Breaking News

Your Ad Spot

Apr 20, 2012

HOJA YA ZITTO YA KUTAKA WAZIRI MKUU PINDA, APIGIWE KURA YA KUTOKUWA NA IMANI NAYE YAKOSA SAPOTI YA KANUNI ZA BUNGE

Spika Anna Makinda
NA MWANDISHI WETU, DOM
Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema hoja ya kutaka kumpigia kura ya kutokuwa na imani Waziri Mkuu Mizengo Pinda, inayokusudiwa kupelekwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini ,Zitto Kabwe (Chadema), ni batili na haina nguvu kwa kuwa haijakidhi matakwa ya kanuni.
Amewataka wabunge kuzisoma kikamilifu kanunzi zinazohusiana na hoja hiyo.
Wakati Spika Anna akieleza hivyo, wabunge nao wamesema wana imani na utendaji kazi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na wasingepanda kumwondoa katika wadhifa huo, lakini tatizo kubwa ni mawaziri wake.
Pia, wamesema hoja ya kutaka kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye, inalenga kumshinikiza kuwawajibisha mawaziri wanaotuhumiwa kwa vitendo vya wizi na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Wakijadili taarifa za Kamati za Hesabu za Mashirika ya Umma, Serikali za Mitaa na Serikali Kuu, wabunge waliwashutumu mawaziri kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kiasi cha wengine kwenda mbali zaidi kwa kuwatuhumu kuwa mawaziri wengi ni wezi na kwamba, wamekuwa wakijali maslahi binafsi kuliko ya wananchi wanaowaongoza.
Mawaziri waliokuwa wakishutumiwa na kutakiwa kuachia ngazi ni Mustafa Mkullo (Fedha), Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara), George Mkuchika (TAMISEMI), Omar Nundu (Uchukuzi), ambapo wabunge waliwataka kuachia ngazi.
Kutokana na tuhuma hizo, Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini-CHADEMA), alitoa pendekezo la kuwataka wabunge 70 kusaini ili kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na waziri mkuu.
Habari zilizopatikana bungeni jana zimesema wabunge 62 kati 70 wanaotakiwa, wamesaini pendekezo hilo huku wanne wakitoka CCM na mbunge pekee wa UDP, John Cheyo ndiyo hajasaini.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana, Zitto na Deo Filikunjombe (Ludewa-CCM), ambao ndiyo wanaratibu shughuli hiyo, walisema tatizo kubwa la wabunge si Waziri Mkuu Pinda bali mawaziri wasio waaminifu.
Zitto alisema tayari kazi ya kukusanya saini inaendelea na wana imani hadi kufikia leo jioni wangekuwa wamekamilisha idadi ya 70 kama kanuni inavyosema.
Amesema wabunge wa vyama vyote wamesaini ispokuwa UDP na kwamba, uongozi wa CUF umetoa maelekezo maalumu kwa wabunge wake kusaini.
Alisema miongoni mwa wabunge waliosaini wanne wanatoka CCM na kwamba, hoja hiyo ni ya wabunge wote bila kujali itikadi za vyama na lengo ni kutengeneza Bunge la utendaji badala ya kulalamika.
Iwapo hoja hiyo itapitishwa na Bunge, Pinda atakuwa Waziri Mkuu wa kwanza kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye.
Zitto amesema kuwa wanatarajia kuwasilisha hoja hiyo kwa Spika wa Bunge, Jumatatu kwa ajili ya hatua zaidi.

1 comment:

  1. watanzania wako makini tunachojifunza toka kwa hawa ndugu zetu CDM wanasema saana na wanapojenga hoja harakaharaka utaona kama kweli ukitulia kutafakari na hasa waliyoyasema yakitolewa ufafanuzi mara zote wanakuwa wamekosea na hukaa kimya kabisa . Sijui ndo kusema kweli hawaelewi au kusomasoma kwao basi kutaka kututumia watanzania wengine tuchukue maamuzi yatakayowanufaisha wao?? binafsi nawastukia

    ReplyDelete

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages