.

MAANDALIZI MPAMBANO WA SIMBA NA AL AHLY YAKAMILIKA, AL AHLY KUTUA KESHO DAR

Apr 25, 2012


Maandalizi ya timu ya soka ya Simba kwa ajili ya kukutana na klabu ya Al Ahly Shandy kutoka Sudan katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF), Jumapili hii, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, yamekamilika.
       Taarifa iliyotolewa leo na msemaji wa timu hiyo, Ezekiel Kamwaga, imesema kutokana na kwamba mechi hiyo itakuwa ya kimataifa, Simba imepanga viingilio ambavyo kila mwananchi ataweza kuvimudu.
       Kamwaga amevijana viingilio hivyo kuwa vitakuwa kama ifuatavyo;-
 Viti vya bluu na kijani itakuwa Sh. 5,000, Rangi ya Chungwa Sh, 10,000, VIP C 15,000, VIP B 20,000 na VIP A 30,000. 
     Amesema tiketi zitauzwa siku ya Ijumaa, katika maeneo yafuatayo, Big Bon, Benjamin Mkapa, Stears Mjini, Mbagala Dar Live, OilCom Buguruni, Tandika Mwembeyanga, Ubungo Oilcom, Mwenge Bus Stand, BP Mwananyamala na Gapco Ukonga
     Kwa mujibu wa Kamwaga klabu imepokea maombi mengi kutoka kwa wanachama na wapenzi wake kutoka mikoani na ingeomba kwamba wale wanaotaka kuja kutazama mechi hii kwa makundi kutoka mikoani, wawasiliane mapema na uongozi ili wanunuliwe tiketi zao mapema na kuongeza kuwa Simba SC imechapa tiketi za kutosha na ingependa wapenzi na wanachama wake kujitokeza kwa wingi kwenye pambano hilo.
     "Wana Simba wote wanaombwa kuja uwanjani wakiwa wamevalia mavazi yao ya rangi Nyekundu na Nyeupe ili uwanja mzima upendeze kwa rangi hizo", alisema Kamwaga. 
      Pia Kamwaga alitoa mwito kwa vyombo vya habari kuisaidia Simba na Tanzania kwa kuelekeza nguvu zao katika uandishi wa taarifa ambazo zitaisaidia timu hiyo kusonga mbele na si kuondoa morali au kusababisha watu wasiende uwanjani.
       "Simba ni timu pekee kutoka katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliyobaki katika michuano yote ya kimataifa inayosimamiwa na CAF na kubwa zaidi ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania waliobaki katika michuano ya kimataifa na hivyo wanabeba bendera ya taifa kokote kule waliko", alisema.  
     Alisema Al Ahly wanatarajiwa kuwasili kesho saa saba mchana kwa ndege ya Ethiopia Airlines. 
      Kwa mujibu wa Kamwaga ,waamuzi na Kamishina wa mchezo wamepangwa kuwasili Ijumaa (keshokutwa) wakitokea nchini Swaziland na Rwanda.
       Pia Simba wametoa shukurani walizoziita za namna ya kipekee kabisa, kwa serikali kutokana na uamuzi wake wa kuruhusu Wekundu wa Msimbazi kufanya mazoezi katika Uwanja wa Taifa kujiandaa na mechi hii muhimu.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª