Breaking News

Your Ad Spot

Apr 14, 2012

HOJA MTAMBUKA


UKWELI UNAPOPOTOSHWA KUHUSU YALIYOJIRI ARUMERU
*Kejeli za Chadema kwa CCM halua, lakini za CCM kwa Chadema shubiri!
Na Mwandishi Wetu
Baada ya matokeo ya uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki kuipa Chadema ushindi mambo mengi yameendelea kujadiliwa katika hadhi mbalimbali.

Kimsingi mjadala sasa si nani mshindi katika uchaguzi huo kwa sababu Chadema wameshashangilia sana ushindi huo na CCM nao kutokana na ukomavu wao kisiasa wameshakubali matokeo na kuipongeza Chadema.

Kwa sababu si nia yangu kuzungumzia tena jinsi na namna uchaguzi ulivyokwenda kama kuna chama kilitumia mamluki kushinda au la, lakini nachotaka kujadili hapa ni jisni ambavyo baadhi ya vyombo vya habari vinajaribu kuonyesha kuwa CCM ilitumia fursa ya kampeni kutukana.

Nitatumia mfano wa mwandishi mmoja mwenye safu yake anayoiita 'FIKRA MPYA' katika gazeti moja la kila siku, akijaribu kuzifanya fikra zilizofikiriwa miaka mingi kuwa ni fikra mpya kwa kueleza kwamba CCM haikupaswa kutangaza kukubali matokeo na kufanya hivyo ilikuwa mbinu tu si kutoka moyoni.

Mwandishi huyo ameeleza mengi katika safu yake hiyo, lakini nataka tujadili naye na wewe msomaji, kuhusu baadhi ya mambo aliyoandika.

Kwa kuwa ninaamini kuwa mpo mnaosoma makala hii ambao hamkuisoma safu ya mwandishi huyo, hivyo   nanukuu baadhi yake kama alivyoandika:-

 "Jumatatu wiki  hii nimeshangazwa na kauli ya  Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi Nape Nnauye, ikiwa ni siku moja  baada ya chama hicho kugaragazwa  na Chadema kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Arumeru Mashariki.

Katika tamko hilo Nape alisema kuwa CCM wanakubali kushindwa na Chadema kwenye uchaguzi huo, ndio uamuzi wa wananchi wa Arumeru kumkubali Joshua Nassari na hivyo wao wanawapongeza washindi na kuwataka watimize ahadi walizozitoa wakati wa kampeni.

Mwanafalsafa mtaalamu wa maadili wa Ujerumani Emmanuel Kant anasema "The end does not justfy the means" kwa kiswahili unaweza kutafsiri maneno hayo kwamba 'Matokeo hayahalalishi njia iliyotumika kuyapata'. 

Kwamba unaweza kufanya jambo kwa nia njema lakini mwisho wake ukawa mbaya au ukafanya kwa nia mbaya mwisho wake ukawa mzuri.

Hivyo, niliposikia kauli ya CCM kupitia kwa Nape, niliduwaa  na kushangazwa sana, kwani nia ilikuwa ni njema lakini matendo ya kipuuzi yaliyofanywa na makada wao kwenye kampeni huko Arumeru na kisha wakapoteza jimbo lao hilo, isingekuwa rahisi kwao kukubali kushindwa.

Nasema hivyo kwa sababu ni CCM hiyo hiyo iliyowatumia  wabunge wake kama Livingstone Lusinde  (Mtera) huko Arumeru kuwatukana matusi mazito viongozi wa Chadema na familia zao, ambayo kimsingi na kimaadili hayawezi kuandikika ila kuonywa na chama chake.

Narudia kusema kuwa inashangaza maana hata Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama, alipozungumza na waandishi wa habari katikati ya wiki hii, bado aliendelea kumsifu Lusinde kwa amatusi yake hayo akisema alikuwa najibu mapigo ya Chadema, sasa hapo ndipo utaona kwamba busara aliyojitwika Nape ilikuwa ya shaka.

Ni CCM hiyo hiyo ilitumia mabilioni ya fedha kuwarubuni wananchi wasiichagaue Chadema, ikatumia polisi, Tume ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama Vya siasa kuhakikisha inalitwaa jimbo kwa nguvu, halafu eti watu wale wale wawe na busara na hekima ya kukubali kushindwa na kutoa pongezi. 

Kama CCM ilikuwa na ukomavu huo kisiasa  ni kwa nini isingeanza kwa kuwakemea na kuwaadhibu  Lusinde kwa matusi na  Benjamin Mkapa na Waziri Stephen Wasira  kwa kusema uongo wa kukashifu familia ya Mwalimu Julius Nyerere na Kanisa Katoliki?

Lakini Kama nilivyotangulia kumnukuu mwanafalsafa  Kant, ndivyo hivyo nataka msomaji wa safu hii uelewe kuwa CCM walikimbilia kutuhadaa kwa kukubali kushindwa Arumeru kwa vile tayari walikwisha kufahamu nini wanataka kukifanya kwenye jimbo jirani la Arusha Mjini". Mwisho wa kunukuu.

Baada ya kukurejesha neno kwa neno kama alivyoandika kwandishi huyo, sasa tuje kwenye hoja zake.

Kwa akili yake anaona kwamba CCM isingejitokeza kukubali kushindwa Arumeru Mashariki eti badala yake angeridhika kama ingewaadhibu kwanza Lusinde kwa matusi na Mzee Mkapa na Waziri Wasira kwa kusema uongo na kukashifu familia ya Mwalimu Nyerere na Kanisa Katoliki. Na kwamba haikuwachukulia hatua hizo na badala yake kukubali matokeo kinafiki eti kwa kuwa ilikuwa tayari inajua ilichopanga kukifanya jimbo la Arusha mjini!

Tena amethubutu kuandika kwamba CCM ilitumia mabilioni ya fedha na taasisi za serikali kuhakikisha inalitwaa jimbo la Arumeru Mashariki.

Katika biblia Methali 9, kuna maandiko yanasomeka hivi  "...Na akili ya mtu mwenye hekima hutafuta maarifa vizuri isile upumbavu"

Yaani huyu mwandishi kwa hekima yake angeridhika kama CCM isingetangaza kushindwa badala yake ianzishe mzozo wa wenyewe kwa wenyewe ndani ya Chama kwa kuwasakama kina Lusinde, Mzee Mkapa na Wasira, CCM si wajinga kiasi hicho.

Kila mtu anatambua kwamba mbinu mbalimbali hutumika kusaka ushindi wakati wa mapambano hata ya ngumi, kama Chadema wanavyoshutumiwa kuwa walitumia mamluki na vitisho kushinda Arumeru, lakini baada ya yote mshindi akisha tangazwa na taasisi halali ni lazima kwa viongozi wenye busara wakubali matokeo kama ilivyofanya CCM.

Haishangazi kwa mwandishi huyo kaona ajabu ya CCM kukubali kushindwa kwa sababu inawezekana hajazoea kuona mshindwa akikiri matokeo kwa kuwa mazoea hayo ameyapata Chadema ambao daima huwa hawakubali matokeo kama walivyofanya, Busanda, Biharamulo na Igunga wakati waliposhindwa chaguzi ndogo.

Lakini CCM haikuona uzito wowote kwa sababu inajua katika ubondia ngumi zimeruhusiwa kupigwa usoni, kwa hiyo mtu anaposhinda katika mashindano halali hata kama amekuumiza usoni lazima ukubali matokeo na umpongeze, huo ndiyo uungwana au 'fair play'  na ukomavu  katika siasa.

Eti CCM ilijua itakachokifanya Arusha Mjini, ndiyo sababu ikakubali matokeo ya Arumeru! ukisikia uvivu wa kufikiri ndio huo. Yaani hata mwandishi huyo hajiulizi kwamba hivi kutenguliwa kwa ubunge wa Lema kunaifanya CCM iwe mshindi Arumeru Mashariki?  Au mtu mwenye hekima na busara isiyoambulia upumbavu kama inavyosema Biblia, anaweza kumuuza mtoto wake mmoja aende kuuliwa, kumukoa mtoto wake mwingine badala ya kutetea wabaki salama wote?

Kimsingi CCM haikuona haja ya kuwaskama kina Lusinde kwa sababu, hakuna walilosema la uzushi au matusi kwa maana ya matusi, kwa  sababu kila waliyokuwa wakitamka yalikuwa majibu kwa yale ya Chadema, na kwa kweli natumia fursa hii kumpongeza Lusinde na aliyekuwa Mratibu wa kampeni za CCM, Katibu wa Uchumi na Fedha, Mwigulu Nchemba kwa jinsi walivyokuwa wakijaribu kuyapangua matusi ya Chadema, maana kwa wale waliokuwa wakifuatilia kampeni za Arumeru, wanajua kuwa Chadema ndio waliongoza kwa matusi na kejeli kwa CCM na viongozi wake.

Tena mwandishi huyo anaandika katika makala yake kuwa matusi anayodaiwa kutoa Lusinde  hayaandikiki ila kuonywa tu na Chama, ni kweli hawezi kuyaona mepesi na ya kutajwa  kwa sababu ni kawaida mtu akitukana tusi zito, anapojibiwa kwa kuambiwa 'mwenyewe' hawezi kulirudia tusi kwa sababu humuuma zaidi,  lakini kiukweli hayo anayoita matusi ya Lusinde yanasemeka tangu kimaadili ya jamii na hata ya uandishi wa habari.

Hivi ni kweli kwamba kutamka neno shoga ni tusi lisilosemeka wala kuandikika? Maana hayo ndiyo yaliyosemwa na wapiga kampeni wote na kama ni baya kiasi hicho na linauma basi wakanywe wote si kumganda Lusinde tu ukawaacha viongozi wa Chadema waliolianzisha.

Kwa mfano baada ya CCM kumpitisha Sioi Sumari, kuwa mgombea wake  Arumeru Mashariki kiongozi mmoja wa Chadema na wenzake waliibuka na kueneza si tusi tu ila uongo kwa  wapiga kura wa Arumeru kwamba wasishughulike na Sioi eti ametoga sikio, neno ambalo mwanamume akiambiwa tafsiri yake haiendi mbali na kumtusi kwamba ni shoga!

Kwa vyovyote Chadema walisema hivyo wakijua kwamba Sioi hakuwa ametoga sikio, lakini kwa bahati mbaya au makusudi wakaona ndiyo 'ngumi' ya kwanza ya usoni  ambayo walidhami ingewachosha CCM mapema na kuwapatia wao kura nyingi.

Je, kwa muktadha huo, CCM ilipaswa kunyamaza isijibu lolote kwa 'dongo' kama hilo kwa kisingizio kuwa itakuwa imetukana? Bila shaka ilikuwa lazima CCM ijibu mapigo kama alivyosema Mukama. Na kwa kweli karibu katika mikutano yote CCM ilijaribu kuijibu kadhia hii ili kujaribu kunusuru isipoteze kura kwa jambo hilo la kipuuzi. 

Katika mkutano mmoja, Lusinde alisema, " Sikilizeni wananchi, hawa Chadema wamekuwa wakisema eti mgombea wetu ametoga sikio, hebu mtazameni, ametoga huyu?  wananchi wakajibu "hapana". Kisha Lusinde akasema "wakati mwingine unaweza ukamrushia mtu tusi ukidhani umemkomesha, kumbe umejitukana na wewe pia, ...wananchi kama Chadema wanasema huyu Sioi katoga na hivyo ni shoga, je hili si tusi pia kwa vijana na wazee wa makabila ambayo hutoga masikio akiwemo baba yake Dk. Slaa?"

Ni dhahiri limekuwa tusi zaidi, lakini mwandishi au Chadema wenyewe wamejiuliza kwamba walipolianzisha kulisambaza neno hilo, hawakuwa wanajua kwamba baadhi ya jamii nyingi za Watanzania wakiwemo wa Arusha hutoga masikio? na je hawakujua kwamba kulisambaza tusi hilo wanajitusi wenyewe pia?

Lingine ambalo linawakera Chadema hadi kujaribu kutumia wandishi wao katika baadhi ya vyombo vya habari  kuonyesha kuwa Lusinde ameikosesha kura CCM kwa matusi, ni mfano aliokuwa akiutoa kwenye kampeni kuilinganisha Chadema na jogoo katika ahadi zao.

Katika mfano huo Lusinde alikuwa akisema, "Chadema ahadi zao ni za uongo kama jogoo ambaye akimtaka kuku mtetea, anamhadaa kwamba nitakushonea nguo ndeeefu hadio miguuni, lakini jogoo mwenyewe akiinama hana hata nguo ya ndani".

Kila akisema hivyo Lusinde alitoa ufafanuzi kwamba, anakusudia kuwaleza wananchi wajue kwamba ahadi za Chadema kwenye uchaguzi huo hazitatekelezeka, kwa sababu uchaguzi huo ni mdogo, haubadilishi serikali, hivyo hata akipita mbunge wa Chadema bado sera na mipango itakayokuwa inatekelezwa ni ya CCM.

Tena akiwapa mifano kwa akuwahoji kwamba, katika kampeni hizo Chadema wanawaahidi kwamba wakichaguliwa watashusha bei ya sukari, je kama ahadi hiyo si uongo mbona  Moshi, Hai na Arusha mjini ambako wana wabunge mbona bei ya bidhaa hiyo haijashuka?

Je, si tusi linalostahili kujibiwa  Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa Chama hicho Dk. Wilbrod Slaa, wanaposafiri kwa magari wamesinzia hadi Arumeru kutokana na ubora wa barabara ya lami iliyojengwa na uongozi wa serikali ya CCM,kisha wakasimama jukwaani na kusema kwamba serikali haijafanya lolote wakati anajua nchi ilikotoka?

Sasa Lusinde akisimama jukwaani akasema Chadema ni waongo wa kutupwa wasio na shukurani, wanaowadanganya wananchi na kuitukana serikali ya CCM kuwa haijafanya kitu, wakati kilichofanyika kipo, kwa mifano michache, wamesoma hadi vyuo vikuu, wengine wamezaliwa katika kliki za hospitali za serikali ya CCM bure, utasema katukana matusi yasiyoandikika gazetini?

Ahh! eti Mzee Mkapa achukuliwe hatua na CCM kwa uongo! uongo gani? Yeye akiwa jukwaani alisema, "huyu Joseph Nyerere si mtoto wa Mwalimu Nyerere"  hakusema si mwanafamilia, lakini kwa ajili ya uchonganishi Chadema wakatumia baadhi ya waandishi kueneza maneno kwamba amesema Joseph si mwanafamilia ya Nyerere,  wakati wanajua wazi kwamba kweli ni Joseph  ni mwanafamilia wa Nyerere  kwa kuzaliwa na mdogo wake Julius Nyerere aitwaye Kiboko Nyerere lakini si mtoto wa Julius Nyerere.

Halafu eti Wasira naye akemewe na CCM kwa kukashifu Kanisa Katoliki kwa kumsema Dk. Slaa kwamba alifukuzwa upadri kwa wizi wa fedha za kanisa kama alivyonukuliwa katika vyombo vya habari! Kama ni uongo mbona Dk. Slaa mwenyewe hajajibu lolote hadi leo? Kanisa katoliki litamjibia nini Dk. Slaa wakati sheria za kanisa haziruhusu malumbano yaliyo nje ya Bwana? Na tena limeshaachana naye? 

Mimi binafsi linaliheshimu sana Kanisa, lakini tuseme ukweli, uliwahi kusikia lini, Kanisa Katoliki likamtangaza mtumishi wake anapokengeuka maadili? Lenyewe likishamhukumu kwa sheria zake, linaachana naye kimya kimya. Hivi huyu mwandishi na wengine wanaoshadadia, hawajawahi kusikia japo tuhuma za mapandri kuwa na watoto? Lakini umewahi kusikia wanatangazwa na Kanisa? Lakini walioshindwa kumtunza kondoo wa bwana wakaachana na upadri hawapo?

Lakini hebu nimuulize huyu mwandishi kama akiweza anijibu kupitia safu nyingine, Je, ni kweli Lusinde alitukana au kuongopa aliposema jukwaani kwamba Dk. Slaa ameachana na upadri na sasa akiwa na umri wa zaidi ya miaka 69 ana mchumba na tena mchumba mwenyewe ameshazaa naye? Kha! eti ni uchonganishi, kwani kweli kuna ndugu wa Dk. Slaa asiyejua hayo!

Kuhusu kwamba, CCM ilitumia mabilioni ya fedha kuwarubuni wananchi wa Arumeru Mashariki wasiichague Chadema inaonyesha mwandishi alivyo na  mapungufu ya kuwaza, maana angekuwa ametiza kuwaza vizuri angeona jinsi gani Chadema walivyotunia fedha nyingi kuwarubuni wananchi wa jimbo hilo wasiichague CCM.

Ndahani huyu hakuwepo jimboni! Yaani hajui kama siku zote za kampeni Chadema walitumia helkopta ya kukodi kwa mabilioni ya fedha kiasi kwamba hadi siku ya kupiga kura helkopta hiyo ilikuwa inapiga misele angani! ilikuwa inatumia maji au mafuta ya bure bileshi kutoka kwa David Cameron wa Uingereza? Nadhani jibu ni kwamba ilikuwa inatumia mafuta ya fedha za jasho la walipa kodi ambazo Chadema hupewa ruzuku na serikali au siyo?

Lakini anachoshangaza zaidi mwandishi huyo, ni hodari kama Chadema kupekua matumizi ya wengine lakini mbona hakuweza kutaja fedha zilizotumiwa na Chadema kuwalaghai wanachi wasiichague CCM, wawachague wao.

Jamani uchaguzi wa Arumeru umeshapita, la msingi tugange yaliyopo na yajayo, maana ni upumbavu mbuzi kulia katika gunia, Tanzania ni nchi yetu wote na kila Chama kikiwemo CCM kinayo haki ya kupendwa na kuchaguliwa ili kitawale.

Tatizo la ugonjwa walionao  watu wa Chadema ni kudhani kuwa wao ndiyo wenye fikira pevu na sahihi, wakiona wenye msimamo tofauti na wao huwaona kama hawajui kufikiri, wamekuwa wakidhani kwamba mabadiliko ni kwa kuiacha CCM hata kama bado inapendwa! wanakuwa kama wanafunzi, wanapogoma kula maharage chuoni kwa kuyachoka wao, wanataka kila mwanafunzi asiyale hata ambaye chakula hakishuki bila kuona.

1 comment:

  1. CCM wameonesha ukomavu kweli hao jamaa ni baba na wazazi wa SIASA za hapa BONGO. Kwa kauli ya kiungwana kabisa Katibu Mwenezi alikiri kukubali.Pamoja na mapungufu LUKUKI wanayokiundia CHAMA. Wapongeze basi japo kauli na uungwana wa NAPE wa kukubali matokeo kiungwana

    ReplyDelete

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages