.

MILLYA 'AJIVUA GAMBA',AJIPELEKA CHADEMA

Apr 17, 2012

CCM yampongeza, yasema bado kijana anao muda wa kujifunza mengi.
Millya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepongeza uamuzi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) James Ole Milya kujiondoa CCM na kujipeleka CHADEMA.


Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati na njia tofauti na viongozi wa CCM wakiwemo Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye na Katibu Mkuu wa UVCCM Martine Shigella, mara baada ya kupata habari rasmi za Millya kujivua uanachama wa UVCCM na kwenda CHADEMA.


"Uamuzi wa Millya tumeupokea katika hali ya kawaida na tunampongeza kwa ukomavu wake wa kisiasa kwa kuwa kujiuzulu kwake wadhifa wake wa Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Arusha ametekeleza maamuzi ya NEC ya kujivua gamba", alisema Shigella alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye aliyeko nje ya Nchi, akieleza msimamo wake kupitia mtandao wa facebook, alisema,  binafsi anampongeza Millya kwa uamuzi wake kwani umelenga kukisaidia Chama  kwa sababu alikuwa mzigo kwa sababu ya mwenendo wake kisiasa.


Habari ulizopata mtandao huu ni kwamba, safari ya Millya kwenda Chadema aliianza rasmi Ijumaa iliyopita kwa kwenda Kilimanjaro, nyumbani kwa Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe.


Inadaiwa nyumbani kwa Mbowe, Millya alitoa masharti ya kuhamia Chadema akitaka aandaliwe wadhifa, lakini Mbowe akamtolea nje akisema, "huna watu wengi nyuma yako" ungekuwa nao tungekufikiria lakini kwa ulivyo sasa hatuwezi kukupa wadhifa wowote ukipenda karibu tu kama mwanachama" kilisema chanzi cha habari zetu.


Akizungumza wakati akikaribishwa rasmi ndani ya Chadema kwa uchache Millya amesema ameamua kuhamia Chadema kwa sababu ameona kwamba akiwa ndani ya CCM malengo yake hayataweza kutimia.


Baadhi ya wadadisi wa masuala ya siasa wamedai kwamba, Millya anayedaiwa kuwa kijana wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amechukua hatua hiyo baada ya kuona kwamba kambi alimo inazidi kudidimia katika kusaka nafasi ya juu ya urais.


Hali ya kudidimia huko inadaiwa kujitokeza hasa baada ya CCM kushindwa uchaguzi wa Arumeru Mashariki uliopita ambapo inaelezwa kwamba mgombea wa CCM Sioi Sumari alikuwa ameshinikizwa na kambi yao (kina-Millya) kugombea ili kupima upepo kama kambi hiyo ina nguvu za kutosha kung'ara kwenye kinyang'anyiro cha urais 2015.


Isitoshe Millya amechukua uamuzi huo, ikiwa ni siku chache baada ya kuenguliwa kugombea ubunge wa Afrika Mashariki kwa tiketi ya CCM, katika kinyang'anyiro kinachomalizika kwa uchagfuzi kufanyika  leo mjini Dodoma.
Salamu za Nape kupitia 'face book'0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช