaichukulia hatua za dhabiti, , hatua hiyo isiwe ya kufurahisha au kuliza yeyote, bali ilenge zaidi kukidhi matakwa ya haki na utawala bora. Mwandishi wa Hoja hii anapatikana kwa si0789498008mu 

1 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช