Na Rose Jackson,Arusha
WANANCHI zaidi kutoka kata ya Lepurko Wilayani Monduli Mkoani Arusha wanaokabiliwa na ukosefu wa maji hivi sasa watanufaika na mradi wa maji ya bwawa la kisasa linalojengwa katika kijiji cha Nanja Wilayani humo.
Bwawa hilo pia litasadia mifugo zaidi ya elfu ishirini kupata maji na kupunguza kuenea kwa magonjwa ya mifugo katika maeneo hayo.
Kwa mujibu wa wananchi hao walikuwa wakitembea mwendo wa kilomita zaidi ya kilomita zaidi ya kumi na tano kutafuta bidhaa hiyo adimu katika eneo hilo la wafugaji wa kimasai.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa kijiji cha Nanja eneo linakojengwa bwawa hilo Tingide Shamburi alisema kuwa bwawa hilo linajengwa na kampuni inayokarabati barababara ya Arusha Minjingu ya Sogea Satom ya nchini Ufaransa.
Alisema kuwa tatizo la kufuata maji katika maeneo ya mbali pia limekuwa likichangia kuenea kwa magonjwa ya mifugo na kusababisha wafugaji kupoteza mifugo yao .
Tingide aliongeza kuwa wanawake wamekuwa wakijeruhiwa na wanyama nyakati za usiku wakati wakifuata maji katika vijiji vya jirani katika eneo hilo lililopo karibu na hifadhi taifa.
Aidha aliwashukuru wahisani hao kwa kuamua kuwasaidia kuondokana na tatizo hilo aambalo limekuwepo katika maeneo yao kwa miaka mingi.
Alisema kuwa kwa mujibu wa wataalamu bwawa hilo litadumu kwa muda mrefu kutokana na kuwekewa kitambaa maalumu katika sakafu yake ili kutoruhusu maji kupotelea ardhini.
Kwa upande wake afisa uhusiano wa kampuni SOGEA SATOM ya nchini Ufaransa Jamal Nassoro Addi alisema kuwa bwawa hilo litagharimu shilingi miloni mia moja za kitanzania na litakamilika katika kipindi cha wiki mbili zijazo.
Addi aliongeza kuwa kampuni yake iliamua kutoa msaada kwa wananchi kama sehemu ya kuonyesha utu.
“Kimsingi sisi hatukuwa na wajibu wa kujenga bwawa hili katika mkataba wetu wa ukarabati wa barabara ya Arusha Minjingu lakini sisi kama kampuni tuna sera ya kujitoa kwa ajili ya matatizo ynayowakabili binadamu wenzetu”alisema Addi.
Alisema zaidi ya msaada huo pia wananchi wa vijiji hivyo watapata hasa zile ambazo hazihitaji wataalamu kama sehemu ya kuwawezesha kupata kipato.
Aliongeza kuwa pia kampuni hiyo inaendesha pia mradi wa afya kwa kugharamia utoaji wa elimu ya ukimwi kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo pamoja na wananchi wa vijiji ambavyo barabara hiyo inapita.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269