.

UNAIJUA HISTORIA YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR? HII HAPA

Apr 25, 2012


MKATABA, HATI NA MAMBO 11 YA MUUNGANO
Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964, Zanzibar.
     Ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Aprili 26, 1964, na Aprili 27, 1964 viongozi hao walikutana katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Dalaam kubadilishana hati za Muungano.
    Sheria za Muungano ilitamka kwamba, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zililazimika,  kuwa dola ya Jamhuri kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, jina ambalo lilibadilishwa Oktoba 28, 1964 na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia sheria ya Jamhuri ya Muungano, sheria namba 61, ya mwaka 1964.
     Msingi wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ni Hati za Muungano za Mwaka 1964.
     Hati za Muungano zilitiwa saini na Nyerere na Karume, Aprili 22, 1964 na hapo Tanganyika na Zanzibar kuwa dola moja kwa misngi inayotambulika kimataifa. Baada ya kuungana, Mwalimu Nyerere alikuwa rais wa kwanza na Karume alikuwa makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
      Aprili 26, 1964, bunge la Tanganyika lilipitisha sheria za Muungano, ambazo baadayezilithibitishwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar.
      Mnamo Aprili 27, 1964 waasisi wa Muungano walibadilishana Hati za Muungano na wajumbe saba wa Baraza la Mapinduzi waliapishwa kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Watanganyika na Zanzibar ambao ni Amani Karume, Kassim Abdallah Hanga, Abdulrahman Babu, Hassan Nassor Moyo, Aboud Jumbe, Hasnu Makame na Idris Abdul Wakil. Kati yao, Aboud Jumbe na Hassan Nassor Moyo wangali hai.
     Katiba ya muda ya mwaka 1965 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianisha mambo 11 ambayo yalikubalika kuwa ni ya Muungano ambayo ni; Katiba na Serikali ya Muungano, Mambo ya nchi za nje, Ulinzi, Polisi, Mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari, Uraia, Uhamiaji, Mikopo na Biashara za nje, Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa Tanzania unaosimamiwa na idara ya forodha, Bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu.
      Katiba ya muda ya mwaka 1965 ilianisha utawala wa serikali ya mfumo wa chama kimoja, TANU kwa Bara na ASP kwa Zanzibar. Katiba hii, ilizingatia misingi ya makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 na sheria za Muungano wa Tangayika za Zanzibar.
      Katiba hiyo ilianisha serikali mbili, uwakilishi wa Zanzibar katika bunge la Muungano ikiwa na mamlaka juu ya mambo yote ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano kwa upande  wa Tanganyika. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa na mamlaka juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano yahusuyo Zanzibar.
       Hata hivyo mambo ya Muungano yaliongezwa kutoka 11 hadi 22 kutokana na mahitaji ya ndani ya nchi pamoja na mabadiliko yaliyokuwa yanaendelea kutokea ulimwengini baada ya Muungano.
       Mwaka 1985, jambo la 12 linalohusu sarafu na fedha kwa ajili ya malipo na kurahisisha usimamizi wa fedha za kigeni na benki katika Jamhuri ya Muunagno wa Tanzania, liliingizwa.
     Kufuatia kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967, mambo matatu ya Muungano yaliyongezwa, ambayo ni leseni za viwanda na takwimu; elimu ya juu; na usafirishaji wa anga.
     Mwaka 1968, mambo ya maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya magari na ama ya petroli na aina nyingine za mafuta au bidhaa na gesi asilia yaliyongezwa kwenye orodha hiyo.
Aidha mambo ya Muungano yaliendelea kuongezeka hadi kufikia 21 kufuatia kuvunjika kwa iliyokuwa  Jumuiya ya Afrika Mashariki.
     Mwaka 1992 kufuatia mabadiliko ya mfumo wa siasa nchini suala la 22 la uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana navyo liliongezwa kwenye orodha hiyo.
      MJADALA KUHUSU MUUNGANO
Katika miaka hivi karibuni kumekuwa na mijadala mbalimbali kuhusiana na muundo wa Muungano, baadhi wakitaka uwe wa zaidi ya serikali mbili, wengine serikali moja, wapo wanaotaka Tanganyika iwe kivyake na Zanzibar kivyake.
      Hata hivyo hekima inaonyesha kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unabaki kuwa ni fahari ya Watanzania, kwani mwelekeo wa dunia katika nyanja mbalimbali, mataifa kuungana kwa ushirikiano wa aina mbalimbali ni muhimu kuliko taifa moja kupambana kivyake.
      Urejeaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika mwaka 1977, uwepo wa SADC, ECOWAS, COMESA, na jumuiya nyingine nyingi duniani kote, ni vielelezo kwamba ushirikiano baina ya mataifa ni suala lisilohitaji mjadala.
       Ieleweke kwamba hakuna ushirikiano usio kuwa na matatizo kama ilivyo kwa Muungano wa Tanzania, vivyo hivyo muungano mwingine kama vile ya United Kingdom (UK), Uingereza na United States of America (USA) kwa maana ya Marekani na United Arabs Emirate (UAE), nayo ina matatizo, lakini hata mara moja mjadala juu ya matatizo hayo siyo kuvunja ushirikiano bali kutatua na wale wanaotaka kuvunja hushughulikiwa ipasavyo.
      "Matatizo ya Muungano kama wa UK ni mabaya zaidi, na hata UAE hawana ahueni, ila wanajua kwamba Muungano wao ni lazima. Wamarekani wanapambana na watu wenye mawazo haya ya kuvunja miungano kwenye majimbo ya Alaska, Hawaii na Texas na mwishowe wameamua kuweka kambi kubwa ya jeshi la nchi kavu Texas; utitiri wa kambi za anga Alaska; na vituo vikubwa kupindukia vya majini kule Hawaii. Hivi, hawa mabingwa wa demokrasia wanapoamua kulinda nchi yao namna hii, unafikiri ni wajinga? Walimwaga damu na waliyanunua majimbo haya na wamepitia shida kubwa, ndiyo maana leo wanajidai," anaandika mchangiaji katika mjadala kuhusu Muungano.
        Ni vyema Watanzania wakati huu wa kusheherekea miaka 48 ya Muungano, kila mmoja akajisikia ufahari wa kuwa na kitu kizuri kilichoasisiwa na Waafrika wenyewe na kudumu kwa umri huo.         Mawazo ya kubaguana kwa sababu zisizo na msingi, pengine kukidhi matakwa na wakati kama vile ya kibinafsi na kisiasa, yasipewe nafasi kuisambaratisha nchi. Chambilecho wahenga, umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.

2 Comments:

Anonymous said...

muungano wa tanganyika na zanzibar ndo muungano pekee uliodumu kwa muda mrefu sana swala la msingi ni kuangalia matatizo ya muungano huo na kuyatatua na si kubomoa

Denice samson said...

Tunahitaji amani nzuri
Kutokana huo muungano

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ยช